NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson, amepata ajali baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongana na gari jingine dogo.
Taarifa zilizopatikana mjini Mbeya zinasema kwamba, Dk. Akson alipata ajali hiyo jana saa kumi mchana alipokuwa akitoka mjini Mbeya kuelekea kijijini kwao Bulyaga, Wilaya ya Rungwe,Mkoa wa Mbeya.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kipoke wilayani humo na kwamba awali Dk. Tulia alitembelea Shule ya Sekondari Loreza alikopata elimu yake ya sekondari miaka mingi iliyopita.
Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Bunge, Owen Mwandumbya, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema hakuna aliyeumia katika ajali hiyo.
“Ajali hiyo ilitokea wakati Dk. Akson alipokuwa akitoka mjini Mbeya akielekea kijijini kwao. Kwa bahati nzuri, hakuna aliyeumia na hivi tunavyozungumza yeye na msafara wake wameshafika kijijini kwao wamepumzika,” alisema Mwandumbya kwa kifupi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi ili azungumzie ajali hiyo, hakupatikana.