27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

TUNAJIFUNZA NINI KWA HATUA ZA NIDHAMU CCM?

MWISHONI mwa wiki iliyopita Chama Cha Mapinduzi kilifanya mikutano yake miwili muhimu. Mkutano wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu. Mkutano wa kwanza ulihitimishwa kwa wajumbe kukubaliana kuwawajibisha wanachama wenzao ambao kwa mujibu wa Katibu Mwenezi  wa chama hicho, Humphrey Polepole, walikuwa wamekiuka maadili na wamevunja katiba ya chama na kanuni zake lakini pia  mwongozo wa wanachama. 


Orodha ndefu ilitajwa ya walioadabishwa kufikia wanachama kumi na wanane ambao wengine ni viongozi  wa chama ngazi ya wilaya, mkoa, jumuiya za chama na hata halmashauri kuu yenyewe.


Hatua hii imepongezwa na baadhi ya watu walioona kuwa chama kinataka kurejesha nidhamu na pia kurudisha hadhi yake  ya kinidhamu ambayo ilionekana kupotea. Mimi niliamua kuangalia kwa undani kidogo hatua hii. Nilipata maswali ambayo kwa  bahati mbaya sijapata wa kunijibu. 


Katika baadhi ya maswali niliyokuwa nayo ni muda  uliochukuliwa kufikia adhabu hizo, iwapo kweli kosa mojawapo ilikuwa ni usaliti wakati wa  uchaguzi mkuu. Nimeona kama baadhi ya wahusika hata kama walikuwa wamekosea wakati wa uchaguzi waliendelea kuwa wanachama na hata kupangiwa nyadhifa  na wengine wakipewa balozi kabisa na wengine wakiwa wabunge. 


Swali jingine ilikuwa ni la kimchakato. Nilipomsikiliza Katibu Mwenezi Polepole akizungumza na waandishi wa habari nilitamani ningekuwa mmoja wa waandishi hao nimuulize kwa kiasi gani watuhumiwa hao walipata fursa ya kujieleza na kujitetea kabla ya hukumu zao hizo kutolewa. Pia ikumbukwe kuwa ilisemekana chombo kilichowahukumu ndicho cha mwisho na hawana mahali wanapoweza kukata rufaa katika mfumo wa chama.


Hata hivyo hoja yangu ya leo si hasa kujadili yaliyoendelea katika Chama Cha Mapinduzi na jinsi walivyopeana adhabu. Ninataka kuona ni kwa kiasi gani tunaweza kupata funzo kubwa kutoka katika tukio hilo. Katika watu ambao wamenigusa katika adhabu hizo na hasa kama adhabu zao zinatokana na uchaguzi mkuu ni Sophia Simba ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa CCM na kwa hivyo amekuwa Mbunge, pamoja na Nchimbi na Kimbisa.

Hawa watatu  kama sikosei walionekana kuonyesha hisia zao wakati wa uchaguzi mkuu  wa mwaka 2015, wakati Waziri Mkuu wa zamani jina lake lilipodondoshwa  katika kinyang'anyiro cha kuwania Urais.  
Sijui kama walihusika pia na kuhamasisha wimbo ulioonekana kumkera sana Mwenyekiti wao wa sasa ulioimbwa kwa  kuwa na imani na mtu ambaye si Mwenyekiti. Mwenyekiti huyu wa sasa amesikika mara kadhaa akisema ingekuwa ni yeye amefanyiwa hivyo asingekaa kimya. Adhabu kwa mmoja imekuwa kusamehewa, mwingine kupewa onyo na mwingine ambaye ni mwanamama pekee kufukuzwa chama.


Huyu mwanamama aliyefukuzwa chama  yuko ndani ya chama hicho kwa muda sasa na ameshika nyadhifa kadhaa ikiwamo kuwa Waziri. Wakati anafukuzwa chama ni Mbunge na pia  ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa CCM.

Hivi hii jumuiya imehusikaje katika  uamuzi huu wa halmashauri kuu? Wanawake wa CCM waliomchagua huyu kuwa kiongozi wao wana nafasi gani katika uamuzi wa  chama ngazi ya halmashauri kuu pale  Mwenyekiti wao anapoadhibiwa kiasi hiki? Hili swali karibu nijijibu mwenyewe kwani wanawake hao wa jumuiya ya chama huenda wakasema halmashauri kuu kama chombo cha chama kikisema wao hawana cha kuongezea.

Ninasema nikikumba  mwaka fulani aliyekuwa  Katibu Mkuu wa chama hicho aliwahi kuwahutubia wanawake wa jumuiya hiyo kule Tanga na ikasemekana  aliwaambia chama chao hakiko tayari kuongozwa na mwanamke na wanawake hao walimshangilia wakati mimi niliona wengi kati yao wakiwa na uwezo mkubwa wa kuongoza ngazi ya Taifa.. 


Kwa hili la Mwenyekiti wao kutimuliwa wakati wenzie wakisamehewa mimi sihusiki lakini ninapata kigugumizi kwa vile huyu ana wanachama wengi sana nyuma yake waliomchagua kuwa mwenyekiti wao. Nafasi yao ni ipi katika uamuzi huu? Hiki si chama cha kwanza kutimua wanachama ambao  ni wabunge wengine waliochaguliwa na majimbo yao kabisa. Ndio maana kuna ambao walikimbilia mahakamani na wakasemekana kuwa ni wanachama wa mahakama.


Kufikia hapa ndipo ninapotaka tuangalie iwapo tunajifunza nini. Kwa Jumuiya ya Wanawake wa CCM  hawa ni wanachama wa CCM na pia ni wanachama wa jumuiya hiyo ambayo ni ya chama. Uamuzi wao umeingiliwa tayari na chombo cha juu katika chama. Hii imenikumbusha mwaka ule mfumo wa vyama vingi ulipoingia nchini.

Tulijaribu kusema kuwa UWT isiwe jumuiya ya chama  bali kiwe chombo cha wanawake wote Tanzania. Tulidhani kuwa wanawake wa Tanzania wana sababu ya kujiunga katika umoja wao bila kujali itikadi za vyama vyao kwani masuala ya wanawake yanawagusa wanawake bila kujali wako katika chama au la. Umoja huo wa wanawake ungejikita katika kupambana na mfumo dume na uonevu wa wanawake wote na ubaguzi na hata unyanyasaji. Hili halikukubalika na umoja huo ukaendelea kuwa jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa mfano kama jumuiya haikuridhika mwenyekiti wake kufukuzwa uanachama wanaweza kufanya nini wakati tayari imesemekana hakuna rufaa?


Jambo jingine ni hili la mbunge kufukuzwa chama na hivyo kupoteza nafasi yake ya ubunge. Hapa ndipo pale tulipodhani na tunapoamini majibu yake au dawa yake  ni uwepo wa Katiba ambayo itaweka masuala kama haya sawa. Suala la mgombea binafsi nalo lingeweza kutatua tatizo hili. Mgombea akiwa hana chama wajibu alionao ni kwa wale waliompa kura tu. Kwa hali ilivyo sasa wananchi waliompa mbunge kura zao wanaweza kujikuta hawana mbunge kwa vile chama chake kimeamua kumuondoa hata kama wanampenda na kumtegemea kiasi gani.  Chama kikisimama wapiga kura hawana chao pamoja na kuwa wao ndio wengi na wenye uamuzi kwa ngazi hiyo ya jimbo.


Kuna wakati ni muhimu kabisa kuvaa miwani ya kijinsia na kuona iwapo ufukuzwaji wa Sophia kama ilivyokuwa kwa Anne Kilango ni kutokana na mtazamo  wanaotazamwa wanawake au la?  Wanawake wakikosea makosa yao huonekana zaidi  ya wanaume. Huu ni ukweli katika jamii yetu hii yenye mfumo dume uliokomaa. Na ukweli katika hili niliona mtu mmoja katika mtandao wa kijamii akisema “huyu mama Sophia alijitakia alionyesha sana msimamo wake" Sidhani kuwa huyu pekee ndio alionyesha msimamo wake.

Walikuwa wengi na wanaume walikuwa wengi zaidi nadhani. Ingebidi  warejee ule mkutano wa uchaguzi ambapo karibu nusu ya ukumbi ndio waliokua wanaimba wana imani na mtu asiye mwenyekiti. Wale wote ilibidi nao waingizwe katika mkumbo huo. Sophia ameponzwa na kuwa mwanamke. Sauti yake  na uwazi wake ndio umeleta shida nadhani labda kama kuna yaliojificha. Wapo ambao hawakuweza kuwa wazi bali nao walikuwa na  msimamao huo huo.

Tukija kwa mtazamo wa haki ya kutoa maoni na haki ya kuwa na maoni  hapa pia kama hayo nilioyasikia ndio sababu naona kuna shida pamoja na kuwa chama kinataka kuondokana na wasaliti. Ni vyema  chama kingepokea hisia zilizoonyeshwa na maneno yaliyonenwa na kutafuta funzo kwa  mambo  kuwa kinyume cha matarajio. Badala ya kufukuzana ni  kujaribu kuwaelewa na kutafuta kinachohitajika ili chama kiaminiwe na wanachama. Haya ni maoni yangu na kwa vile pia sina taarifa  za ndani sana ninasikitika tu kuwa kulikuwa na uwezekano wa kusamehewa lakini nafasi hii imetumika kwa mmoja tu hasa ukitilia maanani kuwa wanawake wako wachache katika nafasi nyingi na hata bungeni.

Nataka kuamini pia kanuni za asili zilifuatwa na hawa waliokosa nidhamu walihojiwa na wengine kutokana na walivyojieleza ikatokea kuwa wapewe onyo au wafutiwe uongozi au wafukuzwe kabisa. Kama hilo lilifanyika huenda itakuwa kitambo kidogo kwani mmoja wa walioadhibiwa yuko nje ya nchi na amepewa onyo na kutakiwa aombe radhi wanachama wenzake akiwa huko huko ughaibuni. Alihojiwa kweli huyu?

Tujifunze katika hili kwa kuona umuhimu wa kuhuisha mchakato wa Katiba Mpya ili maswali mengine hapa yajibike. Ningependa kuwasikia UWT katika hili. Lile wazo la kuwa na Jumuiya ya Wanawake wote wa Tanzania pia ni vizuri tulifikirie tena hata kama walio kwenye vyama hivyo watabaki na jumuiya zao. Suala la mgombea huru ni muhimu zaidi kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote. Kujisafisha napo ni tabia njema ila iwe katika usawa. Katiba Mpya ni Jawabu.

Imeandaliwa na  Dkt.Helen Kijo-Bisimba Mkurugenzi Mtendaji  LHRC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles