31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri wa JK alia na Lowassa

lowassa-1
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

 

* Asema wimbi lake lilimnyima ubunge 2015

Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA

HATIMAYE aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Dk. Cyril Chami, amevunja ukimya na kusema alishindwa ubunge, baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuhamia Chadema.

Dk. Chami ambaye alikuwa anagombea ubunge katika Jimbo la Moshi Vijijini kwa mara ya tatu, aliangushwa na mgombea wa Chadema, Anthony Komu aliyepata kura 55,813 dhidi ya 24,415 za kwake.

Itakumbukwa Lowassa alihama Chama Cha Mapinduzi (CCM),baada ya jina lake kukatwa na Kamati Kuu ya chama hicho mjini Dodoma.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, Dk. Chami alisema Lowassa alikuwa na nguvu kubwa kisiasa ambayo ingemsaidia kushinda ubunge kama asingeondoka CCM.

“Sababu kubwa iliyofanya nikose ubunge katika jimbo langu mwaka 2015, ni kutokana na Lowassa kuhamia Chadema, aliondoka na wapiga kura wake ambao walimwunga mkono katika mbio za urais.

“Wimbi la Lowassa kuhamia upinzani ndilo lililoniangusha pamoja na jimbo langu kuwa na viongozi watano wa vyama vikubwa vya upinzani. Yupo Philimon Ndesamburo, Edwin Mtei (Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Augustine Mrema (TLP),” alisema.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Lowassa aligombea urais kupitia Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Katika uchaguzi huo, Lowassa alipata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.97, wakati mgombea wa CCM, Rais Dk. John Magufuli aliibuka na ushindi wa kura 8,882,935, sawa na aslimia 58.46.

SOMO KWA JPM

Kuhusu utawala wa Rais Magufuli, Dk. Chami alisema umeanza vizuri na kumtaka anunue viwanda kwa fedha za Serikali kama alivyofanya katika ununuzi wa ndege mbili aina ya Bombadier Q400.

Alisema Rais Magufuli, anatakiwa ajenge viwanda kwa fedha za Serikali kama alivyofanya kwenye ununuzi wa ndege, kisha atafute wataalamu wazuri wa kuviendesha.

‘’Kama alivyofanya kwa kununua ndege kwa fedha za Serikali, ahakikishe anajenga viwanda kwa fedha zake zenyewe…hakuna kitu muhimu kama viwanda ni usalama wa nchi,.

“Akifanikiwa kujenga viwanda itakuwa njia nzuri ya kuimarisha ajira,najua wachumi wenzangu watapingana na hili lakini ndiyo njia sahihi ya kutukwamua moja kwa moja kutoka hapa tulipo,’alisema.

Alisema anaunga mkono uamuzi wa Rais Magufuli kuzuia mikutano ya kisiasa hadi mwaka 2020, kwa sababu kuna  vyama vya siasa ambavyo havina hata diwani vinataka kufanya mikutano.

‘’Nashauri vyama ambavyo havijapata udiwani au ubunge vyote vifutwe, haiwezekani hauna hata diwani halafu wewe ndiyo unazunguka Tanzania nzima kumtukana Rais…unajua walizoea wakati wa utawala wa Kikwete,’’alisema.

SAKATA LA NYALANDU

Kuhusu mvutano wake na aliyekuwa naibu wake wakati huo, Lazaro  Nyalandu juu ya kumwajibisha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),Charles Ekerege kwa madai ya kutoa msamaha kwa kampuni moja iliyokuwa inakakugua magari kutoka nje, Dk. Chami anasema suala hilo halikuwa na ukweli wowote.

“Jambo hili halikuwa na ukweli wowote, yule bwana sikuona kama amefanya kosa mahali popote,” alisema.

Dk. Chami ambaye sasa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St.John cha mkoani hapa,  alisema jambo hilo halikuwa na ukweli wowote  na lilipandikizwa ili Ekerege atolewe  kwenye nafasi yake.

“Kulikuwa na shinikizo tu la upande wa pili, walitaka wamtoe Ekerege ili waweke mtu ambaye wanamtaka wao jambo nililipinga kwa nguvu zangu zote.

“Kumbuka yule alikuwa mteule wa Rais, kwa msingi huo pale hakukuwa na mtu ambaye angeweza kutengua uteuzi wake bila idhini ya mamlaka husika.

“Nasema sijaona kosa la yule bwana…maana  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na mahakama wameshindwa kudhibitisha mpaka leo, pia kamati iliyoundwa na Bunge wakati huo chini ya mwenyekiti marehemu Deo Filikunjombe na Kangi Lugola nayo ilishindwa kuthibitisha,’’alisema Dk. Chami.

JK  

Akiuzungumzia utawala wa Rais mstaafu Kikwete, Dk. Chami alisema alikuwa mfano wa kuigwa kutokana na uvumilivu, busara na hekima.

Alisema kutokana na kuwa na sifa hizo, Kikwete aliweza kuishi vizuri na kila aina ya mtu wakiwamo wana siasa waliokuwa wanapinga utawala wake.

“Ilifikia kipindi mpaka mtu  unaogopa, unasema  tutavuka salama kweli, jamaa alikuwa na busara za ajabu akiona mambo yamebadilika anaahirisha kikao, baadae  mnarudi tena hasira zinakuwa zimepungua mambo yanaendelea na mnatoka salama,’’alisema.

Kuhusu mafanikio yake, Dk. Chami anasema moja ya mambo ambayo anajivunia ni kufanikisha mradi wa Mchuchuma na Liganga na kuwa na nembo za barcodes katika bidhaa.

“Tangu nisaidie kupatikana kwa barcodes, sasa hivi bidhaa nyingi zinauzwa nje ya Tanzania pamoja na uzinduzi wa trekta lilotengenezwa na Tanzania la Camartec,’’alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles