26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

Mauzo ya dhahabu kuzua mjadala

KAMPALA, UGANDA

KIWANGO cha mauzo ya nje ya dhahabu nchini Uganda kimeongezeka hadi kufikia mauzo ya thamani ya Dola milioni 160 ndani ya mwezi wa Juni pekee, suala lililozusha mjadala.

Tayari zimeibuka tuhuma kuhusu vyanzo halisi vya dhahabu hiyo na kama ni halali au inatoka mataifa ya jirani na nchi hiyo.

Hata hivyo mwandishi wa BBC, Isaac Mumena alinukuu takwimu za Benki kuu ya Uganda, kwa mwezi wa Juni mwaka huu na kwamba taifa hilo lilisafirisha zaidi ya kilogramu 3,000 za dhahabu ikiwa ni mara mbili zaidi ya kiwango kilichokisafirishwa mwezi uliopita.

Kuna mashaka huenda dhahabu hiyo inatokea nchi jirani ya DRC sehemu zilizokumbwa na vita na makundi ya waasi.

Mwezi uliopita, Benki ya Dunia ilikadiria kiwango cha dhahabu haramu ya thamani ya dola milioni moja kilichosafirishwa kibiashara kupitia nchini Uganda.

Inadaiwa pia kuwa kutokana na janga la Covid-19, wafanyabishara wa magendo wanatumia ndege za kukodisha kusambaza vifaa vya huduma za afya kusafirisha dhahabu za magendo.

Serikali ya Uganda imekiri kuwa haiwezi kuzalisha kiasi kikubwa kama hicho, lakini kuwepo kwa mitambo ya kusafisha dhahabu kunasababisha kuwepo kwa kiwango cha juu, Kamishina wa Wizara ya Madini, Vincent Kedi alieleza.

“Kiwango cha uzalishaji wa dhahabu nchini Uganda kimeongezeka ukilinganisha na miaka 3 iliyopita, pia tuna viwanda vitano vya kusafisha dhahabu hapa nchini, na hivi vinasafisha dhahabu ya ndani na kutoka nje ya nchi hivyo usafirishaji wa dhahabu umeongezeka kutokana na hilo,” alisema.

Kedi alikana kuwepo dhahabu ya magendo kutoka mataifa jirani kama vile DRC ndiyo imesababisha kuongezeka kwa usafirishaji zaidi, “Kwa sasa siwezi kusema ni kweli au ni uongo, ila ninachofahamu ni kwamba kiwanda cha kusafisha dhahabu kinasafisha dhahabu ya Uganda na ile inayotoka mataifa ya ukanda huu, siyo DRC pekee ni pamoja na mataifa mengine kama Sudan na mataifa mbalimbali ya Afrika.”

Aidha, Naibu wa Mwenyekiti wa Kampuni ya AGR, Alphonse Katarebe alisema tangu kuanzishwa kwa kampuni za kusafisha dhahabu nchini Uganda , kiwango cha uzalishaji kimepanda.

Licha ya kuwa Uganda haina migodi mikubwa ya dhahabu, hivi karibuni madini yamekuja kuwa mojawapo ya bidhaa kwa masoko ya nje zinazoiletea fedha nyingi za kigeni hata kuliko zao la kahawa.

Hali hii imeleta ushindani mkali miongoni mwa wanaoshiriki biashara hiyo huku wawekezaji kadhaa wakianzisha mitambo ya kusafisha dhahabu nchini ambako dhahabu huandaliwa kwa soko la kimataifa.

BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles