23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

ZANTEL YADAIWA SH MIL 700 ZA PANGO

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zantel Tanzania, imepewa siku saba iwe imelipa zaidi ya Sh milioni 700 za kodi ya pango inazodaiwa na Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Zantel iliingia mkataba wa miaka sita na Manispaa ya Kinondoni kutumia  majengo yake na kukubaliana kulipa Dola za Marekani 45,000, karibu Sh milioni 98 kwa mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za kampuni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, alisema tangu manispaa hiyo iingie mkataba na Zantel mwaka 2009 hadi 2014 ulipomalizika, hakuna vielelezo vyovyote vinavyoonyesha kuna malipo yaliyowahi kufanyika.

Alisema kampuni hiyo imekaa kimya, huku ikiendelea kutumia majengo ya manispaa bila kulipia pango.

“Iwapo siku hizo zitapita bila kulipa, Zantel watatakiwa kulipa kwa riba na kwa muda wote ambao wameendelea kufanya biashara katika majengo hayo,” alisema.

Hapi alisema walifuatilia sababu za kutolipwa kwa fedha hizo kwa kipindi chote hicho na kubaini uongozi wa manispaa haukupeleka risiti za madai (invoice).

“Hoja ya Zantel ya kutolipa fedha hizi, ilikuwa eti manispaa haijawapelekea risiti za madai (invoice), sasa mkurugenzi amezipeleka, wanatakiwa kutulipa malipo yote tangu walipoingia mkataba.

“Katika uchunguzi tuliofanya, tulibaini Mei 12, 2009 kuna malipo ya Dola 45,000 yalifanyika ambayo mfumo wao unaonyesha yalilipwa kupitia akaunti ya benki ya NBC… cha kushangaza kwa upande wa manispaa haionekani kama kuna malipo kama hayo yaliwahi kufanyika na wala hii akaunti haipo, mjiridhishe kama kweli malipo hayo yalifanyika.

“Kama msipofanya hivyo, hatutahesabu fedha zimelipwa na badala yake tutaiweka kwenye deni ambalo mnatakiwa kuilipa manispaa, kutokana na viwango vya thamani ya ardhi katika eneo hili vinaweza kuwa vimepanda, mkurugenzi na timu yako mfanye ukokotoaji kulingana na thamani ya eneo la mraba (square meter) kama itakuwa inalingana na ile iliyopo kwenye mkataba au itakuwa imepanda, basi Zantel itatakiwa kulipa ongezeko hilo kuanzia mwaka 2014 hadi muda huu,” alisema Hapi.

Alisema Januari 31, mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni pamoja na Kampuni ya Zantel, wanatakiwa kukutana ili kuuangalia upya mkataba ulioisha na kuingia mpya ambao utazingatia nafasi ya Serikali kukusanya mapato kwa mujibu wa thamani ya ardhi.

Kutokana na hali hiyo, Hapi ameagiza kufanyika uchunguzi wa kina kwa benki na tawi ambalo malipo ya fedha hizo yalifanyika.

Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu wa Zantel, aliyekaimu nafasi ya Mkurugenzi Joanitha Mrengo, alisema mkurugenzi wa kampuni, Benoit Janin yuko safarini na yeye hawezi kuthibitisha tuhuma hizo.

“Ameondoka leo asubuhi kuelekea Zanzibar, lakini tunatarajia kuwa leo atarudi, hivyo baada ya kikao hiki nitamfikishia huu ujumbe kwa simu, lakini pia atakapofika nitamkabidhi hizi risiti za madai (invoice) pamoja na mwanasheria wetu,” alisema Joanitha.

Akizungumzia suala hilo, Meneja Bidhaa na Mawasiliano wa Zantel, Rukia Mtingwa, alisema suala hilo linafanyiwa kazi ngazi ya menejimenti ili kufikia mwafaka.

“Tumepokea ugeni wa DC Happi, tumemsikiliza na sisi tumeanza kulifanyia kazi kupitia ngazi ya menejimenti yatu, tunataka kuona linamalizika,” alisema Mtingwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles