29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mwelekeo mpya

Mwenyekiti wa Kamati ya uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge
Mwenyekiti wa Kamati ya uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge

MAREGESI PAUL NA RACHEL MRISHO, DODOMA

KAMATI ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imewasilisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ikionyesha jinsi ilivyoifumua rasimu iliyowasilishwa bungeni hapa mwanzoni mwa mwaka huu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Rasimu hiyo iliwasilishwa bungeni jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Andrew Chenge ambapo imeongeza mambo ya muungano kutoka saba yaliyopendekezwa na rasimu ya Warioba hadi 14.

Kwa mujibu wa Chenge, rasimu hiyo ina sura 17, ibara 274 na katika ibara hizo, 233 zimetokana na rasimu ya Jaji Warioba.

Alisema pia kwamba ibara 47 za rasimu ya Jaji Warioba hazikufanyiwa marekebisho, ibara 186 zimefanyiwa marekebisho ya uandishi na kimaudhui, ibara 28 zimefutwa kabisa na pia zimeongezwa ibara mpya 41.

Pia alisema wakati wa kuandika rasimu hiyo, wajumbe walichukua mambo machache ya msingi na mengine yaliachwa ili yaandaliwe mazingira ya kuyatungia sheria kwa kuwa Katiba haiwezi kubeba kila kitu.

SURA YA KWANZA

Katika sura hii inayozungumzia muundo wa Serikali, Bunge Maalumu la Katiba katika rasimu yake, limependekeza muundo wa Serikali mbili tofauti na muundo wa Serikali tatu zilizokuwa zimependekezwa na Tume ya Jaji Warioba.

Kwa maana hiyo, mapendekezo ya uwapo wa Serikali ya Shirikisho lenye mamlaka kamili yaliyotokana na mapendekezo ya muundo wa Serikali tatu yametupwa rasmi.

Akizungumzia kutupwa kwa Serikali tatu, Chenge alisema kumetokana na kuhofia uwapo wa mgawanyiko katika jamii pindi nchi itakapokuwa na muundo wa Serikali tatu.

Kwa upande wa tunu za taifa ambazo ziko katika sura hii, rasimu mpya imezitaja kuwa ni lugha ya Kiswahili, muungano, utu na udugu pamoja na amani na utulivu tofauti na ilivyo katika Rasimu ya Warioba ambapo tunu hizo zimetajwa kuwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa.

SURA YA PILI

Sura hii inayozungumzia malengo muhimu, misingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali na sera za taifa, Bunge Maalumu la Katiba limeongeza majukumu kwa Bunge kutakiwa kutunga sheria itakayofafanua juu ya utekelezaji wa malengo muhimu kwa mujibu wa Katiba.

Katika sura hii, baadhi ya mambo yaliyoongezwa yalitokana na mchango uliotolewa na kada wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru aliyetaka Katiba ieleze wazi juu ya masuala ya kiuchumi kwa kuhimiza mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi, mapinduzi ya viwanda na kujenga sekta muhimu za nishati, mawasiliano na miundombinu.

SURA YA TANO

Sura hii inayozungumzia haki za binadamu, wajibu wa raia, jamii na mamlaka za nchi, katika rasimu mpya, vijana wanaruhusiwa kuanzisha baraza lao la taifa wakati katika rasimu ya Jaji Warioba baraza hilo halikuwapo.

SURA YA SABA

Katika rasimu mpya, sura hii inayozungumzia muundo wa Jamhuri ya Muungano, Bunge Maalumu linapendekeza Tanzania kuundwa na Serikali mbili ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati Rasimu ya Jaji Warioba ilipendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu.

Rasimu hiyo inazitaja serikali hizo kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Tanganyika.

SURA YA TISA

Sura hii katika rasimu mpya inahusu uhusiano na uratibu wa mambo ya muungano, lakini katika rasimu ya Warioba inahusu uhusiano na uratibu wa Serikali.

Katika rasimu mpya sura hii katika ibara ya 122 inasema kutakuwa na Tume ya Usimamizi na Uratibu wa Mambo ya Muungano itakayoitwa Tume ya Mambo ya Muungano, lakini Tume ya Jaji Warioba ilipendekeza tume hiyo iitwe Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali.

Katika rasimu mpya imependekezwa tume hiyo iwe na wajumbe ambao ni Makamu wa Kwanza wa Rais atakayekuwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu, kiongozi wa shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi na mawaziri wenye dhamana ya Muungano.

Lakini katika rasimu ya Jaji Warioba wajumbe waliopendekezwa ni makamu wa rais atakayekuwa mwenyekiti, rais wa Tanganyika, rais wa Zanzibar, mawaziri wa kazi, mawaziri wenye dhamana ya mambo ya nje wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

SURA YA KUMI

Sura hii inahusu muundo wa Bunge la Muungano na katika rasimu mpya inasema kutakuwa na wabunge watano watakaoteuliwa na rais ambapo inafanana na ilivyopendekezwa na Tume ya Katiba.

Kitendo cha kuwapo kwa mapendekezo hayo kunatofautiana na mapendekezo ya vyama vya walemavu ambao walitaka wawe asilimia tano ya wabunge wote.

Katika rasimu mpya, Bunge Maalumu la Katiba limependekeza idadi ya wabunge isizidi 360 wakati Rasimu ya Warioba ilipendekeza wabunge 75 katika Bunge la Muungano.

Hata hivyo, rasimu hii mpya haikueleza wazi jinsi wabunge wa viti maalum watakavyopatikana ingawa wakati wa mijadala ya Bunge, wajumbe wanawake walikuwa wakitaka wagombee sambamba na wabunge wanaume.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles