24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mvutano umeya Kinondoni wapamba moto

aron-kagurumjuliNa WAANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikitarajia kwenda mahakamani kupinga uchaguzi wa Meya wa Kinondoni, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli, ametetea uchaguzi na kusema umefanyika kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, Kagurumjuli alisema uchaguzi huo ulikuwa halali na ulizingatia kanuni na taratibu zote.

Alisema licha ya hali hiyo waliwasiliana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ili kupata mgawanyo wa madiwani ambao walimpa mwongozo kwa mujibu wa sheria kusimamia mgawanyo huo ikiwemo mgawanyo wa madiwani wa viti maalumu.

“NEC walinielekeza cha kufanya ikiwemo kugawanya madiwani wa viti maalumu kuwa theluthi moja ya madiwani wa kuchaguliwa na kwa Kinondoni Chadema wana madiwani 7 wa kuchaguliwa ambayo theluthi moja ni madiwani watatu wa viti maalumu wao wakaleta wanne,” alisema Kagurumjuli.

Alisema diwani huyo mmoja amepelekwa Ubungo ambako Chadema wana madiwani tisa wakuchaguliwa ambayo theluthi moja ni madiwani wanne wa viti maalumu.

Kuhusu madai ya Profesa Joyce Ndalichako na Dk. Tulia Akson kuingia katika kikao wakiwa si madiwani wa Kinondoni alisema wabunge hao ambao ni wateule wa rais makazi yao wote yako katika halmashauri hiyo.

“Profesa Ndalichako hakushiriki uchaguzi Ilala kama inavyodaiwa bali alikataliwa kwa madai kuwa nyumba zao zipo Kinondoni na  CCM ilishatoa taarifa za kuhama makazi wabunge hao mapema,” alisema Kagurumjuli.

Kuhusu madai yaliyotolewa na Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee kuwa akidi haikutimia, alisema tofauti na vikao vya kawaida, vikao maalumu huwa havina akidi bali idadi ya wajumbe wanaotakiwa ni nusu ya wajumbe wote.

“Jumla ya madiwani ni 34 na kwa kuwa kilikuwa ni kikao maalumu huwa kinaangalia nusu ya wajumbe na kwa wajumbe 18 waliokuwepo kulikuwa na uhalali wa kufanya uchaguzi kwani walivuka nusu ya wajumbe wote,” alisema.

Aliongeza kuwa walifikia uamuzi wa kuendelea na uchaguzi kwa sababu madiwani wa upinzani walifika na kwamba waliondoka pasipo sababu za msingi.

Alisisitiza kuwa sasa Baraza la Madiwani litaendelea na shughuli zake kama kawaida na endapo madiwani wa vyama hivyo hawatashiriki hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hata hivyo hakuwa tayari kutaja hatua zinazoweza kuchukuliwa kwa madiwani kutoshiriki vikao vya baraza na kusema: “Waulize wao wanafahamu hatua hizo na siwezi kuzisema kwa sababu hutekelezwa na baraza si mimi,” alisema.

Chadema

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema jopo la wanasheria na mawakili wa chama hicho wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, wamepanga kuwasilisha katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam hoja za kupinga uchaguzi huo.

“Sisi Chadema na Ukawa kwa ujumla hatuutambui ushindi wa Sitta (Benjamin) kwa sababu uchaguzi haukufuata utaratibu, akidi ya wajumbe haikutimia, pamoja na kasoro hizi bado madiwani wa CCM walipiga kura jambo ambalo linashangaza.

“Hivyo, hadi sasa tunapoongea (jana mchana) tayari mawakili wetu wakiongozwa na Lissu wapo mahakamani wakiendelea ‘ku-draft case’ (kuandaa kesi) na kesho (leo) watawasilisha hoja hizo za msingi za kupinga matokeo ya uchaguzi huo uliompa ushindi Sitta ambaye ni Diwani wa Kata ya Msasani,” alisema Makene.

Uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, ulifanyika juzi ambapo Diwani wa Msasani, Benjamin Sitta (CCM), alichaguliwa kuwa meya wa manispaa hiyo huku Diwani wa Kigogo, Mangulu Manyama kuwa naibu wake.

Hata hivyo uchaguzi huo ulisusiwa na madiwani wanaotoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo ni Chadema na CUF kwa madai haukufuata misingi ya sheria ikiwemo kuruhusiwa baadhi ya wajumbe ambao si halali.

Kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, alisema hawautambui uchaguzi huo kwa sababu haukuwa halali.

Madai mengine ya Ukawa ni uchaguzi huo kufanyika na idadi ya wajumbe ambao hawafikii akidi ambayo ambayo ni theluthi mbili ya wajumbe wote.

Imeandaliwa na Jonas Mushi, Veronica Romwald na Maneno Selanyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles