31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

NIYONZIMA AFUNGUKA KINACHOMBAKISHA TANZANIA

NA CLARA ALPHONCE

MASHABIKI wengi wa soka Tanzania wanaamini kiungo Haruna Niyonzima, amekomaa Tanzania kwa kuwa anavuna fedha nyingi, lakini mwenyewe amefunguka kuwa mazingira rafiki ya kuishi na kufanya kazi ndiyo hasa yanamfanya asitamani kuondoka.

Niyonzima ambaye ni raia wa Rwanda, amedumu katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa miaka sita, baada ya kusajiliwa kwa mara ya kwanza na Yanga mwaka 2011, akitokea APR ya nchini kwao.

Baada ya kujiunga na Yanga, kiungo huyo aliichezea kwa miaka mitano na kuisaidia kushinda taji la Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne, kabla ya msimu uliopita kuikacha na kujiunga na Simba.

Usajili wake Simba ulizua sokomoko miongoni mwa mashabiki wa Yanga, ambao baadhi walichukua uamuzi wa kuichoma jezi namba nane iliyokuwa ikitumiwa na kiungo huyo wakati anaitumikia timu yao.

Akizungumza na MTANZANIA, Niyonzima alisema amani iliyoko Tanzania na upendo walionao wananchi wake vimekuwa vikimfanya ahisi kama yuko nyumbani kwao Rwanda.

“Nilipata ofa nyingi nje ya Tanzania kwa ajili ya kwenda kucheza soka, lakini sikutaka kwenda kwa kuwa hapa ninaishi vizuri sana na familia yangu.

“Nikitaka kwenda nyumbani nakwenda na narudi vizuri, jambo hili limenifanya nishindwe kabisa kuiacha hii nchi,” alisema Niyonzima.

Niyonzima alisema mpango wake ni kuhakikisha anaendelea kuishi Tanzania hata baada ya kutundika daluga.
“Mafanikio mengi ya soka nimeyapata nikiwa hapa, si kwamba mimi ndiye mchezaji mzuri kuliko wote, hapana, wapo wengine wengi zaidi yangu, lakini Mungu ndiye anapanga yote.

“Nimepanga hata baada ya kuachana na soka niendelee kubaki hapa, kwani mimi Tanzania ni nchi ya pili baada ya Rwanda nilikozaliwa,” alisema Niyonzima.

Ukiachilia sababu hizo, kiungo huyo inadaiwa ana uswahiba na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, ambaye alifanikisha usajili wake katika klabu hiyo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles