23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa: Rasilimali watu ni nyenzo bora ya maendeleo

Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa ametoa wito kwa viongozi wa nchi za Afrika na wadau wa sekta ya biashara kutumia vilivyo rasilimali watu iliyopo ili kusukuma gurudumu la maendeleo kwa nchi husika.

Mkapa ametoa wito huo mwishoni mwa wiki Dar es Salaam wakati akizungumza na wanagenzi 16 waliopo chini ya mpango maalumu wa kutoa mafunzo kwa viongozi wajao (CAP) unaoratibiwa na Jukwaa la Taasisi ya Wakurugenzi na Wamiliki wa Kampuni binafsi Tanzania (CEOrt) kwa kushirikiana na Chuo cha Strathmore Business School (SBS).

Alisema hadi sasa Afrika ina watu zaidi ya bilioni 2.3, wakati idadi ya watu Tanzania nayo ikiendelea kuongezeka hadi milioni 50.

“Wingi huo wa watu unachangia vilevile katika maendeleo kama ilivyo China na India,” alisema Mkapa ambaye alikuwa mgeni mwalikwa katika mdahalo huo.

Alitoa wito kwa wanagenzi hao kuheshimu na kujifunza kwa kupitia wakongwe waliowatangulia kazini ili kupata mbinu nzuri za kiuongozi.

“Kwa mfano mimi Mwalimu Nyerere ndie aliyenitoa na kunikuza kisiasa, nilikuwa najifunza mengi kuhusu uongozi kutokana na mambo aliyokuwa akiyafanya wakati huo.

“Lakini ukishachaguliwa kuwa kiongozi unatakiwa kufanya tathmini na kupitia maamuzi yote yaliyowahi kufanywa katika nafasi uliyonayo ili usahihishe makosa yaliyotendeka na hata kuboresha kile unachoona ni sahihi kwa kampuni na taasisi unayoongoza kiujumla.

“Katika uongozi, ni muhimu kutambua watu wanaofaa kufanya kazi nao na hakikisha unawajua kabisa, hii itakusaidia katika kupiga hatua katika biashara yako.

“Vilevile uonyeshe uchangamfu katika utekekezaji wa majukumu yako,” alisema Mkapa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Majengo alisema wamemkaribisha Mkapa kutoa darasa kwa wanagenzi hao ili kuwapiga msasa kutokana na uongozi wake kuweka alama ya mageuzi katika mambo mbalimbali ambayo Tanzania inajivunia hadi sasa.

Majengo alisema baada ya kukamilisha mpango huo wa miezi 12, washiriki watakuwa wamepata mafunzo mazuri ambayo yatawasaidia kupiga hatua katika taasisi na kampuni wanazozitumikia.

Alisema kuwa CAP inakusudia kujenga watendaji na wakurugenzi wakuu wa miaka ijayo kwa kuwapatia maarifa na ujuzi stahiki wa kuongoza.

“Pamoja na utajiri wao wa maarifa na utaalamu, watendaji wakuu wa sasa wanaweza kutoa ujuzi zaidi kwa kukuza kizazi kijacho cha viongozi wa Tanzania,” alisema Majengo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles