25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

MCB: Taasisi ya fedha inayotegemewa Mbinga

mcb_bankNa AMON MTEGA, MBINGA

WANANCHI wengi wanaofanikiwa kimaisha, wakati mwingine hupata mafanikio hayo baada ya kuzitumia vizuri taasisi za fedha.

Wananchi hao wanafanikiwa pale tu wanapokuwa na uhusiano usioyumba na taasisi hizo pindi wanapokopa na kurejesha mikopo yao kwa wakati.

Pamoja na uwepo wa fursa hizo, baadhi ya taasisi za fedha nchini, zimekuwa zikishindwa
kuwafikia walengwa kwa wakati na hivyo wananchi kushindwa kupiga hatua kupitia sekta ya kilimo, ufugaji na biashara zingine za uzalishaji.

Wakati kukiwa na taasisi za fedha za aina hiyo, wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma kuna taasisi ya fedha iitwayo Benki ya Wananchi Mbinga (MCB), ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwafikia wakulima na kuwapa mikopo ya fedha kwa masharti nafuu.

Pamoja na mambo mengine, taasisi hiyo ya fedha inaonyesha nia ya dhati ya kutimiza nia ya Serikali ya awamu ya tano
iliyodhamiria kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake hivi karibuni, Kaimu Meneja wa MCB, Edwin Namnauka, anasema lengo la benki hiyo ni kuhakikisha uchumi wa mtu mmoja mmoja unakua kupitia mikopo wanayoitoa kwa wananchi.

“Sisi kwetu ni kazi tu kwa sababu tunajua bila kutoa mikopo kwa wananchi, Taifa haliwezi kupiga hatua kwani wananchi wanatutegemea pia.

“Kwa mfano, mwaka jana 2015, tulitoa mikopo kwa watu mbalimbali wakiwamo
wafanyabiashara wadogo wadogo, wakulima pamoja na baadhi ya vikundi
vya kuweka na kukopa.

“Katika mikopo hiyo, jumla ya wafanyabiashara 4,147 walinufaika na mikopo hiyo kwa sababu tulitumia kama shilingi bilioni mbili hivi.

“Kwa upande wa vikundi ambavyo ni 828, tulivikikopesha shilingi bilioni 2.6 kwa sababu huko kuna wafanyabishara ndogondogo wapatao 15,365.

“Kuna Saccos nne tulizikopesha shilingi milioni 200 na vicoba tulivikopesha shilingi milioni 106. Kwa takwimu hizo, sasa unaweza kuona ni kwa jinsi gani MCB imedhamiria kuwakomboa wananchi katika kipindi hiki ambacho Serikali inajiandaa kuufikia uchumi wa kati,” anasema Namnauka.

Kwa mujibu wa Namnauka, idadi kubwa ya waliokopa, wamebadilika kimaisha kwani maisha yao yamebadilika na sasa wanachangia kukua uchumi wa nchi.

“Tuliowakopesha wamebadilika kimaisha kwa sababu baadhi yao walikuwa wakila leo, hawajui kesho watakula nini, lakini baada ya kuwakopesha fedha, maisha yao yamebadilika na wana miradi ya kuwaendeshea maisha,” anafafanua Namnauka.

Akizungumzia jinsi ya utoaji wa mikopo, meneja huyo anasema walengwa hupewa elimu ili wajue namna ya kutumia fedha watakazokopeshwa.

“Kuna baadhi ya wanaokopeshwa wanahitaji fedha, lakini hawana uelewa wa mikopo na hawajui madhara ya kushindwa kulipa mikopo.

“Kwa hiyo, tunachokifanya kwanza ni kujiridhisha kama biashara husika ina leseni, haiharibu mazingira na inatambulika kisheria.

“Baada ya kujiridhisha na sifa hizo, tunawapa elimu na kuwaeleza kwa kina faida za mikopo na madhara ya kushindwa kurejesha mikopo yao kwa wakati,” anasema.

“Kupitia elimu tunayotoa, nina kila sababu ya kusema MCB ambayo ilianza mwaka 2003, imefanikiwa kuzalisha baadhi ya matajiri kwa kupitia mikopo yetu.

“Kwa hiyo, nawashauri Watanzania wanaoogopa mikopo, wasiogope, wakope ila wakumbuke kuirejesha kwa wakati ili wengine nao wakope,” anasema.

Kwa upande wake, Ofisa Mikopo wa MCB, Emilian Komba, anawahimiza wakazi wa Mbinga kuitumia benki yao kwa kuwa itawakomboa kimaisha.

Pia anavitaja baadhi ya vituo wanavyotolea huduma hizo kuwa ni Mbinga mjini, Mbamba Bay, Lituhi na Tingi wilayani Nyasa.

“Vituo vingine ni Kigonsera, Kindimba, Kihungu vilivyoko katika Halmashauri ya Mbinga Vijijini, Peramiho, Songea na Namtumbo.

“Pamoja na kwamba kuna baadhi ya maeneo hatujayafikia, bado tunaendelea kujipanga kwani lengo letu ni kuwahudumia Watanzania wengi kadiri tutakavyoweza,” anasema Komba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,430FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles