26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

Mshukiwa wa mauaji atiwa nguvuni na kuachiliwa

THE HAGUE, UHOLANZI

Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, Charles Ntahontuye Ndereyehe amekamatwa kutoka nyumbani kwake mjini Amsterdam nchini Uholanzi kisha kuachiliwa,  kimesema chama chake.

Rais wa chama cha chake cha FDU, Justin Bahunga akizunguma na BBC alieleza kuwa Ndereyehe alikamatwa kutoka nyumbani kwake ambako anaishi na mke wake . 

Kulingana na Bahunga mshukiwa huyo hata hivyo aliachiliwa na kurudi nyumbani baada ya kulala kizuizini wakati wakili wake alipoingilia kati.

Ndereyehe (70) ni mjumbe maarufu wa FDU na mkosoaji wa serikali ya Rwanda. Wakati wa mauaji ya kimbari alikuwa ni mkuu wa taasisi ya utafiti wa kilimo ya serikali iliyopo Kusini mwa Rwanda.

“Alipokuwa akikamatwa polisi walimwambia kuwa aliombwa na serikali ya Rwanda. Hicho ndicho tunachokifahamu ,” Bahunga alisema.

Polisi bado hawajatoa kauli yoyote juu ya kukamatwa kwa Ndereyehe, ambaye amekuwa akiishi nchini Uholanzi kwa miaka zaidi ya 15.

Ndereyehe anashukiwa kuwa mmoja wa watu waliopanga mauaji ya mwaka 1994 na kesi yake ilisikilizwa bila mtuhumiwa huyo kuwepo katika mahakama ya kijadi maarufu Gacaca mwaka 2008.

Mnamo mwaka 2010, Rwanda ilitoa kibali cha kimataifa cha kumkamata na alikuwa katika orodha ya watu waliokuwa wakisakwa na polisi wa kimataifa Interpol.

Wakati huo huo, Ofisi ya Upelelezi wa Uhalifu nchini (RIB) imekamilisha uchunguzi wake dhidi ya Paul Rusesabagina na itawasilisha faili za uchunguzi wake kwa waendesha mashitaka nchini humo Jumatano , umeandika wavuti wa gazeti la New Times.

Kiongozi huyo wa vuguvugu la upinzani la Rwanda, Rwanda Movement for Democratic Change (MRCD) anatuhumiwa kufanya makosa ya ugaidi, kuharibu mali kwa kuziteketeza kwa moto , utekaji nyara na mauaji.

Rusesabagina amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Paul Kagame.

Julai mwaka 2018, kundi lenye silaha la vuguvugu lake la MRCD lilidai kuwa ndilo lililohusika na mashambulio katika mkoa wa Kusini mwa Rwanda.

Rusesabagina alikamatwa  Agosti 31 katika mji Mkuu wa Muungano wa nchi za kiarabu Dubai.

Familia yake imezishutumu mamlaka za Rwanda kwa kumteka nyara na kuwakataa mawakili wake wawili wanaomuwakilisha katika kesi dhidi yake.

Akizungumza kuhusu kukamatwa kwake, Rais wa Rwanda Paul Kagame Jumapili alisema kwamba Rusesabagina hakutekwa, alidanganywa akajileta mwenyewe nchini Rwanda.

Rais Kagame alisema kwamba lazima Rusesabagina awajibishwe kuhusu mauaji dhidi ya raia wa Rwanda kufuatia mashambulio ya makundi ya waasi anayoongoza yaliyofanywa dhidi ya maeneo ya Rwanda miaka miwili iliyopita.

Rusesabagina alifahamika kufuatia filamu ya Hotel Rwanda ikielezea jinsi alivyookoa maisha ya Watutsi waliokuwa wamekimbilia katika hoteli moja mjini Kigali aliyokuwa meneja wake mwaka 1994.

Hata hivyo manusura wa mauaji ya kimbari ya Rwanda walisema katika filamu hiyo alitia chumvi juu ya hali halisi ya mauaji ya kimbari na kupotosha ukweli juu ya mauaji ya kimbari.

BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles