Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, ameendelea kuwasha moto baada ya kuisaidia timu yake ya  Difaa  El-Jadida kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya CR Khemis Zemamra, katika mchezo uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Grand Prix, Marrakech.
Kwa ushindi huo, Jadida imefuzu raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Ligi nchini Morocco, maarufu kama ‘Throne Cup’.
Katika mchezo huo, Msuva, aliyejiunga na Difaa Hassan El-Jadida, akitokea kwa mabingwa wa Tanzania, Yanga, alifunga bao la tatu dakika ya 62.
Mabao mengine ya Jadida kwenye mchezo huo yalizamishwa na beki Marwan Aghudy, aliyefunga la kwanza dakika ya 28 na mshambuliaji Bilal Almkra aliyetumbukiza la pili dakika ya 34.
Katika mchezo huo, Msuva alionyesha kiwango maridadi na kuisumbua vilivyo safu ya ulinzi ya CR Khemis Zemamra.
Kabla ya mchezo huo, ambao ni wa kwanza rasmi wa mshindano, winga huyo alifunga mabao sita kwenye michezo ya kujipima ubavu.
Msuva alisaini mkataba wa miaka mitatu na Jadida, baada ya kuichezea Yanga kwa msimu minne na kuisaidia kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara tatu mfululizo.
Pia amewahi kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili mfululizo, huku akiwa miongoni mwa wapachika mabao wazawa tishio kwa miaka ya hivi karibuni.
Kabla ya kutua Yanga aliwahi kupitia akademi ya Azam, aliyojiunga nayo akitokea kituo cha kukuza vipaji vya wanasoka chipukizi cha Wakati Ujao pamoja na kuichezea klabu ya Moro United, iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.