28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Mzee Mwinyi umeondoka na darasa kuu la ‘Hekima za Mfalme Suleiman.’

Na Absalom Kibanda

LALA salama Rais wa mioyo ya watu wema, Alhaji Ali Hassan Mwinyi. Darasa lako gumu la uongozi limeacha ombwe.

Waliovaa kiatu chako cha uongozi (urais) Zanzibar tangu uondoke (1984-85) na Tanzania (1985-95) takriban wote kiliwapwaya.

Utu wema, kutokuwa na makuu, utajiri wa maarifa na hekima na kukataa kwako kulipa kisasi ni tunu ulizobeba ukiwa madarakani hata baada ya kuondoka.

Hata ulipopigwa na kushambuliwa kwa kejeli na matendo, ulitangaza msamaha kwa kauli thabiti na kwa vitendo.

Ulituvusha kutoka nyakati za majaribu makubwa ya kitaifa na kidunia. Japo haikuwa rahisi kuwarithi, Aboud Jumbe Mwinyi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lakini wewe uliweza.

Uliwaenzi waliokutangulia wakiwa hai kwa kuwastahi hata walipokuvunjia heshima na zaidi walipokukosoa na pengine kukunyanyasa.

Ukiwa katika kilele cha madaraka, ulijinasibu kwa ‘Hekima za Mfalme Suleiman’ kwamba kwa Mwalimu, wewe ulikuwa KICHUGUU naye alikuwa MLIMA KILIMANJARO.

Alipotokea ‘mwehu’ akakushambulia kwa makofi hadharani ukiwa umestaafu, ulimtangazia msamaha.

Wehu wengine waliopata kushambulia viongozi wa namna yako kwa maneno na matendo ama walipata mapigo hadharani au walipotezwa na kutokomea.

Mambo haya yamewashinda marais wetu. Wako waliotuumiza kwa sababu tu ya kuamini kwao kwamba tuliwaumiza tena kwa maandishi yetu tu.

Wako walioteka, waliotesa na kupoteza watu kwa sababu tu ya hasira na kiburi cha urais.

Nani hajui kwamba leo kisasi kinachotokana na kiburi cha madaraka kimekuwa ada Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Kikombe cha kiburi cha madaraka kimewajaa warithi wako. Wako walioumiza hadi wasaidizi wao wakuu kwa sababu tu ya ulevi wa mamlaka.

Kile ambacho Baba wa Taifa alipata kukisema kwamba, kwa katiba hii angeweza akawa dikteta, kilikuja kujidhihirisha wakati ukiwa umestaafu

Warithi wako walipoka haki ya uraia kwa watu waliowapinga au kuwakosoa, walishitaki mahakamani wale waliowanyoshea vidole na wengine wakafanya mabaya zaidi ya hayo kwa yeyote aliyekwenda kinyume tu cha maneno yao.

Jenerali Twaha Ulimwengu, Balozi Timothy Bandora wanaweza wakaandika hili vyema zaidi kuhusu utu wema wako na ustahimilivu wako kuliko miye.

Mzee wetu Mwinyi, watu wa aina ya Dk. Stephen Ulimboka, Saed Kubenea, Ndimara Tegambwage, Theophil Makunga, Samson Mwigamba na Absalom Kibanda wanacho pia cha kusema kuhusu hasira za Rais aliye Ikulu zinavyoweza kuwa maelekezo ama mtaani au mahakamani.

Absalom Kibanda.

Si hao tu, simulizi ya jeuri ya urais, na thamani ya utu wako wema inaweza ikasemwa kwa ufasaha na Tundu Antipasi Lissu au Ben Saanane, Freeman Aikaeli Mbowe, Zitto Zubeir Kabwe, Ismail Ladhu Jussa na Ansbert Ngurumo ambao kila mmoja kwa namna yake amepata kukutana na nguvu ya mamlaka ya rais aliye madarakani, wadhifa uliouvaa na ukakataa katakata kukuvaa.

Nina hakika, Mwalimu Julius Nyerere, Aboud Jumbe Mwinyi, Benjamin William Mkapa, Maalim Seif Sharif Hamad, Edward Ngoyai Lowassa waliofanya kazi nawe na ambao leo wametangulia mbele ya haki pia, wanaweza kushuhudia wema wako huko mliko.

Sikumbuki kukusoma au kukusikia ukitamba au ukijisifia kwa lolote kubwa au dogo ulilofanya ukiwa madarakani au baada ya kustaafu kwa nchi yako.

Somo la unyenyekevu ni mtihani mgumu kwa warithi wako. Sina jina la rafiki yako yeyote au msaidizi wako hata mmoja uliyemsaliti au kumtesa au kumuumiza.

Mzee Kitwana Kondo angekuwa hai leo angetoa ushuhuda huu. Nilikuwapo Arusha ulipokuja kumpa joto Edward Lowassa wakati kijana wake Robert alipokuwa akifunga ndoa nyakati ngumu za Magufuli.

Iwapo Mzee wetu marehemu Jackson Makwetta aliyekutesa, kukudhihaki na hata kukudhulumu wakati nyote mkiwa mawaziri angekuwa hai leo angeshuhudia namna alivyopata tabu sana kukuelewa namna ulivyomstahi na hata ukamteua kuendelea kuwa waziri wako ulipokuja kuwa rais.

Miaka mingi baada ya wewe kuondoka wako warithi wa kiti chako cha urais walioadhibu ndugu, jamaa na marafiki zao eti kwa makosa waliyofanyiana shuleni, makazini au mitaani miaka kadhaa kabla wao hawajawa madarakani.

Natamani kuwapo na kumsoma mwalimu wangu, Salvatory Rweyemamu atakapoamua kuandika kitabu cha maisha yake ya kazi ndani ya vyumba vya habari na baadaye akiwa msaidizi wa rais, mbali ya yeye mwenyewe kuungama kwa kuchangia kikombe cha mateso kwa wengine kwa kujua au kutojua, aje pia kutoa ushuhuda wa namna alivyoonja machungu ya makali ya rais aliye madarakani wakati akiwa mwandishi wa habari na baada tu ya Rais Kikwete kutoka madarakani.

Kidogo ninachokijua, Salva, mwamba halisi wa maandishi ya kufikirisha, atakuwa na rejea nzuri ya maisha yake yaliyoguswa na marais watatu, Mkapa, Kikwete na John Pombe Magufuli ambao wote kila mmoja kwa kiwango na wakati wake, kiatu cha utu wema, ustahimilivu na kusamehe saba mara sabini, ulichovaa wewe Mzee Rukhsa kiliwapwaya walipokuwa madarakani.

Hayati Rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na mkewe, mama Sitti Mwinyi, wakiwa ndani ya basi la mwendo kasi wakati walipofanya ziara ya kutembelea mradi huo enzi za uhai wake, Picha na Maktaba.

Unyenyekevu ni ada. Bado nakumbuka namna ulivyolishtua taifa ulipokwenda Ikulu na kutoa kauli nzito ya kujishusha wakati Magufuli alipokuwa madarakani siku ulipomsifia kwa kufanya makubwa ambayo ninyi watangulizi wake watatu, wewe, Mkapa na Kikwete mlishindwa kuyafanya kwa miaka 30 mkiwa madarakani.

Rekodi bado ziko hai zinazoweza kuthibitisha kwamba si watangulizi au warithi wako waliopata kuwa na uwezo wa kulifanya hilo kabla ya kuingia Ikulu, wakiwa madarakani na hata walipostaafu.

Ulijali utu na maisha ya watu ukiwa waziri wa mambo ya ndani ukajiuzulu kwa sababu tu vifo vya mahabusu waliokufa Shinyanga. Uliwajibika kwa makosa ya wengine na kwa unyenyekevu.

Ukiwa Rais wa Zanzibar, aliyekuwa Waziri Kiongozi wako, Maalim Seif Sharif Hamad ameshuhudia katika kitabu chake namna ulivyomfanya msaidizi wako mwema na kwa jinsi mlivyoitendea haki kimageuzi na kimaendeleo.

Ukipoondoka tu madarakani mwaka 1985, mrithi wako akamgeuka, wakamshitaki na kumzushia na miaka mitatu tu baadaye wakamfukuza katika chama chenu.

Kwa kauli thabiti, Maalim Seif wakati akiwa hai kwa nyakati tofauti amepata kuwataja kwa majina namna warithi wako, Abdul Wakil Nombe, Salmin Amour Juma, Mkapa na Kikwete walivyodhulumu haki yake na ile ya Wazanzibari wakati kila mmoja wao akiwa madarakani. Kwake ulibakia kuwa mwanasiasa mwema na rais wa moyo wake.

Pumzika kwa amani Rais Ali Hassan Mwinyi. Darasa lako gumu litabakia rejea ya kitaifa na kimataifa. Tuna deni kubwa la UONGOZI kwako.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles