26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ACHENI LUGHA ZA KUUDHI KWA WATEJA WENU

Na FARAJA MASINDE


KUMEKUWAPO na tabia ambayo imekuwa ikifanywa na vijana wanaoendesha pikipiki maarufu bodaboda kwenye maeneo ya miji mikubwa hapa nchini kutoa lugha chafu kwa wateja pindi wanapokataa kutumia vyombo vyao vya usafiri.

Tatizo hili limeendelea kuwa kubwa kadri siku zinavyozidi kwenda ambapo imesababisha baadhi ya watumiaji wa usafiri huo unaoaminika kuwa wa haraka zaidi kuacha kuutumia kufuatia lugha za kuudhi wanazotolewa na bodaboda hao ambao kwa asilimia kubwa bado ni vijana.

Hali hiyo imekuwa ikijitokeza hasa pale abiria anaposhindwa kufikia makubaliano ya bei na mwendesha bodaboda – hapo ndipo lugha za udhalilishaji huanzia zikiwamo za kuudhi.

Wengi huwaita abiria hao wanaoshindwana nao kama watu wasiokuwa na fedha au kusema wana fedha za mawazo jambo ambalo limekuwa likikera wengi kwani hata kwa wale ambao wamekuwa wakipita njia karibu na vyombo hivyo vya usafiri na kulazimishwa kuutumia bila mafanikio pia wamekuwa wakiambulia lugha chafu na maneno makali ambapo kadhia hii hasa imekuwa ikiwakumba zaidi akina dada.

Tabia hii kamwe haina budi kufikia ukomo kwani imekuwa ikiharibu hadhi ya kazi yenu licha ya kwamba si wote mnaofanya hivyo.

Kazi ya kufanya ni kuhakikisha mnakuwa na msimamo kwa wote wanaoenenda kinyume na taaluma yenu hii kwa kuwachukulia hatua ikiwamo kuwaondoa kwenye vituo vyenu lengo likiwa ni kuhakikisha mnakuwa na kijiwe cha watu wenye weledi na kazi yao.

Kwani tofauti na hivi mtaendelea kunyooshewa kidole kama watu msiokuwa na kauli nzuri kwa wateja wenu na hivyo kujikuta kwamba watu wanaukimbia usafiri wenu huku wakiwaweka kundi moja.

Ndio maana kumekuwa na sheria mbalimbali zinazotungwa dhidi yenu ambazo nyie mnasema kuwa zinawakandamiza kutokana tu na kushamiri kwa tabia za baadhi yenu ambazo hazifai kwenye jamii na hivyo kushawishi mamlaka husika kuwaundia sheria kali ambazo ninyi mnaziona kuwa ni kandamizi.

Lakini lengo ni kutaka kuwanyoosha ili muweze kuachana na tabia zisizofaa zinazochochea kuporomoka kwa maadili kwenye jamii.

Binafsi naamini kuwa fani hii ya udereva wa bodaboda ni sehemu nzuri ambayo kwa kiwango kikubwa imesaidia kuondoa makali ya ajira kwa kuchukua kundi kubwa la vijana kutoka katika sehemu mbalimbali nchini, hivyo haitakuwa busara kuona ikiendelea kuharibiwa na watu wachache wasiokuwa na uchungu wa kukosa ajira.

Hivyo, mnapaswa kuacha kutumia lugha za matusi kwa abiria na wapita njia hasa kwenye vituo vya daladala ambapo ndiko mchezo huu umekuwa ukichukua nafasi kubwa kutoka kwa waendesha bodaboda wa vituo hivyo vya mabasi.

Tuna tambua kuwa hali ya upatikanaji wa ajira nchini ni ngumu kwani tunashuhudia wasomi wenye viwango vya juu vya elimu wakihangaika usiku na mchana kusaka ajira hivyo ni vyema mkaikumbatia ajira yenu hiyo kwa kuwa na kauli nzuri kwa wateja wenu hatimaye kuweza kuthaminika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles