24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

WOCE: Taasisi binafsi inayosafisha mazingira

usafiNa TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

TATIZO la ajira limeendelea kuwa sugu nchini kutokana na Watanzania wengi kutegemea ajira serikalini badala ya kubuni mbinu za kujiajiri.

Wasomi wengi, wamekuwa wakiamini kwamba, kila wanapohitimu masomo, lazima waajiriwe serikalini au katika mashirika makubwa wanayoamini yana uwezo mkubwa kifedha.

Pamoja na imani hiyo, wasomi hao wanasahau kwamba, wanaweza kutumia elimu na maarifa waliyonayo, kujiajiri na wakati mwingine kutoa ajira kwa Watanzania wenzao.

Wakati hali ikiwa hivyo, wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, kuna Kampuni iitwayo Way Operator and Cleaners Enterprises (WOCE)  inayojishughurisha na masuala ya usafi wa mazingira huku ikiajiri watu mbalimbali.

Kampuni hiyo imesajiliwa Machi 8, mwaka huu na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni  (BRELA).

Katika mahojiano na MTANZANIA hivi karibuni, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Erick Raphael, anasema changamoto ya ajira nchini, ni kubwa na ilichangia uanzishwaji wa kampuni hiyo.

“Watanzania wengi hawana ajira na baada ya kuona tatizo hilo mkoani Mara, tuliamua kusajili kampuni yetu ili pamoja na kujikita katika usafi wa mazingira, tupate fursa ya kuwaajiri Watanzania wenzetu.

“Katika utekelezaji wa majukumu yetu, tunafanya usafi wa aina zote katika taasisi binafsi na serikalini. Tunasafisha mitaa mbalimbali mijini, tunatunza mazingira kwa kupuliza dawa za kuua wadudu pamoja na kusaidia usalama wa barabarani.

“Kwa hiyo, katika hili, tutahakikisha ndani ya miaka miaka mitatu, Watanzania wengi wanapata ajira bila kujali viwango vyao vya elimu,” anasema Raphaeli.

Pamoja na hayo, anasema kila eneo watakalokuwa wakifungua tawi, wanufaika wa kwanza ni wakazi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa Raphaeli, hadi sasa wameshaajiri watu 30 ingawa mkakati wa kuajiri watu wengi zaidi unaendelea.

Akizungumzia lengo la kupuliza dawa za kuua wadudu, Raphael anasema waliamua kuchukua jukumu hilo ili kukabiliana na magonjwa kama malaria, kipindupindu na homa ya tumbo ambayo husababishwa na uchafu wa mazingira.

“Kwa hiyo, katika jitihada za kuunga mkono kauli ya Rais Dk. John Magufuli ya kuimarisha usafi, tunatarajia kutoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi.

“Katika hili, tutawawezesha Watanzania kuishi katika mazingira bora, safi na salama kwa kupanda miti ya matunda na kivuli kwa kuwa tunajua umuhimu wake kwa binadamu,” anafafanua.

Wakati Raphael akisema hayo, Meneja wa Kampuni hiyo, Musimu Maximilian, anasema wanatarajia kutoa elimu ya usafi wa mazingira katika shule za msingi ili kuandaa mazingira ya kuwa na jamii inayothamini mazingira.

“Kimsingi, elimu ya mazingira inahitajika kutolewa katika shule za msingi kwani wanafunzi wakifundishwa na kuelewa umuhimu wa mazingira, watakuwa mabalozi wazuri wa mazingira.

“Pamoja na mikakati hiyo, changamoto tunazokutana nazo ni pamoja na jamii kutotuunga mkono katika shughuri zetu hizo.

“Kazi yetu ni kusafisha mazingira katika maeneo mbalimbali yakiwamo minadani, hospitalini, barabarani, mitaani na kwenye masoko.

“Pamoja na umuhimu wa kazi zetu, baadhi ya wananchi hawatoi ushirikiano kwa kuchangia gharama za mradi kwa sababu hawaoni umuhimu wa usafi,” anasema Maximilian.

Pamoja na hayo, anasema baada ya kufanya usafi katika mji wa Bunda, wilayani Bunda na Nyamongo, wilayani Tarime, sasa wameanza kutoa huduma hiyo jijini Mwanza.

“Kwa hiyo, tunaomba Serikali iendelee kutuunga mkono na wananchi nao watuunge mkono kwa sababu madhara ya uchafu wa mazingira yanamgusa kila mmoja,” anasisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles