28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanamume azaa pacha wake aliyembeba tumboni miaka 36

kijusi-kilichoondolewa

INGAWA kinaweza kuwa si kitu kipya, simulizi katika makala haya inashtua, ngumu kuamini iwapo kweli ipo, ingawa huo ndio ukweli.

Si kitu kipya kwa mwanamume kuwa mjamzito na kuzaa mtoto. Ni hivi karibuni katika safu hii ilikuwa na mwanamume Mmarekani aliyezaa watoto watatu, akihesabiwa kuwa pekee duniani kuwahi kufanya hivyo.

Hata hivyo, mwanamume huyo awali alikuwa mwanamke kabla ya kuamua kubadili jinsi, lakini akiwa ameacha viungo vyake vya uzazi vya kike ikiwa ni mahsusi kwa kuzaa siku za usoni. Ndivyo ilivyotokea!

Achana na simulizi hiyo ya Mmarekani, ambaye kwao wanawake kubadili jinsi kuwa wanaume na wanaume kuwa wanawake ni kitu cha kawaida simulizi hii kutoka India inashtusha.

Ni kuhusu mwanamume aliyeishi na ujauzito kwa miaka 36, tena wa pacha wake mwenyewe aliyepaswa kuzaliwa naye kutoka tumboni mwa mama yake miaka 36 iliyopita.

Awali hakukuwa na mtu aliyehisi tatizo hilo, kila mtu akiwamo yeye mwenyewe alidhani tu kwamba ana tumbo kubwa kwa sababu hakuonesha hali yoyote ya maumivu au kujisikia vibaya.

Kisa hiki kilichoiteka vyombo vya habari mwaka 1999 kinamhusu Sanju Bhagat, mkulima aliyekuwa na umri wa miaka 36 kipindi hicho.

Akiishi katika Jiji la Nagpur, Bhagat alisema kwamba alijisikia fadhaa kipindi chote cha maisha yake kuhusu tumbo lake hilo.

Tumbo la Bhagat awali lilivimba kiasi cha kuonekana yu mjamzito wa miezi tisa na alikuwa akipumua kwa taabu.

Usiku mmoja wa Juni 1999, tatizo lake lilizidi kuwa kubwa kuliko alivyofikiria.

Gari la wagonjwa lilimkimbiza Bhagat katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Tata mjini Mumbai kwa upasuaji wa dharura.

Kwa kutazama tu, akili za madaktari ziliwaambia huo ni uvimbe unaokua ndani ya tumbo.

Lakini wakati upasuaji ulipoanza walikutana na kitu ambacho hawakuwahi kukiona wala kukiota kabla.

“Kimsingi uvimbe ulikuwa mkubwa na ndio maana hakuweza kupumua vyema,” anasema Dk. Ajay Mehta wa hospitali hiyo.

“Kwa sababu ya ukubwa wa uvimbe, ilitupatia shida mno kuendesha operesheni. Tulikutana na matatizo mengi.”

Mehta anasema kwa kawaida huweza kubaini uvimbe mara upasuaji unapoanza. Lakini wakati wa kumshughulikia Bhagat, Mehta aliona kitu ambacho hakuwahi kukutana nacho wala kukiota.

Kwa kadiri alivyokuwa akikata kwa ndani zaidi katika tumbo la Bhagat, maji maji mengi yalichuruzika na kitu cha ajabu kikatokeza.

“Kwa mshangao wangu na wasiwasi, nilijikuta nikishikana mkono na mtu ndani ya tumbo. Ilitushtusha na kutushangaza sana. Mbali ya kujikuta akishikana mkono na mtu, alihisi mifupa mingi,” anasema.

Wakati wa kutoa uvimbe huo, kwanza uliibuka mguu mmoja, ukafuatia mwingine. Kisha sehemu za siri, nywele na miguu tena, taya na mikono.

Ilionekana kana kwamba Sanju amezaa. Madaktari walibaini kuwa Sanju Bhagat ana moja ya hali za kitabibu za nadra na kushangaza zaidi duniani – kijusi ndani ya kijusi.

Kwa mujibu wa Mehta, kuna kesi zisizozidi 90 duniani za kijusi ndani ya kijusi zilizorekodiwa katika historia ya tiba duniani.

Kiuhalisia Bhagat alikuwa amebeba mwili uliobadilika wa pacha wake kwa miaka 36, ambaye aliweza kutoa miguu, nywele na kucha ndefu.

Ni hali ya nadra mno, ambayo hutokea wakati kijusi kinaponasa ndani ya pacha wake.

Kijusi kilichonasa kinaweza kuishi kama kimelea hata baada ya uzazi kwa kutengeneza umbo kama la mwavuli, ambao humsambazia damu pacha wake hadi kinakua kikubwa kiasi cha kuanza kumsumbua mwenyeji yaani mbeba mimba hiyo.

Ni wakati ambao, madaktari hulazimika kuingilia kati.

Mara nyingi mapacha wote hawa hufa kwa sababu ya matatizo ya kuchangia ‘mji wa mimba.’

Lakini katika suala la Bhagat, aliweza kufanya viishi na kuzaliwa, na cha kushangaza hakuna aliyefahamu alisaidia maisha ya kijusi kwa miaka 36.

Hiyo inamaanisha pia pacha hao waliibuka muda mchache tu baada ya Bhagat kuzaliwa. Lakini pia hakukuwa na mji wa mimba katika mwili wa Bhagat.

Mara baada ya upasuaji, maumivu aliyokuwa nayo Bhagat na matatizo ya kupumua yalitoweka na alipona mara moja.

Uzito wake ulipungua kutoka lbs 200 sawa na kilo 91 hadi lbs 88 sawa na kilo 40.

Kesi hii inaweza kuwa miujiza kwa madaktari, lakini kwa Bhagat hali yake ilikuwa chanzo cha fedheha na fadhaa.

Katika maisha yake yote watu wa kijijini kwake walikuwa wakimcheka na kumwambia anaonekana kuwa yu mjamzito huku wengine wakienda mbali kuhoji nani baba wa mtoto huyo na lini alitungwa kitandani.

Ijapokuwa sehemu kubwa ya dhihaka ziliegemea katika utani, kiuhalisia katika suala la mimba walikuwa sahihi.

Leo hii Bhagat yu mzima wa buheri ya afya, akiishi maisha ya kawaida kijijini kwake, lakini pia akiendelea bado kutaniwa mara kwa mara.

Watu bado wanamcheka na kuwa alijifungua kwa njia ya upasuaji.

Hata hivyo, Bhagat alisema anashukuru kwa upasuaji huo na hakupenda kufahamu kile Mehta alichofanya au kukiona, zaidi ya kufurahia kuondolewa kiumbe kutoka tumboni mwake.

“Wala hakutaka kuona kile tulichokitoa tumboni mwake kwa sababu kilionekana kutisha mno,” Mehta anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles