21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wachakachuaji mizani kwenda jela miaka mitatu

augustine-mazikuNa MWANDISHI WETU, TANDAHIMBA

 MENEJA wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Mtwara, Augustine Maziku, amesema wafanyabiashara watakaobainika kutumia au kuchezea mizani ya kupima korosho watakabiliwa na adhabu ya miaka mitatu jela.

Alisema adhabu ya wakosaji bado ni ndogo kutokana na sheria kuwa ya zamani, hata hivyo alisema wataanza kutumia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela ili iwe fundisho kwa wafanyabiashara wanaotaka kujinufaisha kupitia jasho la wakulima.

Akizungumza na wakulima wilayani Tandahimba wakati wa utoaji elimu kwa vyama vya msingi kuhusu matumizi sahihi ya mizani ya korosho, Maziku  alisema sheria ya zamani iliweka faini ndogo ya Sh 10,000 ambayo hailingani na viwango vya sasa.

“Sheria hii ya zamani tutaiacha na kutumia zaidi adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela, ili iwe fundisho kwa wafanyabiashara wanaotaka kujinufaisha kupitia jasho la wakulima kama  tulivyofanya kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu  wa zao la Pamba” alisema Maziku.

Meneja huyo alisema WMA imeamua kupiga kambi Tandahimba kuhakikisha elimu za matumizi sahihi ya mizani inawafikia wakulima wengi kwa kuwa ni wilaya inayoongoza nchini kwa uzalishaji wa korosho.

“Mwezi huu wote, tutakuwa wilayani hapa kuhakikisha mizani yoyote itakayotumika kununulia zao la korosho, inahakikiwa kabla ya msimu wa ununuzi kuanza ili mkulima aweze kupata thamani ya jasho lake kupitia matumizi sahihi ya vipimo.

WMA inaendelea na kampeni yake katika mikoa ya Kanda  ya Kusini  inayolima korosho  kabla ya msimu wa korosho kuanza.

Mwaka huu tutajitahidi kuongeza elimu zaidi kwa wakulima ili kuwadhibiti baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kuchezea mizani kwa lengo la kuwaibia wakulima.

“Sheria ya Vipimo Sura 340, inatutaka tuhakiki na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara na pia kufanya ukaguzi wa kushtukiza wakati wowote ili panapokuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu uonevu katika mizani, yaweze kutatuliwa wa haraka” alisema Maziku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles