25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NI MAZOEZI YA AEROBICS AU CARDIO?

Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD.


TUKUBALIANE kabisa kwamba, maneno yote hayo mawili ni ya kuazima. Sina uhakika kama Baraza la Kiswahili limeshatoa tafsiri sahihi na maneno halisi ya Kiswahili yanayobeba maana ya aerobics au cardio. Lakini hata hivyo sina shaka kuhusu matumizi ya maneno haya katika jamii ya watu wanaopenda na kufanya mazoezi. Wengi wetu tunayatumia mara kwa mara.

Tukubaliane pia kwamba, kuna utata kidogo katika matumizi ya maneno haya mawili.  Utata huu upo pia katika matumizi ya maneno haya kwa lugha ya Kiingereza. Je, maneno haya yana maana sawa, au tofauti? Na kama yana maana sawa kwanini yatumike maneno tofauti? Kwa ufupi, maneno haya yanawakilisha vitu viwili tofauti ambavyo vinahusika kuleta mabadiliko yanayofanana. Kwa maana rahisi, maneno haya yanamaanisha kitu kimoja, na hutumika kwa kubadilishana. Mtu mwingine amezoea kutumia cardio wakati mwingine anakuwa amezoea zaidi neno aerobics.

Chukulia mfano mzuri kabisa wa mazoezi ya cardio, kutembea au kukimbia kwa mwendo wa kawaida. Nimesema kukimbia kwa mwendo wa kawaida kutokana na ukweli kwamba kukimbia kwa mwendo wa kasi sana (sprinting) kama mtu anapokimbia mita 100 au 200, hakukidhi vigezo vya kuwa cardio. Hili tutaliongelea kwa undani katika andiko lingine. Mtu anapokimbia kwa mwendo wa kawaida au kwa lugha ya kitaalamu mchaka mchaka, mambo mawili muhimu hutokea. Kasi ya mapigo ya moyo na ile ya kupumua huongezeka na kuwa juu kwa kipindi chote anachofanya mazoezi
Ni rahisi kutambua mabadiliko haya tunapokuwa tunafanya aina hii ya mazoezi. Nia kubwa ya kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo na kupumua, ni kuweza kufikisha hewa ya oksijeni katika chembe hai, hususani zile za misuli ambazo hufanya kazi ya ziada wakati wa mazoezi. Oksijeni hii ndiyo inayowezesha kupatikana kwa nguvu inayotumika wakati wa mazoezi ya cardio au aerobics.

Sasa tumesema vitu viwili, kasi ya mapigo ya moyo na ile ya kupumua, vikiwa na lengo la kupeleka hewa ya oksijeni ya kutosha kwenye misuli. Neno cardio hapa lina maanisha moyo. Limetokana na neno la kilatin ‘kardia’ likimaanisha moyo.  Hii ni kutokana na ukweli kwamba mazoezi ya aina hii huongeza kasi ya mapigo ya moyo.

Lakini pia mazoezi haya huongeza kasi ya kupumua kwa kufanya kazi kwenye mapafu. Nia na madhumuni ni kuimarisha utumiaji wa hewa ya oksijeni. Neno aerobics, limetokana na neno la Kigiriki ‘aerobic’ ambalo maana yake halisi ni  ‘yenye hewa ya oksijeni.’ 

KUTEMBEA NI MFANO MZURI WA MAZOEZI YA CARDIO/AEROBIC

Kwa maana hiyo kama tulivyoona hapo awali mazoezi ya cardio, hali kadhalika yale ya aerobics, huchochewa na uwepo wa hewa ya oksijeni. Fikiria aina zingine za mazoezi ya aina hii-cardio au aerobics. Kuogelea, kucheza dansi, kuendesha baiskeli na mazoezi yote yanayohitaji kufanyika kwa kipindi cha muda fulani, kwa ujumla yanasababisha kasi ya mapigo ya moyo na kupumua kuongezeka kwa muda hivyo kupeleka hewa ya oksijeni katika chembe hai za misuli. Unapokuwa unafanya mazoezi haya unatambua kiurahisi kwamba moyo na mapafu yako vinafanya kazi ipasavyo, tofauti na unapofanya mazoezi kama kunyanyua au kusukuma uzito. Unapofanya mazoezi ya kunyanyua au kusukuma uzito-ambayo si cardio wala aerobics, japo mwanzoni utahisi moyo na mapafu kufanya kazi sana, baadaye utahisi ni misuli ndiyo inafanya kazi zaidi.

Mazoezi kama kunyanyua vyuma, kusukuma mashine, kukimbia mbio fupi kwa kasi kubwa na hata kuvuta kamba, ni tofauti kabisa na mazoezi ya cardio au aerobics. Kitaalamu mazoezi haya hujulikana kama resistance exercises, strength training, weight training au anaerobic exercises. Japo aina Fulani za mazoezi ya aina hii husababisha kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo na kupumua pamoja na utumiaji wa oksijeni haraka haraka, mazoezi haya hayawezi kufanyika kwa muda mrefu hivyo kutokukidhi vigezo vya kuwa cardio au aerobics.

Kwa maana hiyo basi, mazoezi ya cardio au aerobics ni yale yanayosababisha kasi ya mapigo ya moyo, kupumua na matumizi ya hewa ya oksijeni kuongezeka kwa kipindi cha muda fulani. Ili kuweza kufanya mazoezi haya kwa muda huo, mazoezi haya huwa ni ya nguvu kidogo mpaka ya wastani. Mfano, huwezi kukimbia kwa muda mrefu kama utakimbia kwa mbio zako zote. Huwezi kubeba uzito mkubwa kwa muda mrefu. Unapotembea, unaweza kutembea hata kwa saa moja.

 

MAZOEZI YA CARDIO/AEROBICS HUSABABISHA KASI YA MAPIGO YA MOYO NA KUPUMUA KUONGEZEKA ILI KUPELEKA HEWA YA OKSIJENI KWENYE MISULI

 

Kwakifupimazoezi ya cardio au aerobics hutegemeanguvu na mudaunaotumika. Kwa kuwa muda ni muhimu, maana yake ni kwamba nguvu kidogo au ya wastani hutumika ili kuweza kufanya mazoezi haya kwa muda mrefu. 

Mazoezi haya basi hutujengea uwezo wa kufanya vitu au shughuli kwa muda mrefu, kitu ambacho kitaalamu kinaitwa ‘endurance.’ Huwezi kujenga endurance kwa kunyanyua au kusukuma vitu vizito. Wakati mazoezi ya cardio au aerobics yakisaidia kwa kiasi kikubwa katika ufanyaji kazi wa moyo na mapafu, hivyo kutupa uwezo wa kufanya vitendo au shughuli kwa muda mrefu, mazoezi ya kunyanyua au kusukuma uzito huimarisha misuli na mifupa.

Kwa ujumla aina zote za mazoezi ni muhimu katika kudumisha afya na kujikinga na magonjwa

Unaweza kuwasiliana na Dk Mashili kwa ushauri zaidi kupitia 0752255949
Au tembelea tovuti yake www.jamiihealthtz.com

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles