25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Miili ajali ya MV Nyerere yaongezeka, wafikia 228

FREDRICK KATULANDA Na PETER FABIAN -UKARA

MIILI ya watu waliofariki dunia kwenye ajali ya kivuko cha MV Nyerere, imefika 228, huku wazamiaji wakidai kwa sasa wameshindwa kutoa mingine ambayo imenasa kwenye viti.

Akizungumza jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alisema mwili mmoja ulipatikana jana na mwingine juzi hivyo kufanya idadi yake kufikia 228.

Miili hiyo inaendela kutambuliwa na ndugu zao kwa kufika na kuitambua na wengine kupima vinasaba (DNA).

Hata hivyo, baadhi ya wazamiaji walisema kuna miili mingine zaidi ya mitano inaonekana kuwamo ndani ya kivuko na kwamba wanapanga kuiopoa baada ya kukiinua kivuko hicho na kutoa maji.

“Kuna maiti wengine wamo nadhani ni kati ya watano hadi sita, lakini hatuwezi kuwatoa, wamevimba na wengine wanaonekana kunasa chini ya viti,” alisema mmoja wa wazamiaji hao.

 

MALIPO KWA MANUSURA

Katika hatua nyingine, Serikali imesema haitowalipa watu wanaojitokeza na kusema pia walikuwa kwenye kivuko hicho tofauti na wale 41 waliookolewa awali.

Kamwelwe ambaye ni Mwenyekiti wa Uokoaji na Uopoaji kwenye ajali hiyo, alisema toka juzi wameshajitokeza watu zaidi ya 10 wakidai kuwa walikuwa kwenye kivuko hicho na kutaka kulipwa Sh milioni moja inayotolewa kwa manusura.

“Mimi Kamwelwe sitolipa mtu ambaye amejitokeza nje ya manusura 41 tuliowarekodi awali na kuingia kwenye taratibu za Serikali, baada ya siku chache kutangazwa nyongeza ya malipo ya kifuta machozi cha Sh milioni moja, sasa wanajitokeza baadhi ya watu kudai kuwa ni walionusurika,” alisema.

Samason Majura anayedai kuwa alishiriki uokoaji, alisema Serikali inapaswa kuhakiki manusura wa ajali hiyo kwa kuwa ni zaidi ya 41 na kwamba yeye mwenyewe aliokoa watu zaidi ya 35 na wenzake pia waliokoa watu wengine.

“Mkuu wa Wilaya Boniface Magembe siku ya awali alitangaza na wote tulimsikia akisema watu zaidi ya 100 wameokolewa, sasa walikuwaje 41?” alihoji.

Naye Bichompa Sendema, mkazi na mfanyabiashara wa Kijiji cha Bwisya, alieleza kuwa yeye ni mmoja wa manusura aliyekuwa ndani ya kivuko hicho na kwamba alipotoka alitoka pia na watu wawili aliokuwa akiwasaidia.

“Mimi nilinusurika kuzama, niliogelea na kuokoa watu wawili akiwemo mama mjamzito, hivyo siwezi kulipwa sababu sikwenda kujiandikisha, nimewaona wamekataa, lakini hata siku ya kwanza nahojiwa na waandishi nilieleza kabla hata sijajua kuna kulipwa,” alisema.

Sendema alisema hakujiandikisha kwa sababu alitoka mzima na kuokoa wengine kisha kwenda nyumbani kupumzika.

Manusura mwingine Cecilia Sabasaba, alisema alipobahatika kuogelea na kujiokoa yeye na binti mmoja wa miaka 10, aliwashuhudia vijana wengine wawili ambao walikuwa wakiokoa watu wengine, lakini pamoja na yeye hawakwenda kurekodiwa katika manusura 41 waliokolewa kwa sababu hawakuumia na hawakuona sababu ya kwenda Kituo cha Afya Bwisya kutibiwa.

Aliiomba Serikali kutumia vyombo vyake kuwahakiki ili nao wapate fedha hiyo wanayostahili sawa na wenzao.

 

WAOKOAJI NAO WAILILIA ASANTE

Mmoja wa wananchi walioshiriki kuokoa abiria ndani ya kivuko hicho, Andrew Magayi ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwashika mkono kwa hatua yao ya kujitolea.

Alisema mara baada ya ajali aliachana na bodaboda yake na kuchukua mtumbwi kuokoa watu.

Magayi alisema wakati wa uokoaji huo hakuwa peke yake, alikuwa na vijana wengine zaidi ya saba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles