28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

MAKATIBU CCM WAWACHONGEA  WAKURUGENZI

NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


MAKATIBU wa Itikadi , Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamemwomba Rais Dk. John Magufuli kuwachukulia hatua kali wakurugenzi wa halmashauri nchini wanaokiuka agizo la kutenga asilimia 10  ya mapato za uwezeshaji kiuchumi kwa vijana na wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, mara baada ya kikao chao cha kazi, Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa Kata ya Saranga Wilaya ya Ubungo, Mohamed Mjema alisema wapo baadhi ya  wakurugenzi ambao hawatekelezi agizo  hilo la Serikali linalowataka kutenga fedha hizo, hivyo kusababisha wananchi kushindwa kujikwamua kiuchumi.

“ Tunashangaa halmashauri nyingi hazitekelezi jambo hili ipasavyo pamoja na kwamba wanakusanya mabilioni ya fedha. Kwa mwaka Manispaa ya Ilala inakusanya Sh. bilioni 60 , Kinondoni Shilingi bilioni  40, Kigamboni Shilingi  bilioni 8.4 na Ubungo Shilingi bilioni 25.

“Wakati wananchi wakisubiri utekezaji wa Sh milioni 50 kwa kila kijiji ni vema wakurugezi watekeleze agizo lile la serikali linalowataka kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya vijana na wanawake,” alisema Mjema.

Mjema alisema kwa kuwa hilo halijatekelezwa wanamwomba Rais Magufuli aingilie kati ili kukomesha tabia hiyo inayofanywa na watendaji wasio waaminifu.

Alisema pamoja na hayo wamefanya tafakari ya uhai wa chama na uhalisia wa mageuzi makubwa yanayofanywa na ndani ya chama hicho.

“Lengo kuu ni kuendelea kupewa dhamana ya kushika dola na ili lengo litimie ni lazima itikadi na misingi ya chama ifahamike kwa umma,” alisema.

Alisema mageuzi makubwa yanayofanywa hivi sasa yamelenga kukirejesha chama kwa wanachama na kushughulika na kero za wananchi.

Alisema ni vyema wana CCM wakaendelea kufanya siasa ya maendeleo, ambazo zinakwenda kubadilisha maisha ya watu, siasa za chuki, husda, matusi na fitina zisipewe nafasi.

Kwa upande wake, Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa Kata ya Kurasini, Sophia Mbarouk  alisema wanampongeza Rais Dk, Magufuli kwa kasi yake ya utumbuaji majipu  na kuziba mianya ya rushwa kwani imeleta heshima ya ndoa.

Alisema wana ndoa wengi sasa wanawahi kurejea majumbani na kuzungumza na familia zao hivyo kasi ya utumbuaji iendelee.

Sophia alisema kuna changamoto nyingi za kiuchaguzi wakati wa uchaguzi lakini katika uchaguzi ujao watoa rushwa wasipewe nafasi wala dhamana katika uongozi ndani ya chama.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles