23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Ni Lowassa vs Slaa

Lowassa vs SlaaFredy Azzah na Elias Msuya

RIPOTI ya utafiti ya taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza yenye kichwa cha habari, ‘Tanzania kuelekea 2015’, imeonesha kuwa asilimia 47 ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, hawatarejea bungeni katika uchaguzi mkuu ujao.

Utafiti huo ujulikanao kama sauti za wananchi ulifanywa kwa njia ya simu ambapo mwaka 2012 watu waliohojiwa ni 2,000,  mwaka 2013 1,574 na mwaka 2014 watu waliohojiwa ni 1,445.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, asilimia 47 ya wananachi waliohojiwa, walisema katika uchaguzi mkuu wa mwakani  hawatawapigia tena kura wabunge wao wa sasa.

“Watu walisema wabunge wao wametimiza mambo machache tu ama hawajatimiza kabisa hata jambo moja waliloahidi katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita,” inasema sehemu ya ripoti ya utafiti huo.

Asilimia 47 ya watu waliohojiwa katika utafiti wao walisema watawarudisha wabunge wao katika uchaguzi mwakani, huku asilimia tano wakiwa hawana msimamo.

Walipoulizwa juu ya mtu wanayetaka awe mbunge wao, watu watatu kati ya wanne (asilimia 74), walisema moja ya kigezo kitakuwa ni elimu.

Nusu ya watu hao walisema wanataka mbunge wao awe angalau na shahada ya kwanza, wakiamini kuwa kiwango cha elimu ni muhimu ili kiongozi aweze kuwa na maarifa mazuri katika kutimiza majukumu yake.

Suala la pili lilikuwa ni umri kisha suala la maadili, uaminifu na kuaminika kwake, zilikuwa ni sifa nyingine zilizotajwa na wananchi waliohojiwa.

“Watu watatu kati ya wanne waliozungumzia suala la umri, walisema wanataka mbunge ambaye angalau anaanzia miaka 40,” utafiti unasema.

Takwimu zaidi zinaonyesha kuwa, waliosema wataangalia umri ni asilimia 55, ukweli na uwazi pamoja na maadili asilimia ya mgombea ni asilimia 26 na watakaoangalia endapo mgombea kaoa/kaolewa au laa ni asilimia 19.

Ahadi za wabunge

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, kati ya wabunge 239 waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu mwaka 2010, wengi walitoa ahadi lukuki ambazo wameshindwa kuzitekeleza hadi sasa.

Inaonyesha kuwa, wapigakura nane kati ya 10 bado wanakumbuka ahadi zilizotolewa na wabunge wao wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Ripoti hiyo inasema kuwa, asilimia 77 ya ahadi hizo zilikuwa za kujenga ama kukarabati barabara, asilimia 64 kuboresha vyanzo vya maji, asilimia 38 ujenzi wa hospitali, na asilimia 23 ni ujenzi wa madarasa.

“Ahadi hizi ziliendana na mambo yaliyobainishwa na wananchi kama matatizo yaliyokuwa yanaikabili nchi yetu, hii inaonyesha kuwa, wanasiasa wanajua wanachohitaji wapiga kura wao,” inasema ripoti hiyo.

Ukawa yatabiriwa anguko

Wakati Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ukijinoa ili kupambana na CCM kuanzia kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa hadi uchaguzi mkuu 2015, utafiti mpya unaonyesha pigo kwa umoja huo.

Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF na NCCR Mageuzi ulitokana na vuguvugu la kudai Katiba mpya ambapo wajumbe wake walitoka bungeni Aprili 14 wakipinga mwenendo wa bunge hilo lililokuwa na wajumbe wengi wa CCM.

Hivi karibuni viongozi wa Ukawa wametia saini makubaliano saba jijini Dar es Salaam ambayo ni pamoja na kudumisha sera za vyama vyote vinne na kuchukua mambo yanayofanana ili kuvifanya viwe na kauli ya pamoja na kusimamisha wagombea wa pamoja katika chaguzi zote za serikali za mitaa, udiwani, ubunge, uwakilishi na rais wa muungano na rais wa Zanzibar.

Hata hivyo, matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza yaliyotangazwa jana jijini Dar es Salaam yameonyesha, endapo uchaguzi mkuu ungefanywa Septemba, asilimia 47 ya Watanzania wangeichagua CCM huku asilimia 28 wakichagua mgombea wa Ukawa, asilimia 19 wakichagua mgombea siyo vyama na asilimia sita hawajui lolote.

“Matokeo ya Septemba 2014 yanaonyesha CCM inaendelea kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wananchi hasa upande wa bara.

Ripoti hiyo inaendelea kufafanua kutokuwepo kwa mgombea mmoja ndani ya CCM kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hivyo mgombea kutoka chama chochote anaweza kushinda.

“Hiyo inaonyesha kuwa Watanzania bado hawajafanya uamuzi wa mgombea gani anawafaa kati ya waliojitokeza na wanaotajwa kugombea… hivyo uchaguzi utakuwa mgumu,” inasema ripoti hiyo.

Lowassa kidedea

Walipoulizwa kama uchaguzi wa urais ungeendeshwa leo, nani ataibuka na ushindi? Mwaka 2014 mgombea aliyepata kura nyingi katika swali hili ni Edward Lowassa wa CCM (asilimia 13), Mizengo Pinda wa CCM asilimia 12 na Dk. Wilbrod Slaa wa Chadema asilimia 11. Wagombea wengine ni Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF asilimia 6 na Bernard Membe wa CCM asilimia 5.

Hata hivyo ripoti hiyo inasema, kundi waliojibu ‘sijui’ linaonyesha kuwa kubwa kwani mmoja kati ya watu watatu sawa na asilimia 33 wajibu hivyo kwa wagombea watatu wa juu.

Hii inaonyesha kuwa, Watanzania bado hawajashawishika na wagombea na kuweka chaguo lao kuwa wazi. Uwanja huo unaweza kugawanya ushindi wa CCM kwa wagombea kujitoa na kuhamia upinzani,” inasema.

Katika swali lililoulizwa ‘nani atashinda urais’ majibu yameonyesha kuelea huku waliojibu wakionyesha kuvutiwa na wagombea kuliko vyama vyao. Kundi hilo la waliojibu linategemea zaidi ubora wa mgombea.

“Kama kura hizo zitagawanywa kati ya CCM na upinzani, CCM watapata ushindi mwembamba. Itakuwa hatari kwa CCM kama wagombea hao wanaoelea wataupigia upande wa upinzani,” inasema.

CCM chama cha wazee

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa, asilimia kubwa ya watu wanaoiunga mkono Chadema ni vijana chini ya miaka 35 huku wale wa CCM wakiwa ni wenye umri juu ya huo.

“Hii inaonyesha kuwa watu wengi wanaounga mkono Chadema ni vijana na vijana wengi wanatarajiwa kupiga kura,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Utafiti huo unasema hali hiyo kwa siku za usoni inatoa zaidi faida kwa vyama vya upinzani.

Kwa mujibu wa utafiti huo, watu wenye umri wa miaka 35 wanaounga mkono CCM ni asilimia 44,  wenye miaka 35 mpaka 50 ni asilimia 60, na miaka 50 na kuendelea ni asimia 63.

Kwa upande wa Chadema, watu wenye umri wa miaka 35 wanaounga mkono chama hicho ni asilimia 34, huku wale wenye umri wa miaka 35 mpaka 450 wakiwa ni asilimia 24 na wenye miaka 60 na kuendela wakiwa ni asilimia 20.

Slaa ang’ara Ukawa

Ripoti hiyo inasema kuwa, watu waliohojiwa walipoulizwa ni  nani anaweza kusimama kuwakilisha Ukawa, watu wanne kati ya 10, walimtaja Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa.

Watu hao ni sawa na asilimia 41, huku majina mengine yaliyotajwa ni Profesa Ibrahim Lipumba, asilimia 14, Freeman Mbowe asilimia 11, Zitto Kabwe asilimia sita, Tundu Lissu, Maalim Seif Sharf Hamad,  James Mbatia na Augustino Mrema wote wakipata asilimia moja.

Umasikini mzigo kwa Watanzania

Taarifa ya utafiti huo inaonyesha kuwa, watu walipotakiwa kutaja vitu vitatu ambavyo ni tatizo kubwa kwa Watanzania, walitaja umasikini, afya na elimu.

Inasema matatizo hayo yamekuwa yakiwakabili wananchi kwa miaka mitatu mfululizo, kuanzia 2012 mpaka mwaka huu.

Kwa mujibu wa utafiti huo, mwaka 2012 asilimia 49 ya waliohojiwa walisema umasikini ni changamoto kubwa, mwaka 2013 waliotaja umasikini kuwa ni kikwazo ni asilimia 46, na mwaka 24 waliotaja kuwa umasikini ni tatizo ni asilimia 47.

Taarifa ya utafiti inaonyesha kuwa, watu waliosema kuwa elimu ni tatizo mwaka 2012 walikuwa asilimia, mwaka 2013 asilimia 46 na mwaka 2014 idadi yao imeshuka na kuwa silimia 38.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa rushwa imeendelea kuwa tatizo kubwa kwani mwaka 2012 asilimia ya walioona kuwa hilo ni tatizo walikuwa asilimia 24, mwaka 2013 asilimia 29 na mwaka huu idadi yao imefikia asilimia 30.

Uchaguzi bado hautabiriki

Ripoti hiyo inasema matokeo ya utafiti huu uliofanyika Septemba, CCM inaonyesha kuungwa mkono na wananchi wengi wa Tanzania bara, hata hivyo kuna kundi kubwa ambao halijaamua limchue nani na hivyo mtu yeyote anaweza kushinda.

“Hata hivyo haizidi sana vyama vingine vya siasa kama ilivyokuwa huko nyuma,” inasema.

Ripoti hiyo kuwa inaonyesha kuwa, bado vyama siasa havitakiwi kuzorota kwani kuna kundi kubwa ambao bado halijaamua litampigia nani kura katika uchaguzi huo.

“Jambo linaloonekana kwa sasa ni kuongezeka kwa kundi la wapiga kura ambao hawajaamua wampigie nani kura, kundi ambalo ni kubwa kuliko idadi ya wafuasi wa mgombea yoyote.

“Hii inaonekana kuwa Watanzania bado hawajaamua wamchague nani ama hawajashawishiwa na mgomea yoyote kati ya wanaoongoza.

“Hivyo Mgombea yoyote miongoni mwa waliojitangaza au atakayeibuka upya ambaye atawavua na kuwashawishi kikamilifu wapiga kura, anaweza kushinda.

“Mwelekeo wa upigaji kura unaonekana kufuata upenzi wa vyama kwa hiyo swali gumu hapa ni iwapo haiba ya mgombea itashinda upenzi wa chama, uchaguzi utakuwa mgumu na hautabiriki,” inasema ripoti hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

5 COMMENTS

  1. Utabiri wa Lowassa kugombea urais wa JMT na kuibuka Mshindi kupitia CCM 2015, sio jambo la siri wala utafiti wa kisanyansi kama huu, hili tayari limekuwa ni mazungumuzo na mapendekezo ya 86% ya wachangiaji wa hoja kupitia makundii mbalimbali wanapojadiriana ” NANI RAIS AJAE BAADA YA KIKWETE?”

    Siasa ni mchezo mchafu, hasa kwa wanasiasa kuchafuana, na hili ndilo lililo mtokea Lowassa mpaka akajiudhuru Uwaziri Mkuu. Lowassa kama kiongozi hakuwajibishwa, aliwajibika kisiasa na sio Kijinai, kisheria hawezi kuhukumiwa nje ya mahakama ya Tanzania, yeye ni safi kikatiba na kisheria, agombee tumchague na historia ya JMT ijirudie.

    Historia kujirudia nina maana ya kurejea alipojiudhuru Uwaziri Mzee Ally H. Mwinyi na baadae Kupitia CCM akachaguliwa Rais wa JMT, na hii ndiyo watanzania tunavyomuona Lowassa kama Mwinyi mpya, atupe ruhusa tena.

  2. Charles siyo sahihi kulinganisha mazingira yaliyomfanya Al Haj Ali Hassan Mwinyi kujiuzulu Uwaziri wa Mambo ya Ndani na Kashfa ya Richmond iliyomfanya Edward Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu. Mwinyi aliwaajibika kutokana na makosa ya Maafisa wake, hakuhusika kwa kuagiza au kushawishi kuteswa kwa raia waliokuwa mikononi mwa Polisi pale Kigoto Mwanza. Hii ni tofauti na Lowassa, alikuwa ndio Kiongozi mkuu wa kuagiza na kusimamia utekelezaji wa mchakato wote uliopelekea kampuni ya Richmond kupewa zabuni ile ya kufua umeme wa dhararu licha ya kukosa sifa za kiufundi na kizabuni. Pia kama wewe binafsi unamuona Lowassa ni sawasawa na Mwinyi hayo ni maoni yako na unao uhuru wa kuona na kusema hivyo. Lakini si vyema na wala huna haki yoyote ya kusema hayo ni maoni ya Watanzania. Uliyakusanya lini, wapi na kwa utaratibu upi? Acha upotoshaji.

  3. kiongozi mzalendo na mwenye mapenzi mema na watanzania hawezi kupatikana kwa ushabiki wa kivyama.kiongozi mzalendo anapatikana kutokana malezi bora aliyoyapata kutoka kwa wazazi wake,kwa walimu wake,kwa viongozi wake wa kidini na jamii yake inayomzunguka kwa ujumla.kiongozi wa aina hii anaweza kutoka chama chochote kile.viongozi wengi wa kisiasa tulio nao wako kichama zaidi au kibnafsi zaidi.wanatumia lugha nzuri kutulainisha watanzania tuwape huku wakiwa ajenda za siri nyuma yao.
    kama ningepiga kura ya urais 2015 kwa wakati huu,basi ningemfikiria Lowasa kwanza kabla ya hao wengine japo mimi si shabiki wa chama chochote kile cha kisiasa.

  4. mimi nafikiri kiongozi tunayemtaka ni yule ambaye kweli anakerwa na shida zetu watanzania sio wanaojirimbikizia mali na kutaka wapate ili waendelee kuchota rasilimali zetu kwa maslahi yao.hivyo ni vizuri tukajiuliza kwanza kiongozi ajae awe wa aina gani? na wala sio kuanza kuwapigia Debe mafisadi ili waendeleze ufisadi wao hapa nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles