26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

MCHUNGAJI MSIGWA AMVAA AG

Na ELIZABETH HOMBO-DODOMA


MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), amemvaa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kwa kile alichodai anaingilia majukumu ya Mnadhimu wa Serikali.

Mchungaji Msigwa alitoa kauli hiyo jana bungeni, baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu, ambapo aliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kwa kutumia Kanuni ya 64 (1).

Katika mwongozo huo, alihoji wanadhimu wa Serikali wako wangapi kwa sababu Masaju amekuwa akiingilia majukumu ya wengine, wakati yeye ni mshauri wa Serikali.

“Mheshimiwa mwenyekiti, naomba mwongozo wangu kwa Kanuni ya 64 (1), lakini pia nitaisoma na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 64 (1) bila kuathiri masharti ya ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge.

“Ibara ya 100 inasema; kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote au mahakama au mahali pengine popote.

“Na 59 (1) ya Katiba inasema; kutakuwa na Mwanasheria  Mkuu wa Serikali kufanya kazi ya uwakili na katika majukumu yake ndiye mshauri wa Serikali, hivyo atawajibika kuishauri Serikali.

“Mheshimiwa mwenyekiti, hivi karibuni kumekuwa na mazoea au utamaduni ambao AG ambaye namheshimu sana, amekuwa akifanya kazi ya Mnadhimu wa Serikali, hivi sasa huwezi kutofautisha kama yeye ni Waziri wa Sheria au Mnadhimu wa Serikali kwa sababu kazi anayofanya si ya Mwanasheria Mkuu.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni mtu uliyebobea katika sheria na ulikuwa AG,  una authority (mamlaka) katika nchi hii. Huyu wa sasa anaingilia hata mambo ya lugha wakati si kazi yake. Yeye ni mshauri wa serikali kwa anayoyafanya sasa anashusha hadhi ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuna siku ulisema tunatakiwa tuwe na wivu na Bunge.

“Sasa mwongozo wangu, ni kwamba je Serikali ni wanadhimu wawili? Nimwombe Profesa Kabudi (Waziri wa Katiba na Sheria), hebu tulinde mhimili huu,”alisema Msigwa.

Akitoa mwongozo kuhusu hilo, Chenge alisema hakuna kinachomzuia Mwanasheria Mkuu wa Serikali au waziri yeyote kusimama, kutoa ufafanuzi au maelezo kuhusu jambo lolote.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,926FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles