23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mgombea Mwenza Chadema ataja vipaumbele

Ramadhani Hassan – Dodoma

MGOMBEA mwenza wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Salum Mwalimu, amesema kama Tundu Lissu atakuwa Rais,  vipaumbele vyake ni ajira kwa vijana na kuboresha maisha ya waandishi wa habari.

Akizungumza kwenye ofisi za Chadema Kanda ya Kati jana, alisema “kama nitachaguliwa nitamshauri vizuri Rais wangu na moja ya jambo nitakalomshauri ni Wizaya ya Vijana kuwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais, pia nitaboresha maisha ya waandishi wa habari kwani nimekaa huko na kuishi maisha ambayo wanaishi waandishi.”

MNYIKA NA RATIBA YA LISSU

Katibu Mkuu wa Chadema, John Manyika, akizungumza kabla ya kumkaribisha Lissu,  alisema mara baada ya zoezi la kutafuta wadhamini Dodoma kukamilika, leo Lissu ataelekea mkoani Singida.

“Kesho (leo) Lissu atakuwa mkoani Singida kwa ajili ya kutafuta wadhamini niwaombe tujitokeze kwa wingi.

LEMA AOMBA KAZI KWA LISSU

Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, alisema kwamba endapo Lissu atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania anaomba kazi ya kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ili anyooshe mambo.

“Nipo na wewe usiku na mchana na endapo ukipata urais nipo hapa ndio maana heshima imeongezeka kwako naomba Uwaziri wa Mambo ya Ndani ili nikanyooshe kule nilipopita,”alisema.

Naye, Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa wa Chadema, Peter Msigwa, alisema Lissu ni tumaini jipya kwa Watanzania ambao walipoteza tabasamu kwa muda mrefu.

“Mungu anataka haki tumepata tumaini la wanyonge  safari hii hatukaa kimya kumwachia mungu tunataka kurejesha tabasamu na tumaini pekee la kurejesha tabasamu hilo ni Lissu.Lissu tupo nyuma yako kwa kila hali,”alisema.

LISSU NDIYE ATAKAETUOKOA

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, John Heche, alisema mtu atakayeweza kuwaokoa Watanzania,   ni Lissu.

“Lissu wakati ukiwa haupo hakuna mtumishi ambaye ameongezewa mshahara, tunamshukuru sana Mungu uliondoka na machela na mimi nilikusindikiza leo umerudi unatembea tunamshukuru sana mungu,”alisema.

MAELEKEZO YA NEC

Awali akitoa maelezo kabla ya kukabidhi fomu  kwa wagombea wote, akiwemo Lissu  Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera alisema fomu namba 8A inatumika kwa ajili ya uteuzi wa wagombea kiti cha Rais na Makamu wa Rais ambayo imeandaliwa na Tume.

“Mtawapatia seti nne ya fomu namba 8A ambayo ni fomu ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha urais na Makamu wa Rais na kila seti kutakuwa na nakala 10 za fomu hizo ili kuwawezesha kujaza idadi ya wadhamini inayotakiwa,”alisema.

Alisema  kuwa watatakiwa kudhaminiwa na wapiga kura wasiopungua 200 ambayo wamejiandikisha kupiga kura katika kila mkoa kwenye mikoa 10 na kati ya hiyo angalau miwili kutoka Zanzibar.

“Majina ya wadhamini katika seti zote yanatakiwa kufanana, pia mtapaswa kuwasilisha fomu za uteuzi kwa wasimamizi wa uchaguzi wa jimbo kule ambako mtaenda kutafuta wadhamini ili watoe uthibitisho kwa wadhamini hao, Tume imeshawapatia wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo yote nakala tepe na orodha ya wapiga kura wa majimbo yote ili waitumie kwa kazi hiyo.

 “Kutakuwa pia na tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi kwa ajili ya Rais ambapo mtapatiwa fomu namba 10, pia kutakuwa na nakala nne kwa ajili ya mgombea wa Kiti cha Rais na nne kwa mgombea wa kiti cha Makamu wa Rais.”

Alisema  kuwa maadili hayo yameandaliwa na kuridhiwa na vyama vya siasa ili kuweka msingi wa uchaguzi ulio huru, haki na wenye amani.

Hata hivyo, aliwataka kurekebisha barua ya kuwatambulisha wagombea hao iliyowasilishwa Tume kutokana na kutoweka jina la Mgombea Mwenza kwenye barua husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles