24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MIFUMO YA  KUTOA HAKI NCHINI IIMARISHWE ILI KUTOA HAKI

Februari 2 ya kila mwaka kumekuwa na desturi ya kuadhimisha Siku ya Sheria kitaifa hapa nchini ambapo huandaliwa dhifa fupi na hotuba husomwa na Mkuu wa Nchi na Serikali ndio huwa mgeni wa heshima.

Dhifa ya mwaka huu 2017 ilitoa sura halisi ya hali mbovu ya mfumo mzima wa kutolea haki hapa nchini ambapO Mjane Swabaha Mohamed Shosi alipenya hadi mbele alipokuwa ameketi Rais na baadaye kumweleza namna alivyodhulumiwa haki yake ya kutopewa mirathi ya Marehemu mume wake.

Katika maelezo yake mama yule pamoja na maelezo mengine alikuwa balozi mzuri wa kuelezea namna mifumo ya kutoa haki inavyominya mianya, mirija na mabomba ya kumwaga maji ya haki hapa nchini; bibi Swabaha alisikika akisema “….kwa kuwa sina uwezo au si Mtanzania ni Mkenya ndio nidhalilishwe kiasi hiki? Nakuomba Mheshimiwa unisikilize kilio changu ninacholia, si mimi peke yangu wanawake wengi wananyanyasika kwa sababu ya haki zao.. wanadhulumiwa haki zao ambazo ziko wapi, nakuomba Mheshimiwa unisaidie kilio changu kisikike”

William E. Gladstone  aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kati ya mwaka 1868 na 1894 alipata kusema kuwa “haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokataliwa” msemo ambao baadaye ulipata umaarufu baada ya aliyekuwa mpigania haki mahiri nchini Marekani wakati wa Ubaguzi wa Rangi Dk. Martin Luther King Jr. kuutumia katika barua yake ya Aprili 6, 1963 kutoka gereza la Birmingham.

Mwanamke Mjane huyu Swahaba anadai haki zake za mirathi miaka saba mfululizo bila kuipata, kwa mujibu wa maelezo yake alianza kudai mirathi tangu mwaka 2010. Kwa ufupi tu mpaka mwanamama huyo anamfikia Rais tayari haki zake zilikuwa zimekataliwa ndani ya mifumo yetu ya kutoa haki.

Mama yule aliendelea kutuhumu mifumo ya kutolea haki akidai DPP na Polisi wanashirikiana na pia Mahakama ilitoa hukumu mbili tofauti na kuendelea kusema kuwa alitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kutishiwa kuuawa! Katika hoja yake mama yule amemtaja Waziri wa Katiba na Sheria kwa jina lake, kamtaja IGP, DCI na Wizara ya Mambo ya Ndani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali! Ni wazi kuwa mama yule alizunguka kila sehemu ndani ya vyombo kusaka haki zake lakini bado akagonga mwamba.

Hizi ni tuhuma kubwa sana mbele ya vyombo vya kutolea haki ambazo zilimfikia Rais wa nchi moja kwa moja kwa mfano hai.

Kubwa zaidi ni kitendo cha mama huyo kusema kuwa wanawake wengi wanadhulumiwa haki zao ambazo zipo wazi. Huu haukuwa tu ujumbe mzito wa Rais bali ni ujumbe mzito kwa ulimwengu pia kuwa mifumo ya kutoa haki hapa nchini ina walakini mkubwa ambao sharti juhudi za makusudi zifanywe na wote wanaohusika kurekebisha kasoro za vyombo vya haki nchini.

Mama huyo Swahaba amefanyika kuwa sauti kwa wasiokuwa na sauti kuhusu dhuluma na udhalimu wanaotendewa na mifumo ya kutolea haki nchini. Sauti yake ni ishara pia kuwa hatuna mifumo mwafaka ya watu kufikisha malalamiko yao na ikapatiwa ufumbuzi pasi na haja ya kumfikia Rais! Moja ya njia ya kutoa malalamiko ni kuruhusu maandamano ya amani na makongamano ili kuruhusu watu kutoa yaliyowajaa moyoni.

Lazima tujenge utamaduni wa kuwasikiliza watu walioonewa na kudhulumiwa ili kuwatafutia ufumbuzi wa kudumu na si kuwaminya wasisikike na kupata sauti zao. Ni matumaini yangu kuwa Rais ataliangalia suala la huyu mama kama picha halisi ya mzigo mkubwa unaolielemea Taifa katika mifumo ya kutolea haki. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles