27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MADEREVA WA MALORI   WAFUKUZWA ZAMBIA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


MADEREVA na wafanyakazi wa malori yanayoshikiliwa Zambia wameanza kufukuzwa nchini humo.

Kwa zaidi ya miezi miwili sasa malori hayo 600 yaliyokuwa na magogo yakisafirishwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuja Tanzania yamekwama nchini humo baada ya kushikiliwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Maroli Tanzania (TATOA), Elias Lukumay, alisema madereva hao wamefukuzwa kwa kile kilichoelezwa kuwa vibali vyao vya kusafiria (viza) vimekwisha muda wake.

“Kuna hali ya sintofahamu, madereva wengine wamefukuzwa kwenye magari viza zao zimekwisha kwa hiyo wanahangaika…Watanzania wenzetu wanateseka na wamiliki wa malori tunazidi kufilisika,” alisema Lukumay.

Kwa mujibu wa Lukumay, kuna madereva 600 na wafanyakazi 600 ambao wanaishi katika mazingira magumu tangu malori hayo yakamatwe.

Alisema pia kuwa baadhi ya familia za madereva hao zimeanza kupiga kambi katika ofisi za chama hicho wakitaka kujua hatima ya ndugu zao.

“Tangu juzi kuna familia za madereva zimeanza kuja ofisini wanalalamika hawana mawasiliano na waume zao na wana hali ngumu.

“Hatuoni ‘initiative’ ya uhakika kutoka Serikali za Zambia katika kushughulikia suala hili,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya FP, Peter Kirigini alisema  ni vema Serikali iongeze nguvu  kushughulikia suala hilo kwa sababu  hata kwa upande wa Zambia Rais wao, Edgar Lung, alikwenda hadi kwenye mpaka wa Nakonde na kuzungumza na madereva wa Tanzania.

 “Licha ya kupoteza biashara, pia magari yetu yanaharibika kwa sababu ulinzi wake haupo mikononi mwetu, hadi funguo za magari wamechukua. Kama yanaendelea kukaa kwenye mikono ya watu wengine, je yatakuwa na hali gani?

“Uvumilivu hapa ulipo umefika mwisho na matatizo yanaendelea kuongezeka, baadhi ya madereva walikaa sana porini uvumilivu umewashinda wameamua kurudi,” alisema,   

  Mkurugenzi wa Kampuni ya Panatlantic Geo Freight, Jumanne Brash, alisema kuna hatari ya kufilisiwa kwa sababu  wengi wao walikopa fedha benki kuongeza mitaji yao.

“Hili ni janga la taifa kwa sababu siku zinazidi kusonga na madereva wetu wanapata shida, wengine tumechukua mikopo benki na kama gari imesimama miezi miwili tutapeleka nini benki?

“Benki hawaelewi kwamba serikali ya upande wa pili wamezuia malori yetu, wao wanachotaka ni marejesho yao,” alisema Brash.

Wiki iliyopita chama hicho kilisema kimepata hasara ya zaidi ya Sh bilioni 15 kutokana na kushikiliwa kwa malori yao nchini humo.

WATINGA WIZARA YA MAMBO YA NJE

Wakati huohuo, ujumbe wa zaidi ya watu 10 wakiwamo viongozi wa chama hicho na wamiliki wa malori, jana walikwenda katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa  kujua hatima ya suala hilo.

“Tumeambiwa kwamba Serikali ya Zambia imeahidi ndani ya saa 72 suala hili litakuwa limepata ufumbuzi, tumemuomba Mkurugenzi wa Idara ya Biashara upande wa Afrika  ongeze kasi katika kushughulikia tatizo hili.

“Tunaamini mkono wa serikali ni mrefu na hatua ambazo tumeziona zikifanyiwa kazi tunaamini ndani ya saa 72 tutapata majawabu,” alisema Lukumay.  

Taarifa za ndani zinasema tangu juzi, Serikali kupitia wizara hiyo,  imekuwa na vikao na ujumbe kutoka Serikali ya Zambia kujadili suala hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles