32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, February 2, 2023

Contact us: [email protected]

Nkurunziza anakiogopa kibano cha Bensouda

bensouda

Na Dennis Luambano, Dar es Salaam

FUKUTO bado linaendelea kufukuta nchini Burundi. Kila siku mwenendo wa kufukuta kwake unabadilika.

Leo likiibuka jambo moja, kesho linaibuka jingine hasa baada ya mgogoro wa madaraka kuchipuka nchini humo.

Wakati fukuto hilo likiendelea, ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ilisema Warundi milioni 4.6 wanakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na mgogoro huo.

Huku wengine zaidi ya 590,000 walikuwa wanahitaji msaada wa haraka wa chakula la sivyo wangekufa kwa njaa.

Yote hayo kasababisha Rais Pierre Nkurunziza anayeongoza kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika Juni, mwaka jana.

Licha ya kupingwa na jumuiya za kimataifa, wanaharakati na wapinzani wake wa ndani lakini akagombea urais kwa hoja kwamba utawala wa awamu yake ya kwanza ulikuwa wa mpito! Eti alisema kwamba katika muhula wake wa kwanza aliitawala Burundi kupitia Katiba ya zamani kwa hiyo kupitia Katiba mpya bado ana muhula wake wa pili ambao ni wa mwisho.

Baada ya kushinda na kutawala tena ndipo machafuko yakaibuka huku maelfu ya Warundi wakipoteza maisha yao na wengine 265,000 wakikimbia nchini mwao na kuwa wakimbizi katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Tanzania, Uganda na Zambia.

Kwanini Nkurunziza aligombea tena. Kwanza ni kutokana na umri wake kuwa mdogo kwa maana anaona bado ana nguvu za kutawala na akiacha kazi ya urais hana kazi nyingine anayoweza kuifanya huku baadhi ya watu ndani ya chama chao cha CNDD-FDD na katika Serikali yake walimshawishi ang’ang’anie madaraka kwa kuwa wananufaika na utawala wake.

Wakati hali ya mambo ikiendelea hivyo, visa vya baadhi ya Warundi kuuawa navyo viliendelea na kusababisha Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Fatou Bensouda, kuibuka Aprili, mwaka huu na kusema atachunguza ghasia za Burundi.

Miezi sita baadaye kwa maana katikati ya wiki hii Bunge la nchi hiyo limeridhia kwa kauli moja kupiga kura ya kujiondoa katika mkataba wa Roma unaoitambua ICC.

Kura hiyo imefanyika siku chache tangu Umoja wa Mataifa (UN) uanzishe uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanyika Burundi.

Muswada huo wa sheria ya kujitoa ICC ulipitishwa kwa kura 94, huku kura mbili zikikataa na wengine 14 hawakupiga kura.

Baada ya hapo, matokeo ya kura hizo yatapelekwa katika Baraza la Seneti la Burundi linaongozwa na wabunge wa CNDD-FDD ambao nao watapiga kura kabla ya kuidhinishwa na Nkurunziza.

Hatua ya Nkurunziza na Serikali yake kufanya hivyo haijaja bahati mbaya bali ni baada ya Bensouda kuonyesha kuanza uchunguzi wa visa vya mauaji vinavyoendelea nchini humo na kama ungekamilika, ICC ingeanzisha mashitaka kuhusu tuhuma za mauaji, mateso, mauaji ya kupangwa, ubakaji na watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Kwa hiyo kitendo cha Burundi kupiga kura ya kujitoa ICC inaonyesha ni jinsi gani Nkurunziza alivyo muoga kushitakiwa, anaogopa kibano cha Bensouda na kitendo cha kushinikiza nchi hiyo ijitoe ni mwendelezo wa kiu ya viongozi wengi barani Afrika ya kutaka kujitoa.

Kwa mfano, mwaka jana ANC iliitaka Afrika Kusini ijiondoe ICC.

Uamuzi wa ANC ulitolewa kwa hoja kwamba ICC imepoteza mwelekeo na hawana imani na namna inavyoendeshwa.

Kwamba inalaumiwa na mataifa ya Afrika kwa kuwaandama zaidi viongozi wa Kiafrika kuliko mataifa mengine duniani.

Sasa swali la kujiuliza hapa, nani kati ya ICC na baadhi ya marais wa nchi za Afrika anayetetea haki batili na haki halali?

Kwa maana ICC inataka haki itendeke kutokana na baadhi ya marais barani Afrika na watu wengine kutekeleza uhalifu wa kivita katika nchi zao kwa kuua na kutesa raia. Lakini baadhi ya marais Afrika wanasema utendaji wake unabagua kwa kuwachukulia sheria baadhi ya wakosaji huku wengine wakiachwa. Nihitimishe kwa kusema kuwa nakubaliana na hoja za viongozi hao kutokana na utendaji wa ICC kutia shaka lakini pia sikubaliani nao wanapokataa wahalifu wa kivita wasishtakiwe ilhali kuna matukio chungu nzima yanatokea kila siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles