Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera Ikulu Jijini Dar es salaam, ambapo pamoja na mambo mengine amepokea taarifa ya maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika Machi 2, mwaka huu jijini Arusha.
Rais Magufuli kwa sasa ndiye mwenyekiti wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Dk. Richard Sezibera, alisema maandalizi kuhusiana na mkutano huo yanakwenda vizuri.
Amesema pamoja na mambo mengine mkutano huo, utajadili masuala kadhaa ikiwamo mpango wa kuanzisha viwanda vya magari ndani ya jumuiya ili kupunguza uingizaji wa magari kutoka nje ya nchi na marais kuzindua pasi ya kusafiria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kuhusu hali ya Jumuiya, Dk. Sezibera, alisema inaendelea vizuri na ametaja baadhi ya mambo ambayo yamefanyika kuwa ni kutiwa saini kwa mkataba wa Umoja wa Forodha, makubaliano ya Soko la Pamoja na makubaliano ya Sarafu Moja.