26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

MO MAMBO MAZURI SIMBA

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

KLABU ya soka ya Simba imeingia rasmi kwenye mfumo wa uendeshaji wa kutumia hisa na kuachana na ule wa awali wa uanachama uliodumu kwa miaka mingi.

Mabadiliko hayo ambayo mchakato wake ulianza mwaka jana, yalipitishwa jana na wanachama wa klabu hiyo katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Kuanza kutumika kwa mfumo huo kunatoa fursa kwa mfanyabiashara maarufu na mwanachama wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, kuwa mmiliki wa klabu hiyo baada ya kuweka wazi nia yake ya kununua hisa zenye thamani ya Sh bilioni 20.

Katika mkutano huo, wanachama 1,216 kati ya 1,217 walipiga kura ya kuunga mkono mabadiliko hayo ambayo yanafungua historia mpya ya klabu hiyo yenye makao yake makuu Mtaa wa  Msimbazi, jijini Dar es Salaam.

Muundo huo umegawanywa katika sehemu kuu tatu, wapenzi, wanachama na wawekezaji ambao kwa pamoja watatengeneza kampuni inayofahamika kama Simba Sport Club Limited.

Wawekezaji kwenye muundo huo watakuwa na fursa ya kumiliki asilimia 50 ya hisa za umiliki wa klabu hiyo, huku asimilia 50 nyingine ikimilikiwa na wanachama na wapenzi.

Katika muundo huo mpya, wawekezaji watatakiwa kununua hisa zenye thamani ya Sh bilioni 20.

Muundo wa kiutawala ndani ya mfumo huo utakuwa na bodi ya wakurugenzi itakayoongozwa na mwenyekiti pamoja na wajumbe saba ambao ni wanachama wa Simba na wawekezaji.

Ndani ya muundo huo pia kutakuwa na bodi ya ushauri ambayo itaongozwa na wazee wa klabu hiyo na nyingine itakayoongozwa na wachezaji wa zamani wa Simba.

Bodi nyingine ya ushauri ni ile ya kibiashara itakayohusisha wanachama wa klabu hiyo wenye taaluma hiyo ili kuunda utawala wa uendeshaji.

Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alisema mabadiliko hayo yanatokana na nia ya dhati ya klabu hiyo kutaka kuwa klabu bora Afrika na yenye uwezo mkubwa kiuchumi.

“Simba inahitaji kuwa klabu bora Afrika, lakini kwa mfumo tuliokuwa nao awali ilikuwa vigumu kufikia malengo.

“Lengo la Simba ni kuwa na uwekezaji ambao klabu itakuwa na uwezo wa kibajeti, miundombinu ya kisasa, shule za mpira na kumiliki uwanja wake,” alisema.

Aliongeza: “Kwa wanachama, kwa kuwa wanaonekana si wenye uwezo wa kutosha kifedha, wao wanatakiwa kuchangia Sh bilioni 4 tu ambazo ni sawa na asilimia 10, huku asilimia 40 ambazo ni sawa na Sh bilioni 16 zitawekwa kando kwa kuangalia uwezo wao hapo baadaye.

“Suala la nani atakuwa mwekezaji itaundwa kamati ya wataalamu ili kuandaa tenda na baada ya watu kujitokeza, kamati ya utendaji itaandaa mkutano kama huu na kuwaita wanachama ili kuwaeleza waliojitokeza ni akina nani.

“Wawekezaji kwenye muundo huo wanaweza kuwa wawili, watatu au vinginevyo na mgawanyo wa hisa kwa maana ya thamani na asilimia ndiyo utakaohusika.”

Naye mgeni rasmi katika mkutano huo, Naibu Waziri Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hamisi Kigangwalla, alisema Serikali inaunga mkono mabadiliko hayo kwa kuwa yana tija katika maendeleo ya soka nchini.

“Serikali itafaidika kadiri klabu zinavyorasimishwa na kuongeza kipato ambacho kitasaidia kulipa kodi.

“Serikali inaelewa changamoto zote na tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachomiliki kwa asilimia kubwa viwanja nchini, kimeanza kufanya maboresho na kuimarisha viwanja hivyo,” alisema Kigwangalla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles