30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Azam yabanwa Mbeya

stewat hall*Yashindwa kuishusha Yanga kileleni

NA PENDO FUNDISHA, MBEYA

TIMU ya soka ya Azam FC jana ilishindwa kurejea kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kubanwa mbavu na maafande wa Tanzania Prisons katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Azam ambao wamefikisha pointi 46 sawa na vinara Yanga wanaoongoza kwa tofauti ya wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, walihitaji matokeo ya ushindi wa aina yoyote ili waweze kushika usukani wa ligi hiyo.

Katika mchezo wao wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Chamazi, Azam waliifunga Prisons bao 2-1, hivyo kwa  matokeo ya mchezo wa jana ambao ulikuwa wa kiporo kwa Azam, Prisons walidhihirisha ubabe wao wanapocheza katika uwanja wa nyumbani kwani hawajawahi kukubali kufungwa wanapokutana na wapinzani wao.

Hata hivyo, wenyeji Prisons ambao wamebaki katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, waliwabana vilivyo wapinzani wao, huku wakionyesha wazi kuwa wamepania kuendeleza rekodi yao ya kutofungwa na Azam  kwenye uwanja wao.

Mchezo wa jana ulianza kwa kasi ambapo dakika ya 16 mshambuliaji wa Prisons, Mohamed Mkopi, alishindwa kuipatia timu yake bao la kuongoza akiwa katika nafasi nzuri baada ya kupiga shuti kali lililopaa juu ya lango na kutoka nje.

Prisons waliendeleza mashambulizi langoni kwa Azam kupitia kwa wachezaji wao, Jeremia Juma na Juma Seif, lakini walishindwa kuzitumia vyema nafasi walizopata kufunga mabao.

Pia washambuliaji John Bocco na Kipre Tchetche wa Azam ambayo ina rekodi ya kupata matokeo yasiyoridhisha katika Uwanja wa Sokoine, walishindwa kuzitumia vyema nafasi walizopata kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya 46, Mkopi akiwa ndani ya eneo la 18, alikosa bao la wazi baada ya kupiga shuti kali ambalo lilitolewa nje na mabeki wa Azam na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Azam walizinduka dakika ya 66 ambapo Ramadhani Singano ‘Messi’ alipiga shuti kali ambalo lilimkuta Shomari Kapombe akiwa katika nafasi nzuri na kupiga kichwa lakini liliokolewa na kipa wa Prisons, Beno Kakolanya.

Baada ya kuzidiwa mbinu, Azam walilazimika kufanya mabadiliko ya kumtoa Michael Bolou dakika ya 79 na nafasi yake kuchukuliwa na Farid Mussa, huku Prisons wakimtoa Nurdin Chona na kumuingiza Meshack Selemani, lakini mabadiliko hayo hayakuzaa matunda kwa pande zote.

Azam: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, David Mwantika, Ramadhan Singano ‘Messi’, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Jean Mugiraneza ‘Migi’, Michael Bolou/Farid Mussa, Kipre Tchetche na John Bocco.

Prisons: Beno Kakolanya, Laurian Mpalile, Salum Kimenya, James Mwasote, Nurdin Chona/Meshack Seleman, Jumanne Elfadhil, Lambart Sabiyanka, Juma Seif, Mohamed Mkopi, Benjamini Asukile na Jeremia Juma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles