33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa akagua Daraja la Kavuu Katavi

kassim-majaliwaNa MWANDISHI WETU, KATAVI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amekagua mradi wa ujenzi wa Daraja la Kavuu linalojengwa na Kampuni ya Nandra Engineering and Construction Ltd ya mkoani Morogoro na kumtaka mkandarasi huyo kulikamilisha haraka.

Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 85.34, ulianza Septemba 2013 na ulitarajiwa kukamilika Septemba 27, 2014.

Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 2.718, unagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.

“Serikali imedhamiria kuimarisha barabara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja. Ujenzi wa daraja la Kavuu utakamilika katika kipindi cha mwaka huu wa fedha, hivyo nawaomba muendelee kuiamini Serikali yenu,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Majimoto, Halmashauri ya Mpimbwe, wilayani Mlele.

“Tumeamua kuwapa kazi wakandarasi wa ndani na tunataka mfanye kazi ili daraja likamilike kwa viwango vyenye ubora ili kuthibitisha kama wasomi wetu mnafanya kazi na hatimaye tuwape kazi nyingine,” alisema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa amewata wananchi wawe makini na kujiepusha na matapeli wanaopita katika maeneo yao na kuwataka wachange fedha za kuanzisha vikundi ili wapewe Sh milioni 50 zilizoahidiwa na Serikali.

“Serikali bado hatujaanza kusambaza fedha hizo. Jihadharini na hao matapeli na wezi, wakija kwenye maeneo yenu, wakamateni.

“Zoezi hilo likianza, mtajulishwa kupitia halmashauri zenu,” aliwasisitiza.

Awali, Mbunge wa Kavuu, Dk. Pudensiana Kikwembe, alimwomba Waziri Mkuu kutoa kipaumbele kwenye ujenzi wa Daraja la Kavuu ili likamilike mapema na kuwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi.

Pia, aliiomba Serikali itekeleze ahadi ya Rais Dk. John Magufuli ya ujenzi wa barabara ya kutoka Majimoto hadi Inyonga yenye urefu wa kilomita 130 kwa kiwango cha lami.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Katavi, Abdon Maregesi, alipokuwa akizungumzia Daraja la Kavuu, alisema umekamilika kwa asilimia 50 na unategemea kukamilika Novemba 30 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles