23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

NIMEKUKUMBUKA DK. SLAA

NIKIAMBIWA nitaje mwanasiasa mmoja aliyekuwa au aliyenivutia mpaka nikaipenda siasa kwa kiwango kikubwa basi bila shaka wala kusitasita nitamtaja Dk. Wilbroad Slaa, nilimpenda mwanasiasa huyu kwa jinsi ambavyo alivyokuwa na uwezo mkubwa wa kuelezea masuala nyeti ya Taifa pasi na kuwa na woga wowote, hata nyakati zipite kiasi gani kila nitakapoulizwa swali la mwanasiasa yupi aliyenivutia nikaipenda siasa kwa kiwango cha juu nitajibu kuwa ni Dk. Wilbroad Slaa.

Pamoja na kuwa sikuvutiwa na namna alivyokengeuka kipindi cha uchaguzi bado hilo halibadilishi mimi kumkubali na hata kama ningeulizwa swali kama nikitaka kuingia kwenye siasa nani ningependa awe kocha wangu (mentor) jibu lingekuwa ni yeye.

Kwa nini nimemkumbuka Dk Slaa?

Mazingira ya siasa kwa kipindi hiki yamenifanya nimkumbuke mwanasiasa huyu, kwa imani yangu hiki ni kipindi tulichomuhitaji Dk. Slaa kuliko kipindi kingine chochote, nasema hivyo kwa sababu kwa kipindi kirefu tumekosa mwanasiasa anayejadili siasa za masuala, pamoja na kuwa Zitto Kabwe anajitahidi sana kwenye suala hili lakini imani yangu inaniambia kuwa bado tulimuhitaji baba yao ambaye alikuwa nduli kwenye masuala hayo, Dk Slaa alikuwa jasiri, Dk alikuwa anaweza kujenga hoja, Dk. Slaa alikuwa anaweza kuwasilisha mada na kuushawishi umma kwa kile alichotaka tukielewe na kukiamini lakini nasikitika kuwa vitu hivyo siwezi kuvipata tena, nasema siwezi kuvipata tena kwa kuwa hivi sasa hawezi kuzungumzia hali ya kisiasa ilivyo nchini kwa sababu yeye ni mmoja kati ya watu waliosababisha leo hii tukafika hapa.

Kitu kingine kinachofanya nimkumbuke mwanasiasa huyo ni kila nnapokitazama chama chake, Katibu Mkuu aliyemrithi anaonekana kuvaa viatu visivyolingana na mguu wake, yawezekana vikawa (size) sawa na mguu wake lakini kwa sababu mtu  aliyemrithi alikuwa na mguu mpana viatu hivyo vinampwaya, leo hii sioni hatua za chama hicho kumtafuta mwanachama wake, Ben Saanane, angelikuwapo Dk. nafikiri zingefahamika mbivu na mbichi.

Kwa hali ilivyo sasa hivi hapa nchini nilifikiri wanasiasa wangekuwa  na ajenda nyingi za kuwaelezea wananchi lakini imekuwa sivyo sasa sijui labda mimi ndio niko nyuma ya muda, labda siasa zile za Dk zimepitwa na wakati maana niliona mahali kada mmoja wa chama cha upinzani ameandika siasa za harakati zimepitwa na wakati sasa hivi ni siasa za madaraka.

Nilitamani kumuona Dk. Slaa akijaribu kupambana na kauli ya Rais juu ya kuzuia vyama vya siasa kufanya siasa mpaka 2020, nilitamani kumsikia Dk. Slaa akizungumzia hali ya uchumi ilivyo sasa hivi hapa nchini, nilitamani kusikia akikielezea msimamo wa chama chake dhidi ya masuala kadha wa kadha lakini nasikitika kuwa sitamsikia Daktari akizungumza juu ya hayo kwa sababu Dk. hayupo tena kwenye ulingo wa siasa, hivi sasa na yeye ni mtoa maoni kama wananchi wengine, hayupo ulingoni na yeye kawa mtazamaji.

Wapo watakaohoji kwa nini nimkumbuke msaliti lakini ninachokifahamu ni kuwa hakuna mwanadamu aliyemkamilifu na ukilifahamu hili ni rahisi kuyaheshimu na kuyaenzi yale aliyoyafanya vyema na zile kasoro zake kuzichukulia kama sehemu ya ukamilifu wa ubinadamu.

Japo ulinigeuka kipindi cha uchaguzi na kwenda tofauti na kile ulichoniaminisha siku zote lakini nimekukumbuka daktari, sema kitu roho yangu ipate kutulia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles