23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Muhimbili yatenganisha watoto walioungana tumbo, kifua

HALIMA ALLY (TUDARCO) Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH), imefanya upasuaji wa kuwatenganisha watoto wawili wa miezi miwili wenye jinsia ya kiume, ambao walizaliwa wakiwa wameungana   tumbo na kifua.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto, Petronilla Ngiloi, alisema upasuaji huo ulifanywa na jopo la madaktari 10 na ulichukua saa tano.

Alisema madaktari sita walikuwa ni mabingwa wa upasuaji huku wanne wakiwa ni wataalamu wa dawa za usingizi na wauguzi wakiwa wanne.

Dk. Ngiloi alisema katika jopo la upasuaji, alikuwapo daktari  mmoja kutoka Ireland ambaye ni mtaalamu wa kupasua ini.

“Tumefanikiwa kuwatenganisha mapacha hawa katika upasuaji uliofanyika Septemba 23.

“Kabla ya upasuaji tulifanya uchunguzi wa kutosha kujua walivyoungana,” alisema Dk. Ngiloi.

Alisema watoto hao walifikishwa katika Hospitali ya Muhimbili, baada ya mama yao Esther Simon, kujifungulia nyumbani kwao Kisarawe Julai 12 kwa kusaidiwa na mama mkwe wake.

“Baada ya kujifungua, watoto hao walipelekwa kwenye zahanati iliyo jirani nao na baadaye walihamishiwa kwenye hospitali ya Kibaha kabla ya kuletwa Muhimbili,” alisema Dk. Ngiloi.

Alisema wakati wanafikishwa Muhimbili, walikuwa na uzito wa kilo nne na kwa utaalamu, inatakiwa watoto walioungana watenganishwe wakiwa na uzito wa chini ya kilo tisa.

“Tuliwahudumia kwa karibu mpaka walipofikia kilo  tisa kwa pamoja (kilo 4.5 kila mmoja) ndipo tulipowatenganisha.

“Tabia za binadamu zinatofautiana na iwapo mmoja atakufa bila kuwatenganisha basi watakufa wote, ndiyo maana tuliamua kuwatenganisha,” alisema.

Dk. Ngiloi alisema baadhi ya sababu za watoto kuzaliwa wakiwa wameungana ni pamoja na kuchelewa kugawanyika kwa yai lililorutubishwa ndani ya wiki nane za mimba.

“Mimba ikifikisha wiki nane mtoto hajakamilika basi hitilafu iliyokuwapo kwenye yai itafanya mtoto azaliwe nayo.

“Hivyo kuzaliwa watoto wa namna hii kunatokana na yai kutogawanyika ndani ya wiki nane za mwanzo za mimba,” alisema Dk. Ngiloi.

Aliwataka wazazi wote wenye watoto wenye hitilafu za kuungana  kuwapeleka Muhimbili wafanyiwe uchunguzi kama inawezekana kuwatenganisha wafanyiwe hivyo.

“Si kila watoto wanaozaliwa wameungana wanaweza kutenganishwa, kuna wakati inabidi kumtoa mhanga mmoja   mwingine aweze kuishi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, alisema  hospitali imefanikiwa kufanya upasuaji kwa mafanikio.

Alisema  upasuaji huo umewezekana baada ya  kuboreshwa  miundombinu ya kutoa huduma katika vyumba vya upasuaji ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wataalamu.

Prof. Museru alisema kuongezwa kwa vyumba hivyo kumesaidia kupunguza msongamano wa huduma ya upasuaji na hivyo kurahisisha utoaji huduma kwa watoto kutoka mara nne hadi mara 10 kwa wiki.

Alisema awali baada ya watoto hao kufikishwa Muhimbili, walilazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kufanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha.

Profesa Museru alisema Muhimbili iligharamia matibabu na upasuaji wa watoto hao hivyo   hawajui kiasi cha fedha walichotumia kwa upasuaji huo.

Naye  Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto, Dk. Zaituni Bokhary, alisema: “Nashauri watoto pacha walioungana au wenye matatizo ya afya waletwe Muhimbili   wafanyiwe uchunguzi wa kina na baada ya kujiridhisha tutawapatia huduma stahiki”.

Mama wa watoto hao, Esther aliwaomba wasamaria wema wamsaidie katika kuhakikisha watoto hao wanapata malezi bora na baadaye kupata elimu stahili.

“Nawashukuru   Muhimbili kwa kuwatenganisha watoto hawa kwa sababu haikuwa kazi rahisi kwangu kuishi nao wakiwa katika hali hii,” alisema Esther.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles