25.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

Waziri Mpango aipongeza TRA

Mwandishi wetu

Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kazi nzuri inayoifanya kuongeza makusanyo ya mapato na kuitaka kuongeza makusanyo ya kodi hadi Trilioni mbili kutoka wastani Sh. Trilioni 1.5 kwa mwezi ambazo inakusanya sasa.

Waziri Mpango ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea banda la TRA katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika Kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

“Nawapongeza lakini bado ningependa serikali ikusanye Trilioni mbili kwa mwezi. Uwezo wa kukusanya kiasi hicho upo”, amesema Waziri wa Fedha na kuishauri TRA kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha mapato yanaongezeka kufikia kiwango hicho.

Amesema kwamba lazima nchi ijitegemee kwani ina uwezo wa kuondoka katika uchumi wa kati na kufikia uchumi wa juu endapo dosari ndogondogo zilizopo katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato zitaondolewa.

Waziri Mpango pia amesema kuwa uchache wa makusanyo ya kodi unatokana na kuendelea kuwepo kwa watu wanaokwepa kodi hivyo ni lazima TRA idhibiti upotevu wa vyanzo vya mapato na iongeze wigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipakodi kwani pamoja na Tanzania kuwa na watu takriban milioni 60 ni watu takribani milioni mbili wanalipa kodi.

Katika kuongeza makusanyo ya mapato, Waziri Mpango ameiagiza TRA kukusanya kwa ufanisi kodi ya majengo ambapo amesema kwamba majengo ni mengi ila kodi inayokusanywa ni kidogo mno hivyo kuna haja ya kuweka mkakati kuhakikisha majengo yote yanayostahili kutozwa kodi yanalipa kodi.

Ameongeza kwamba mapato yataongezeka endapo watumishi wasio waadilifu hususan katika Idara ya Forodha watashughulikiwa ikibidi kuwafukuza ili wabaki wachache waadilifu kwani ni eneo ambalo linalalamikiwa sana.

Katika hatua nyingine, Waziri Mpango amempongeza kwa kipekee Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo kwa jitihada anazofanya kuelimisha umma kuhusu masuala ya kodi na kushauri nguvu zaidi iendelee kuelimisha wananchi namna nzuri ya kulipa kodi na kuwasilisha ritani za kodi.

Amesema kwamba kutokana na kiwango cha elimu kwa wananchi kuwa kidogo TRA haina budi kuwa rafiki, kuwasikiliza na kuwaelimisha walipakodi namna nzuri ya kulipa kodi na kuwa sehemu ya kuwasaidia kukuza biashara badala ya kufunga biashara ili kupata mapato zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles