31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NDOA YA MITALA YA KISIASA INAYOITATANISHA UINGEREZA

INAWEZEKANA usiwe mfano mzuri kulinganisha mchakato wa Uingereza kujitoa katika jumuiya ya Ulaya (EU) na ndoa ya mitala lakini kuna mkanganyiko unafukuta, kwa baadhi ya himaya zilizoko chini ya Dola ya Uingereza zinazotumia mchakato huo kuvuta kamba ili kutimiza matakwa yaliyobinywa kwa miaka mingi.

 

‘United Kingdom’ inaundwa na England, Scotland, Wales na Ireland Kaskazini ikiwa na watu milioni 64 na ushei wengi zaidi wakiwa England (milioni 53), waliosalia wanaishi katika maeneo mengine yanayojumuishwa katika dola hiyo. Kinachofananisha mchakato wa Uingereza kujitoa EU na ndoa ya mitala ni dhamira ya Scotland kujitenga iliyoibuka tena hivi karibuni kwa kujadiliwa kwa hisia kali bungeni, wakati Uingereza ikijiandaa kuanzisha rasmi mchakato wa kujitoa EU unaotarajiwa kukamilika mwaka 2019.

 

Wakati ‘talaka’ ya EU ikijadiliwa Scotland iliyoshindwa ‘kutalikiwa’ mwaka 2014 inachagiza nia yake ya kujitenga na Falme ya Uingereza huku Bunge la Uingereza likipitisha Muswada wa Matumizi wa Ibara ya 50 inayosimamia mchakato wa kujitoa.

 

Kitakachofuatia ni kuundwa rasmi kwa sheria ya kusimamia mchakato wa kujitoa inayompa mamlaka Waziri Mkuu Theresa May kuanzisha rasmi majadiliano ya vipengele vinavyohusika baina ya Uingereza na jumuiya hiyo. Bunge lilikubaliana kwa kauli moja juu ya uendeshaji makubaliano hayo ya kujitoa kwa mustakabali wenye tija kwa taifa hilo, kwamba kwa kila hatua Serikali ya Waziri Mkuu lazima ipate idhini baada ya kuripoti maendeleo ya mchakato.

 

Kwa kuwashiwa taa ya kijani kuanzisha mchakato huo Waziri Mkuu May amejipanga kuanza utekelezaji wakati huu Mwezi Machi unapoisha. Ibara ya 50 inayotajwa ni mpango mkakati uliowekwa kwenye utaratibu wa EU kwa nchi yoyote inayotaka kujitoa uanachama kutokana na makubaliano yaliyofikiwa Lisbon mwaka 2009 na kuridhiwa na wanachama wote, kabla ya makubaliano hayo hakukuwa na mchakato uliosimikwa wa namna ya kujitoa uanachama.

 

Kwa mujibu wa Kipengele hicho mwanachama anayetaka kujitoa analazimika kutoa taarifa rasmi kwa baraza la umoja huo, ili kuanzisha mchakato wa majadiliano uliopewa miaka miwili hadi kuafikiana misingi kamili. Ili kujitoa asilimia 72 ya wanachama wote wanapaswa kuridhia makubaliano yaliyoafikiwa, lakini pia lazima ipigwe kura ya kuridhia na wabunge wa Bunge la Ulaya (MEPs). Kwa hiyo Uingereza inawajibika kuitaarifu EU ili kujipimia miaka miwili ya mchakato, ingawa Serikali ilitaka kulisimamia jambo hilo kwa mamlaka yake pekee lakini iliwekewa zuio katika Mahakama Kuu ikalazimika kuwasilisha muswada bungeni ambao uliridhiwa na pande zote mbili za Bunge la Taifa hilo.

 

Baada ya kupokea taarifa rasmi ya kujitoa Baraza Kuu la EU litakutana mwezi ujao (Aprili) kuidhinisha Kamisheni yake kuanzisha mjadala na Uingereza. Mjadala rasmi utaanza mwezi Mei na kukamilishwa Oktoba 2018 kwa idhini ya wanachama waliosalia wa EU, utakaofikia hitimisho Machi 2019 ili kutoa fursa kwa mabunge ya nchi wanachama, Baraza la Ulaya na Bunge la Ulaya kupiga kura kuidhinisha maridhiano hayo ambayo yakiafikiwa Machi 2019 Uingereza itakuwa imejitoa rasmi kwenye jumuiya hiyo.

 

Hata hivyo changamoto kadhaa zinatarajiwa kuugubika mchakato huo ikiwamo Uingereza kutaka kusimamia makubaliano yake ya kibiashara na nchi nyingine wakati mchakato ukiendelea, pamoja na idhini ya raia wa nchi nyingine za EU wanaoishi Uingereza na Waingereza wanaoishi katika nchi nyingine wanachama. Mengine ni pamoja na usalama mipakani, mamlaka ya ukamataji wahalifu, kuhamisha makao makuu ya taasisi za EU yaliyoko Uingereza na malipo ya pensheni za wafanyakazi wa EU zitakazoligharimu taifa hilo pauni bilioni 50.

 

Lakini Uingereza itafaidika na kujitoa kama ikisimamia vyema makubaliano ya kujitoa ikiwamo ruzuku ya EU kwa wakulima wake, sera ya kidiplomasia inayohusiana na vikwazo, uhuru wa makubaliano ya kibiashara na nchi nyingine, bima ya afya kwa Waingereza kwenye mataifa mengine na mikataba ya ulinzi wa mazingira iliyoingia kupitia UN. Ikiwa maafikiano hayatafikiwa baada ya mchakato wa miaka miwili Uingereza itakuwa imeshatoka EU na kuamua matakwa yake yakiwamo ya kibiashara kwa kupitia kanuni za WTO (World Trade Organisation).

 

Licha ya yote hayo lakini kinachofukuta nchini Scotland kinachochagizwa na Waziri Mwandamizi, Nicola Sturgeon  wa chama  cha Scottish National Party (SNP), ni dhamira ya kupiga Kura ya Maoni wakati majadiliano ya kujitoa EU yakiendelea ili makubaliano yatakapokamilika Scotland ijitawale kwa kujitoa kutoka Falme ya Uingereza. Lakini matakwa hayo yamekataliwa na Waziri Mkuu wa Uingereza na kusababisha mkanganyiko miongoni mwa wakazi wa Scotland, asilimia 44 wakiunga mkono kusubiri mchakato wa kujitoa EU lakini asilimia  48 wakipinga ubabe wa Uingereza kuwalazimisha kuendelea kubakia kwenye Falme hiyo kama ilivyofanya  hila na kuzima jaribio kama hilo mwaka 2014.

 

Theresa May anashutumiwa kutosimamia vyema mchakato wa kujitoa EU pia kutoelewa vyema dhamira ya Scotland kujitoa, Waskoti wanavutia kamba kwao kwa kuwakaribisha nchini kwao wanaokerwa na hulka za ubabe wa Falme ya UK wakatumie fursa lukuki zilizokosa watumiaji ili kujiepusha na uhafidhina unaobinya matakwa ya fursa kwa faida ya wachache wanaosimamia mfumo wa Dola ya Uingereza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles