28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa Chadema Dar mbaroni

Dk. Wilbrod Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa

Na Waandishi wetu

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam jana, liliwakamata  viongozi na wafuasi 11 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dar es Salaam.

Wafuasi hao walikamatwa jana asubuhi walipojaribu kufanya maandamano ya kuelekea ofisi  ya  Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki kwa nia ya kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma.

Wafuasi hao ambao walifika saa 12 asubuhi wakitokea maeneo mbalimbali ya mkoa huo, bila ya kuvalia sare za chama hicho na kuanza kurandaranda karibu na ofisi za mkuu wa mkoa.

Baadhi ya wanaandamanaji walionekana kukusanyika karibu na jengo la Mwalimu House, Ilala,wengine walikuwa karibu na hoteli ya Lamada, huku wakikusanyika jirani na soko la Karume kwa ajili ya kusubiriana ili waweze kufika katika ofisi hizo.

Wakiwa katika maeneo hayo, polisi walifika mapema lakini waandamanaji hawakuweza kuwabaini kutokana na polisi hao kuvaa kiraia.

Chanzo cha habari kutoka kwa baadhi ya waandamanaji hao kilisema kuwa polisi walionekana kutumia mbinu mpya ya kuwakamata wafuasi hao kwa kumshika mmoja baada ya mwingine hali iliyosababisha waandamanaji hao kubaki wachache.

Chanzo hicho kilidai kuwa wakati tukio la kukamatwa kwa baadhi ya waandamanaji hao likiendelea, polisi wengine waliokuwa wamevaa sare walitanda katika ofisi hiyo ya mkuu wa mkoa na maeneo ya jirani kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.

Baada ya waandamanaji hao kubaini mbinu hizo, walianza kuondoka mmoja mmoja kwa kuhofia kukamatwa, huku polisi wakipata nafasi ya kuimarisha ulinzi zaidi. Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa hakuwapo ofisini.

Akithibitisha tukio hilo, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema  taarifa za wafuasi wa chama hicho kuelekea kwa mkuu wa mkoa alipewa na viongozi wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema waliokamatwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kinondoni, Waziri Mhunzi na Sifa Majura, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Ilala.

Wengine waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) Wilaya ya  Temeke, Sina Manzi na Penina Rajabu ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji Ubungo na Katibu wa Baraza la Vijana (BAVICHA) Kata ya Mwananyamala  aliyejulikana kwa jina moja la Urio.

Wengine ni Mweka Hazina Baraza la Wazee Wilaya ya Kinondoni, Mchungaji Zephania na mkewe, Magret Zephania ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA), Kijitonyama.

Wengine na vyeo vyao katika mabano ni Vailet Seko (Mhazini Mwananyamala), Ally Dadia (Mwenezi Kata ya Hananasif), Anjela Njiro (Mwenezi BAWACHA Wilaya ya Kinondoni), John Kobelo (Mwenezi wa Kata ya Mbezi juu).

Miongoni mwa wafuasi walioandamana ni pamoja na Mwita Waitara ambaye alisema maandamano hayo ni utekelezaji wa azimio la kamati kuu ya chama hicho ya kuwataka kuandamana na kufanya migomo ya mara kwa mara.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanachama hao wataendelea kufanya maandamano hayo na migomo hiyo ni njia mojawapo ya kuitaka serikali kusitisha shughuli zao.

“Mkutano mkuu uliazimia kufanya maandamano na migomo isiyo na kikomo, lengo ni kuitaka serikali kusimamisha shughuli za Bunge Maalum la Katiba, tutaendelea kufanya maandamano na migomo isiyo na kikomo,”alisema Waitara.

Naye Mwalimu wa Chadema ni Msingi Taifa,General Kaduma alisema maandamano hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu wameweza kusitisha shughuli za serikali ikiwamo ya ofisi ya mkuu wa mkoa.

“Shughuli za kijamii katika ofisi ya mkuu wa mkoa zilisimama kwa muda ili kutusubiri sisi, mkakati wetu ni kuhakikisha kuwa tunaendelea kusimamisha shughuli za serikali katika ofisi mbalimbali nchini,”alisema Kaduma.

MAKAMANDA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alielezea tukio hilo la maandamano iwapo liliathiri ulinzi katika mkoa wake wa kipolisi, alisema hali ilikuwa shwari na hakuna na maandamano yoyote yaliyofanyika.

“Katika mkoa wangu hakuna kundi la watu ambalo limefanya maandamano na tangu mapema tumeimarisha ulinzi katika maeneo yote ya ya Kinondoni,” alisema Wambura.

Aliongeza kuwa kutokana na kutofanyika maandamano hayo katika Mkoa wa Kinondoni hivyo hakukuwa na mfuasi wala kiongozi wa chama hicho aliyekamatwa.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya alisema hakuna mtu yeyote aliyethubutu kujitokeza kuandamana katika mkoa wake.

“Tuko ngangari na tumeimarisha ulinzi kila mahali kama kawaida yetu na ninashukuru huku hakuna Chadema aliyejitokeza kushiriki katika maandamano hayo,” alisema Kamanda Kihenya.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alithibitisha kuimarisha ulinzi maeneo yote hasa katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ambako waandamanaji walikuwa wamepanga kufikisha ujumbe wao wa kutaka kusitisha Bunge la katiba linaloendelea mjini Dodoma.

“Ulinzi umeimarishwa kila eneo, nadhani mtakuwa mmeona wenyewe, ila hadi sasa sijapokea idadi ya waliokamatwa katika operesheni hiyo na  bado tunaendelea kufanya doria katika mkoa huu wa kipolisi,” alisema Kamanda Nzuki.

KAGERA

Habari kutoka mkoani Kagera, zinasema wafuasi wa Chadema jana waliwapiga chenga polisi na kufanya maandamano katika kata za Bukoba na Kibeta, wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Habari Hii imeandaliwa na Shabani Matutu, Patricia Kimelemeta na Grace Shitundu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles