29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

NILIMSIKIA LISSU AKISEMA DIKTETA UCHWARA – SHAHIDI

maxresdefault

Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MRATIBU Msaidizi wa Jeshi la Polisi, ASP Kimweli, amedai alimsikia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, akisema dikteta uchwara ni lazima apingwe kwa nguvu zote kama amefanya utawala wa kijinga, hawawezi kuvumilia utawala mbovu wa kidikteta uchwara, hata kama alichaguliwa kuwa Rais.

ASP Kimweli alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa, alipokuwa akitoa ushahidi wa upande wa mashtaka akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mohammed Salum.

Shahidi huyo alidai maneno ya Lissu aliyotoa Juni 28, mwaka huu,  aliyaona ni ya uchochezi kwa sababu ni mbunge aliyechaguliwa na watu, mwanasheria na kiongozi wa chama, hivyo kuzungumza kwake mbele ya vyombo vya habari, maneno yangesambazwa na kuwa tatizo katika nchi.

Alidai kuwa Lissu alipotoka ndani ya mahakama, alikuwa na kundi kubwa la watu, alifika nalo nje na kuanza kuzungumza.

Kwamba alimsikia Lissu alisema nchi ipo ndani ya giza nene mamlaka ya Serikali mbovu ya kidikteta uchwara yanapaswa kupingwa kwa nguvu zote.

“Dikteta uchwara huyu ni lazima apingwe kwa nguvu zote kama amefanya utawala wa kijinga, hatuwezi kuendelea kuvumilia utawala mbovu wa kidikteta uchwara, hata kama ulichaguliwa kuwa rais ni lazima kila mahali upingwe, hata kama tutapelekwa mahakamani kwa ajili ya kufungwa mdomo tutapambana tutashinda,” Kimweli alidai hayo maneno yalitamkwa na mshtakiwa.

Alidai hakuchukua hatua yoyote wakati Lissu akitamka maneno hayo, kwa sababu alijua ni mtu anatambulika na anaweza kuitwa polisi wakati wowote.

Akihojiwa na Wakili Peter Kibatala kwamba alibaini nini kuhusu dikkteta uchwara lazima apingwe, Kimweli alidai hakumtaja ni nani na wala yeye hakujua ni nani, na kwamba hakuna nchi iliyotajwa na wala hakueleza ni kwa namna gani ipingwe.

Shahidi huyo alidai ni kweli mbunge wa upinzani anaruhusiwa kupinga Serikali iliyopo madarakani kwa nguvu zote, kwa demokrasia na kwa mujibu wa sheria.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 18, 2017 mashahidi wa upande wa mashtaka watakapoendelea kutoa ushahidi.

Lissu anadaiwa kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles