24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

Wapiga kura wanaoelea waitisha CCM

Wawakilishi boraElias Msuya na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

KATIBU wa Itikadi na Uendezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema licha ya matokeo ya utafiti wa taasisi ya Twaweza kuonesha kuwa chama hicho kinaongoza dhidi ya wapinzani, bado kuna wasiwasi wa kura za wananchi wasiofungamana na upande wowote (swing voters).

Akizungumza katika mjadala wa matokeo ya utafiti wa Twaweza wa Tanzania kuelekea 2015 uliozinduliwa jana jijini Dar es Salaam, Nape alisema kuna haja ya kuwaangalia wapiga kura hao kwani ni dalili ya vyama kupoteza mvuto.

“Kuna ongezeko la watu wasio na imani na vyama. Hii inaonyesha idadi ya wanaotaka mgombea binafsi inaongezeka. Ni jambo la kuangalia, hata watu waliojitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 inaonyesha kuwa wapiga kura walikuwa wachache,” alisema Nape.

Akizungumzia takwimu zinazoonyesha Chama cha Mapinduzi kuwa juu ya vyama vya upinzani, Nape  alisema ni kutokana na mikutano ya hadhara waliyoifanya kati ya mwaka 2012 na 2013.

“CCM tumefanya ziara mikoani kwa siku 30 na mikutano kati ya 60 hadi 70. Katiba ilizungumziwa kidogo. Wananchi walikuwa wanazungumzia kilimo, afya, elimu na mengineyo,” alisema Nape na kuongeza:

“Takwimu zinaonyesha CCM inaungwa mkono, kazi imefanyika kati ya mwaka 2012 na 2013 tukiwa na mikakati ya kurudi kwenye reli. Hilo ni jambo zuri kuelekea 2015 na ni baya kwa watani wetu.”

Alisema licha ya vyama vya upinzani vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuungana, bado CCM imevipita.

“Itatokea nini wapinzani wakiungana? Mmeona takwimu jinsi walivyopitwa kati ya asilimia 47 hadi asilimia 28? Hata hizo kura zinazoelea asilimia 35 bado tunaweza kunyang’anyana,”alisema.

Akizungumzia mgombea urais watakayemsimamisha uchaguzi mkuu ujao, alisema hata kama wananchi wanamkubali mtu lakini kama mtu huyo hakubaliki ndani ya chama hawatamsimamisha.

Dk. Slaa auponda utafiti

Akizungumzia ripoti hiyo Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema hana imani na utafiti huo kwani ripoti inaonyesha imepikwa.

Alisema utafiti huo unaonyesha umefanyika Septemba mwaka huu kabla hata Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) haujatangaza kumsimamisha mgombea mmoja.

“Nimeshangazwa sana inaonyesha ni jinsi gani ripoti imepikwa…kwanza nina mashaka sana na mkuu wa utafiti huo ninamjua na Watanzania nao wahoji ni nani, anakubalika kiasi gani hapa nchini na ameshwawahi kufanya tafiti ngapi.

“Utafiti unaonyesha umefanyika Septemba kabla hata Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hatujatangaza kuungana Oktoba 26 mwaka huu, binafsi bado sijasoma ripoti hiyo lakini nashangazwa kwamba mganga wa utabiri huo ni nani, hata Ukawa wakimsimamisha mgombea mmoja wanakuwa wameachwa mbali na CCM yaani ‘hai-reflect’ kabisa.

Matatizo ya uchumi

Kwa upande wake Maria Sarungu kutoka shirika la Change Tanzania alisema utafiti huo umeonyesha kuporomoka kwa uchumi wa Tanzania hali inayoashiria kuporomoka kwa Serikali.

“Haya matatizo ya umasikini wa uchumi, afya, elimu yanaashiria kuporomoka kwa Serikali. Kwa mfano Marekani mwaka 2008 uchumi ulipotetereka ndipo Obama alipopata nafasi ya kushinda, hata Clinton alishinda hivyo hivyo. Wananchi wengi wamekosa imani na taasisi za siasa, ukiangalia takwimu ‘swing voters’ ni wengi,” alisema Sarungi.

Naye Jenerali Ulimwengu alikosoa utafiti huo huku akitaka wagombea waliotajwa kupimwa na kazi zao.

“Tukiangalia hawa wagombea urais, wametajwa kwa msingi upi? Kwa mfano Mizengo Pinda (Waziri Mkuu) amefanya nini kwenye kilimo? Samuel Sitta amefanya nini? Zitto amefanya nini? Kutaja watu tu ni sawa na mashindano ya urembo,” alisema Ulimwengu na kuongeza:

“Tunatumia muda mwingi kuchagua mbuzi wa kuchinja kesho kule Vingunguti kuliko viongozi wetu. Tunaangalia kwato, pembe wakati anakwenda kuchinjwa kesho yake. Kwa mfano Pinda amefanya nini katika ‘Piga tu?” alihoji Ulimwengu.

Naye Profesa Kitila Mkumbo kutoka Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu, alisema utafiti huo umeonyesha jinsi wananchi walivyopoteza imani na viongozi waliopo hivyo jitihada zifanyike kuwalazimisha watu wasiotaka uongozi lakini wanafaa.

“Idadi ya watu wasiokubali utendaji wa viongozi wetu ni kubwa mno ukilinganisha na utendaji wa Rais wa Marekani Barrack Obama ulio juu ya asilimia 30. Tutafute viongozi wasiotaka kuwa viongozi lakini wanafaa, tuwasukume kama kina Warioba (Jaji Joseph)”

Profesa Bana aumbuliwa suala la Katiba

Suala la Katiba nalo lilitawala mjadala huo ambapo mmoja wa wanajopo, Profesa Benson Bana kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema Katiba si muhimu katika kutatua matatizo ya Watanzania.

Akichangia katika mjadala huo ulioongozwa na Mkurugenzi wa Twaweza, Rakesh Rajani, Profesa Bana licha ya kuusifu utafiti huo, alisema kwa miaka zaidi ya 50 ya uhuru kumekuwa na kero zinazowasumbua Watanzania za ujinga, umasikini na maradhi, lakini Katiba si jawabu la mambo yote.

“Kuhusu Katiba, inaonyesha kuwa ndiyo jawabu la mambo yote, hiyo siyo sahihi. Katiba siyo mwarobaini wa kila tatizo la wananchi, ni muhimu lakini siyo lazima,” alisema Profesa Bana.

Kauli ya Profesa Bana iliungwa mkono na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliyesema: “Tukisema Katiba ndiyo kila kitu, tutaiweka kwenye kabati na hatutaitekeleza. Si vizuri kusema Katiba siyo muhimu na siyo vizuri kusema Katiba ndiyo kila kitu.”

Hata hivyo akichangia katika mjadala huo, mwanajopo mwenzake, Jenerali Ulimwengu alisema Katiba ni mambo yote yanayohusu wananchi.

“Katiba siyo lazima iandikwe na Warioba (Jaji Joseph) na Chenge (Andrew). Ni suala la kuheshimu sheria na taratibu zote tulizojiwekekea. Katiba ni kila kitu kinachowahusu wananchi, yawe ni maji, afya, elimu na uchumi,” alisema Ulimwengu na kuongeza:

“Tatizo huyu Profesa Bana haelewi nikisema Katiba, labda mpaka niseme ‘constitutionalism’.”

Naye Maria Sarungi kutoka shirika la Change Tanzania alisema mabadiliko ya kweli yanakuja kwa kubadilisha Katiba ambayo ndiyo mfumo unaotawala wananchi kuliko kufikiria mtu atakayekuja kuwakomboa wananchi.

“Tuna dhana ya ‘Messiah complex’, yaani Watanzania wanasubiri mtu mmoja atakayekuja kuwakomboa na kuleta mabadiliko. Ni vizuri lakini ni hatari.

“Mabadiliko yanakuja kwa kubadili mfumo ambao ndiyo Katiba, tatizo wanasiasa wetu huwa wanafurahia kinachowafurahisha lakini si yale ambayo hayawafurahishi,” alisema Sarungi.

Kwa upande mchangiaji wa mada ambaye ni mwandishi wa vitabu, Godfrey Swai alisema data za utafiti huo zinaonyesha utawala na Katiba ni mbovu ndio maana wengine wakasema hawako upande wowote.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Utafiti huo ni maandalizi ya “wisi na uchakachuaji wa kura” watanzania lazima tuwe macho na jambo hili. Nafurahi kwa sababu watanzania sas wanajua kuhoji mambo wazi wazi, nina imani tukiendelee hivi basi tutapata rais yule ambaye kweli anatakiwa na Watanzania lakini pia na Mungu, kwaajili ya kuwasaidia na kuwaongoza siyokuwatawala Wananchi wa Tanzania. Msomi yeyeote aliyefanya research na anayeijua research atagundua mara moja kasoro zilizopo katika utafiiti huu. Kifupi utafiti umepikwa kwa manufaa ya nani mwenye kuuandaa anajua.lakini muda ukifika mamboyatajulikana. Hii ni kutaka kupima upepo tu watu wanasema nini, na sasa wanajua watu hawakubaliani na upuuzi wanataka ukweli. Na ukweli utatuweka huru.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles