31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

MWAKA MMOJA MADARAKANI HUPIMWA KWA MWELEKEO-(1)

johnmagufuli

Yamesalia majuma matatu kutimia kigezo cha kipimo cha wachambuzi wengi wa siasa kuhusu mafanikio ya serikali ya awamu ya tano itakayotimiza mwaka mmoja Novemba 5 mwaka huu.

 Kuna namna tofauti za kupima tangu wakati wa kampeni ambapo sera zinazomuuza anayejinadi kusaka uongozi humkubalisha kwa wapiga kura katika muda uliotengwa. Kipimo cha pili kinachotumika mara nyingi ni siku 100 za kwanza madarakani na cha tatu ni mwaka mmoja ingawa kwa tafakuri yangu, si lazima iwe hivyo bali ni kutokana na mazoea ya ufuasi wa wengi kwa kuwa kama mgombea alitangaza sera za chama kilichomsimika ugombea hatimaye akafanikiwa kuingia madarakani, basi ahadi za sera ndani ya ilani ndizo zinazopaswa kupimwa utekelezaji wake hususan katika mwelekeo wa kutimiza kilichobainishwa. Ni mwelekeo kwa kuwa kuna mikakati mbadala na aliyoikuta katika kuimarisha au kubadilisha mbinu ili kufikia malengo, lakini pia kuna ambayo hayakukamilishwa na awamu iliyopita yanayorithiwa ili kufanikisha ukamilishwaji.

 Nitohoe kutoka ilani iliyomnadi Mheshimiwa Rais JPM katika kampeni iliyomfanikisha kuingia madarakani, eneo linalonivutia zaidi ni kuhusu viwanda na biashara maana amesikika mara nyingi akieleza dhamira ya serikali yake kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda hivyo kuongeza kasi ya maendeleo. Aya ya 32 ya ilani hiyo inabainisha msukumo wa miaka mitano iliyopita wa uimarishaji wa uzalishaji wa viwanda na mauzo ya bidhaa nchi za nje kwa ushirikiano na sekta binafsi kupitia mashirika ya umma yanayohusika.

Kwamba mafanikio yaliyopatikana ni ukuaji wa asilimia 0.2 kutoka 7.7 hadi 7.9 kutokana na mchango wa pato la viwanda kwa uchumi kuongezeka kwa asilimia 0.3 kutoka 9.6% hadi 9.9% kwa miradi ya viwanda ipatayo 454. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyoanishwa kwenye ilani hiyo (2010-2013) mauzo kwenye EAC yamepanda kutoka dola milioni 419 hadi 450, kwenye SADC kutoka dola milioni 625 hadi 1, 209 na kwenye AGOA kutoka dola milioni 50 hadi 76.

Muono mbele kutoka kwenye takwimu hizo za ilani ya CCM kwenye uchaguzi uliokipa ushindi unaakisi mafanikio lakini haulezi changamoto za kutofikia kiwango cha juu zaidi ya hapo.

 Inabainishwa kwamba serikali itajielekeza zaidi katika utekelezaji wa sera ya maendeleo endelevu ya viwanda katika awamu ya tatu (2010-2020) kwa sekta ya viwanda kuongeza mchango wake, kama ilivyobainishwa katika dira ya maendeleo ya taifa kufikia mwaka 2025 kwa kujikita katika utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano (2015/16 hadi 2020/21).

Kwamba katika kipindi hicho ujenzi wa viwanda mama utaanzishwa pamoja na kuimarisha vilivyopo, ili kuimarisha mchango wa sekta hiyo adhimu ndani ya miaka saba (2013-2020) kufikia  asilimia 15 kutoka 9.9% inayobainishwa na takwimu zilizopita likitafutwa ongezeko la asilimia 5.1, ili sekta hiyo iongeze ajira kwa asilimia 40 kwa vipaumbele vya matumizi ya ghafi za ndani kutokana na kilimo, uvuvi, mazao na maliasili kwa bidhaa zitakazozalishwa kwa kuweka mazingira yanayowezesha utekelezaji kwa kuhamasisha sekta binafsi kujikita zaidi katika uwekezaji huo na kuvilinda viwanda vya ndani dhidi ya bidhaa za nje.

 Lengo ni kuongeza  tija  na kupanua wigo wa masoko kwa kutumia fursa zilizopo COMESA, SADC, EAC, EU na mataifa makubwa ya Magharibi. Katika sehemu hii ya kwanza ya mfululizo wa tafakuri yangu nimejikita katika ilani ya serikali ya awamu ya tano kwa kuwa kama inafanikiwa kutimiza malengo kwa mujibu wa vipaumbele vya sera yake, tutaweza kupima mwelekeo walau kwa mwaka mmoja kwa kuangazia iliyobainisha kuyatekeleza kama kweli mashiko yake yanajisadifu maana hapo ndipo mzani wetu unaweza kutupa jibu la mwelekeo wa safari yetu.

Matumaini ya wengi walipoichagua CCM ni kuimarika maisha yao na malengo ya sekta mtambuka ya viwanda ndani ya ilani, yanabeba sekta nyingine ambazo zitaleta nafuu kwa wananchi wanaozitumikia kwani viwanda havitafanikiwa bila uimara wa kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na mazingira rafiki yasiyo na urasimu wa ushirikishwaji sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi unaotuimarisha kimaisha, kutokana na uzalishaji utakaoongeza kodi na kuifanya serikali ijiendeshe bila ukata hivyo kutuhudumia vyema.

 Hiyo ni sehemu ndogo tu ya ilani ya CCM yenye kurasa 228 zenye aya 189 zinazojumuisha vifungu vingi kwa kila aya, ambapo kimsingi ni kwamba ahadi zilizobainishwa ni nyingi mno hususan ukichanganya na zilizopita ambazo hazikukamilika, huku baadhi zikipigiwa upatu wa kuanza kutekelezwa (kuhamia Dodoma) ingawa kwenye ilani zina maelezo mafupi yasiyojitosheleza. Lakini swali la kimsingi ni je, ndani ya mwaka mmoja mwelekeo ulionadiwa ndiyo unaofuatwa?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles