24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Museveni, Kagame wasaini makubaliano kumaliza mgogoro

LUANDA, ANGOLA

MARAIS  Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda wamesaini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Angola, Luanda kumaliza uhasama uliopo kati ya mataifa hayo jirani.

Walifikia makubaliano hayo katika mkutano wa pili huko Luanda mbele ya marais wa Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo , Angola na rais wa Congo Brazaville waliokuwa wapatanishi katika mgogoro huo.

Joto la kisiasa limekuwepo kwa takriban miaka mitatu sasa na limeathiri maisha ya watu kijamii na kiuchumi katika mataifa hayo jirani.

Maofisa nchini Rwanda wameishutumu Uganda kwa kuwafunga na kuwatesa kinyume cha sheria raia wake nchini humo wakati Uganda nayo inaishutumu Rwanda kutekeleza ujasusi katika ardhi yake.

“Tutashughulikia matatizo haya yote” Rais Kagame aliwaambia wandishi habari baada ya kusaini makubaliano hayo.

Makubaliano  hayo yamefikiwa baada ya jitihada za Angola  ikisaidiwa na DRC.

Viongozi hao wawili wamekubaliana kutilia mkazo kutatua mzozo wowote baina ya mataifa yao kwa njia amani.

Machi mwaka huu katika hotuba aliyoitoa kwenye mkutano wa kitaifa, Rais Kagame alieleza chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita nchi ya Uganda ikitaka kuangusha utawala wake.

Rais Kagame alisema mgogoro huo ulishika kasi hivi karibuni baada ya wananchi wa Rwanda wanaoingia nchini Uganda au kufanyia kazi nchini humo kushikwa na kuzuiliwa sehemu ambazo hazijulikani na kufanyiwa vitendo vya mateso huku akishtumu utawala wa Uganda kutoa nafasi ya ushirikiano kwa kundi la Rwanda National Congress linaloongozwa na mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda jenerali Kayumba Nyamwasa:

”RNC wanafanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vya usalama vya Uganda.kilicho wazi ni kwamba Wanachokifanya ni kunyanyasa wanyarwanda ambao hawataki kuungana nao huku wakiwasingizia kwamba wametumwa na utawala wa Rwanda kuhujumu usalama wa Uganda na kuuwa wanyarwanda wa upinzani.Ni madai yasiyo na msingi, lakini haya yote yanaonyesha ushirikiano wa dhati uliyopo baina ya serikali ya Uganda na kundi la RNC.” Alisema.

Uganda nayo imekuwa ikiishutumu Rwanda kuwatuma majasusi na kufanyia vitendo vya ujasusi kwenye ardhi yake,shutuma ambazo Rwanda inakanusha.

Rais Kagame amesisitiza kwamba mara kadhaa mwenyewe aliwasilisha malalamiko hayo kwa Museveni na kwamba hakuonyesha utashi wowote wa kuyatatua.

Jambo jingine lililoonyesha ishara ya kuingia kwa doa kwenye uhusiano wao, mwezi Mei Uganda na Rwanda zilishutumiana kwa mauaji na utekaji nyara wa raia wa kutoka mataifa hayo mawili.

Kutokana na uhasama huo Rwanda iliamua kufunga mpaka wake na Uganda wa Gatuna.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles