24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wachukua fomu ya urais wakiwa peku, wasujudu

RAMADHAN HASSAN -DODOMA

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mgombea wa nafasi ya urais, kupitia Chama cha Sauti ya  Umma (SAU) Mutamwega Magaiwa na mgombea mwenza Safia Berwa  na baadhi ya wapambe wa chama hicho  jana walifika katika  ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC) ,Dodoma kwa ajili ya kuchukua fomu za kugombea urais  huku  wakiwa hawajavaa viatu.

Wakiongozwa  mgombea wa nafasi ya urais kupitia SAU Magaiwa na mwenzake kabla ya kuingia katika jengo la NEC huku wakiwa hawajavaa viatu wote waliinama na kusujudu ardhini na kisha kuelekea katika chumba ambacho kipo ghorofa ya tatu kwa ajili ya kuchukua fomu.

Baada ya kutoka kuchukua fomu huku wakiwa na mkoba waliinama na kusujudu tena na kisha, Magaiwa kuanza kuzungumza na Waandishi wa Habari ambapo alieleza sababu ya kusujudu na kutokuvaa viatu ni kutokana na ardhi kuwa ndio kila kitu.

Alisema wao ni watoto wa wakulima na siku zote mkulima halimi akiwa kavaa viatu hivyo waliamua kuvua viatu ili kuwawakilisha wakulima wote kwamba wanawaheshimu na wao wapo kwa ajili yao.

 “Tumeanza  na Mungu na tutamaliza na Mungu, vipaumbele vyetu ni amani sisi ni watoto wa wakulima na mkulima halimi na kiatu kuna watanzania wengi wana shida na hadi leo hawana viatu na sisi hadi leo tupo kwa ajili ya wanyonge.

VIPAUMBELE

Alisema vipaumbele vyao ni kilimo, amani, upendo na umoja hivyo watapigania kuhakikisha bei za mazao ya pamba, kahawa na korosho zinakuwa shilingi 5000 kama ilivyo katika soko la dunia.

“Mkulima wa pamba  apate bei ya shilingi 5000 bei ya dunia kahawa 5000,korosho 5000 na ndio maana leo tumesujudu kuhakikisha kwamba amani itatawala na kila kitu kwenye dunia hii ni ardhi, nyumba ni ardhi kila kitu ni ardhi. Ardhi ndio mama ndio baba wa kila kitu,”alisema.

MARA YA PILI KUGOMBEA

Magaiwa alisema hii ni mara yake ya pili kugombea urais wa  ambapo mara ya kwanza aligombea mwaka  2010 lakini bahati mbaya kura hazikutosha.

Alisema huu sasa ndio wakati wa kuchapa kazi kama Watanzania watamuamini na kumpeleka Ikulu kwa kumpigia kura.

“Mimi ni mkulima, mtoto wa mkulima  kutoka Mkoa wa Mara nimekuwa bungeni kwa miaka 10 wakati  huo nikiwa Waziri mwambata enzi za Mkapa (Marehemu Benjamini Mkapa)   nimepata uzoefu wa kutumikia Nchi yangu na pia nimewahi kugombea urais mwaka 2010 lakini kura hazikutosha nikavumilika kwa miaka 10 sasa ninarudi kwa nguvu mpya kuhakikisha kuwa nafanya ukombozi wa kweli kwa Watanzania,”alisema.

Pazia la uchukuaji fomu za kugombea nafasi ya urais lilifunguliwa Jumatano, Agosti 5 mwaka huu ambapo  mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima(AAFP), Seif Maalim Seif alikuwa wa kwanza kufika  katika ofisi hizo akiwa ameambatana na Mgombea Mwenza wake Rashid  Rai na baadhi ya  wanachama wa chama hicho.

Mgombea wa pili aliyefika kuchukua fomu ya kugombea urais katika ofisi hizo ni  kutoka Chama cha Democratic Party(DP), Philipo Fumbo ambaye  alitinga katika ofisi hizo saa 5:30 asubuhi akiwa peke yake bila mgombea mwenza, Zainab Juma Hamisi.

Mgombea wa tatu alikuwa  kutoka Chama cha NRA, Leopard  Mahona ambaye  alifika katika ofisi hizo saa 6:30 mchana  na mgombea mwenza wake, Hamis Ali Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alichukua fomu juzi katika Ofisi za NEC ambapo aliambatana na mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan,Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa,Spika wa Bunge na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM wakiongozwa na Katibu Mkuu,Dk.Bashiru Ally.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles