25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Urais 2020 waja na rekodi mpya

MWANDISHI WETU

WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikitarajia kufunga pazia wiki ijayo kwa  wagombea kutoka vyama mbalimbali kuchukua fomu ya nafasi ya urais, idadi ya waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hadi sasa inaelekea kuvunja rekodi ile ya mwaka 2015. 

Hadi kufikia jana tayari wagombea nane kutoka vyama mbalimbali walikuwa wamefika NEC kuchukua fomu hizo, huku wengine wakitarajiwa kuchukua kesho na wiki ijayo.

Waliojitokeza kuchukua fomu hizo jana, ni  mgombea wa nafasi ya urais, kupitia Chama cha Sauti ya  Umma (SAU) Mutamwega Magaiwa aliyekuwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Safia Berwa.

Mwingine aliyefika kuchukua fomu hiyo ni mgombea wa ACT, Wazalendo, Bernard Membe aliyekuwa ameongozana na mgombea mwenza wake pamoja na mgombea urais wa chama hicho upande wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Chama kingine kilichochukua fomu jana katika ofisi za NEC  ni chama cha Alliance For Democratic Party (ADC) ambapo mgombea wa nafasi ya urais, Queen Sendiga naye aliambatana na mgombea mwenza wake, Shoka khamis Juma.

Chama kingine kilichochukua fomu jana ni Chama cha United Democratic Party (UPDP) ambapo mgombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho,Twalib Ibrahim Kadege  alifika katika Ofisi za NEC akiwa na mgombea mwenza, Ramadhan Ally Abdallah.

Pazia la uchukuaji fomu za kugombea nafasi ya urais lilifunguliwa Jumatano, Agosti 5 mwaka huu ambapo  mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima(AAFP), Seif Maalim Seif alikuwa wa kwanza kufika  katika ofisi hizo akiwa ameambatana na Mgombea Mwenza wake Rashid  Rai na baadhi ya  wanachama wa chama hicho.

Mgombea wa pili aliyefika kuchukua fomu ya kugombea urais katika ofisi hizo ni  kutoka Chama cha Democratic Party(DP), Philipo Fumbo ambaye  alitinga katika ofisi hizo saa 5:30 asubuhi akiwa peke yake bila mgombea mwenza, Zainab Juma Hamisi.

Mgombea wa tatu alikuwa  kutoka Chama cha NRA, Leopard  Mahona ambaye  alifika katika ofisi hizo saa 6:30 mchana  na mgombea mwenza wake, Hamis Ali Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alichukua fomu juzi katika Ofisi za NEC ambapo aliambatana na mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan,Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa,Spika wa Bunge na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM wakiongozwa na Katibu Mkuu,Dk.Bashiru Ally.

Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 waliojitokeza kuchukua fomu NEC kuwania urais waliokuwa ni wagombea  nane tu.

Wagombea hao ni  Anna Mghwira aliyegombea kupitia chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo),  Chifu Lutalosa Yembe wa Alliance for Democratic Change (ADC), Edward Lowassa aliyegombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika orodha hiyo alikuwemo pia Fahmi Dovutwa wa chama cha  United People Democratic Party (UPDP), Hashim Rungwe wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Janken Kasambala wa National Reconstruction Alliance (NRA).

Pia alikuwepo John Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Machmillan Lyimo wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP) .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles