28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

MSAJILI AZUA JAMBO NCCR -MAGEUZI

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


BUNDI ametua ndani ya Chama cha NCCR Mageuzi kutokana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kumrudisha mwanachama aliyefukuzwa ndani ya chama hicho, Leticia Musore katika nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti (Bara).

Hatua ya Msajili wa vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kumrudisha Musore inaweza kufanana na ile aliyoifanya kwa Chama cha Wananchi (CUF) alipomrudisha aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na kukifanya chama hicho kuingia katika mgogoro hadi sasa.

Taarifa ya barua kutoka kwa Msajili kwenda NCCR-Mageuzi ambayo MTANZANIA ina nakala yake inaeleza kuwa  kwa mujibu wa Ibara ya 22 (5) (ii) ya katiba ya chama hicho, Halmashauri Kuu ya NCCR Mageuzi inayo madaraka ya kumsimamisha uongozi Makamu Mwenyekiti wa Taifa  kama ilivyofanya kwa Musore.

“Lakini kwa mujibu wa Ibara ya 22 (5) (i) Halmashauri Kuu  ya Taifa ya NCCR  haina mamlaka ya kumsimamisha mtu uanachama kwa sababu adhabu hiyo haipo katika katiba ya chama hicho,” ilieleza barua hiyo.

Katika barua hiyo Msajili alisema kutokana na vifungu vya katiba ya chama hicho Musore bado ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.

Jaji Mutungi alisema katika sakata hilo kumekuwa na ukweli kwamba Musore hakupewa fursa ya kujua tuhuma zake na kujibu kama katiba na kanuni zinavyoelekeza na ndio sababu baada ya kupitia maelezo yake, ofisi hiyo imeona kuna sababu za kumrudisha katika nafasi hiyo.

Leticia  alisimamishwa uanachama na kuvulia nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Bara na  Mwenyekiti wa chama hicho,  James Mbatia mwaka jana.

Pia maelezo ya uongozi wa NCCR yenye kumbukumbu  M-MM/MSV/VOL.111/14/40 ya September 16 ni wito  wa kikao  unaomkaribisha Leticia na hakuna tuhuma ambazo anatakiwa kujibu.

Alisema mwenyekiti huyo aliyewasilisha ajenda ndiyo mlalamikaji  katika kikao na mwendesha kikao kinachojadili malalamiko na kuchukua hatua.

Jaji Mutungi aliongeza kuwa hali hiyo inaonesha licha ya kanuni za NCCR kukiukwa hapakuwa na misingi ya haki katika kufanya maamuzi.

Alisema katika hatua hiyo hoja zilizojitokeza za Msajili kutoa hitimisho katika mamlaka ya kushughulikia malalamiko hayo yakiwa na angalizo kwamba katiba ya NCCR imebainisha fursa ya kukata rufaa ndani ya vikao vya chama imefikiwa.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa ofisi yake imewataka NCCR-Mageuzi  kuondoa tofauti zao na kuendelea na kazi na Leticia ni Makamu Mwenyekiti halali, hivyo wafanye kazi kwa pamoja.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles