24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

ASANTE MAGUFULI KWA KUIKATAA EPA LAKINI… 2

KATIKA sehemu ya kwasnza ya makala hii  nilimshukuru na nilimpongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuukataa mpango wa EPA. Nilimpa shukrani na pongezi hizo nikionyesha ubaya wa mpango huo kwa uchumi wa nchi kama Tanzania ambayo inajizatiti kujenga uchumi wa viwanda.

Hata hivyo, nilionyesha kuwa kuna mambo kadhaa ambayo hayajakaa sawa kuhusiana na hilo.

Moja kati ya mambo ambayo hayajakaa sawa ni jinsi ambavyo tumechelewa kuukataa mpango huo. Kimsingi, majadiliano yenye mwelekeo huu wa EPA, ambayo baadaye yakazaa EPA, yalianza katikati ya miaka ya 1970. Tangu wakati huo, vipengele vibaya kibiashara vilikuwapo, lakini cha ajabu nchi zetu zikaendelea si tu kujadili kuhusiana na vipengele hivyo, bali walifikia makubaliano na kutaka kusaini. Kama si Rais Magufuli kugoma, Tanzania nayo ingekuwa imesaini makubaliano hayo mwaka jana pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Inashangaza kuwa jambo hilo liliachwa na viongozi wetu liendelee kwa jinsi lilivyo hadi kufikia hatua ya kutaka kutuingiza mkenge mwaka jana.

Kutokana na viongozi wetu kuruhusu nchi zetu kujadili makubaliano hayo yenye vipengele vinavyotukwamisha, wakaruhusu nchi za Afrika zigawanyike. Wengi tunaufahamu ule msemo maarufu wa Kiingereza wa ‘divide and rule’. Wazungu waliutumia wakati wa viongozi wetu walipokubali kuingia kwenye majadiliano ya EPA.

 

Matokeo yake, kwa mfano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakati Tanzania na pengine Uganda ambayo Rais wake naye ametaka kuwapo majadiliano ya kina kuhusu EPA, zimeonyesha kutokubaliana na mpango huo, wenzao wa Kenya na Rwanda tayari wameshasaini kwa kuonyesha kukubaliana nao.

Kwa kuwa EAC iliingia katika majadiliano kama kundi, sasa hivi unaweza kutokea mgongano mkubwa baina ya wanachama wake ambao wana misimamo inayokinzana katika jambo hilo. Hii ni kwa sababu licha ya kuukubali, lakini Kenya na Rwanda hazitaweza kuutekeleza mpango huo pamoja na  nchi nyingine zote za EAC ziukubali pia.

Hili ni jambo baya sana kwa sababu kwa kuruhusu majadiliano haya yadumu kwa muda mrefu tumewapa nchi za Ulaya mwanya wa kutugawanya ili waweze kututawala kwa urahisi.

Itakuwa ni vigumu sana kwa Afrika Mashariki kukubaliana kuhusiana na mpango huo. Katika mazingira haya ya sasa ambapo Tanzania na Uganda zinaupinga huku Kenya na Rwanda zikiwa zinakubaliana na mpango huo, mgongano mkubwa baina ya wanachama wa EAC hauepukiki.

Sioni namna ambavyo Rais Magufuli anaweza kugeuka jiwe na kukubali kusaini EPA kwa jinsi ilivyo sasa na lakini pia sioni ni kwa namna gani Rwanda na Kenya zitakubali kuachana na mpango huo eti kwa sababu tu wanachama wenzao wa EAC hawaupendi.

Somo jingine linalopatikana hapa ni kuwa kama nchi tunapaswa kuwa na sera ya kiuchumi na sera ya mambo ya nje inayoeleweka na kukubalika. Suala hili la EPA linaonyesha misimamo inayokinzana ya uongozi wa awamu ya tatu, ya nne na sasa ya tano.

Wakati Rais Benjamin Mkapa akifahamika kuwa anaupinga mpango huu, Rais Jakaya Kikwete aliyemfuata baada ya Mkapa aliendeleza majadiliano kiasi cha kufikia kutaka kusaini lakini hali imegeuka ghafla baada ya aliyempokea kijiti, Rais Magufuli, kuonyesha kutokubaliana na mpango huo.

Hali hii haitoi sura nzuri. Ingawa inaweza kuwa ilisababishwa na mambo ambayo yapo nje ya mikono yetu, lakini kama nchi tulipaswa kulifahamu jambo hili na kuliwekea msimamo thabiti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles