23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

MBINU ZA KAKONKO KUFAULISHA WANAFUNZI HIZI HAPA

Na Judith Mhina – MAELEZO


HALMASHAURI ya Wilaya ya Kakonko ilifaulisha wanafunzi 743 kati ya watahiniwa 784 na kushika nafasi ya tatu kitaifa kati ya halmashauri 178 hapa nchini.

Katika mahojiano maalumu na Idara ya Habari Maelezo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kakonko, Lusubilo Joel Mwakabibi anasema: “Shule za Serikali zimeanza kurudisha heshima ya kufaulisha kama ilivyokuwa miaka ya 1970 na 1980, mara baada ya matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka mwaka huu.”

Mwakabibi anaeleza kuwa halmashauri hiyo inajumla ya shule           za sekondari 14, kati ya hizo 11 ni za Serikali na tatu za binafsi.

Matokeo ya kidato cha nne mwaka huu yanaonesha daraja  la  kwanza shule za binafsi ni 10,  pili  35, tatu 40, nne 41 na zilizopata sifuri ni 13. Kwa upande wa shule za Serikali daraja la kwanza ni sita, pili 47, tatu 149, nne 400 na sifuri 38.

 “Siri ya mafanikio yetu ni usimamizi wa karibu na ufuatiliaji shuleni, umoja na mshikamano kati ya walimu, wazazi, viongozi wa halmashauri na ofisi ya mkuu wa wilaya; walimu wetu tupo pamoja nao, tunawatia moyo katika kazi ya kufundisha,” anasema.

Mkurugenzi huyo anasema kuwa mwaka 2016 halmashauri imeshika nafasi ya tatu kitaifa kati ya halmashauri 178 Tanzania.

“Katika matokeo ya kidato cha nne na pili mwaka 2015, halmashauri yetu ilikuwa ya kwanza kitaifa na kuzawadiwa ngao ya ushindi kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia. Anataja mikakati ya halmashauri yake kuwa ni kurudi namba moja, lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wote watakaosajiliwa kufanya mtihani wanafaulu kwa viwango vya juu na kufuta kabisa aibu ya kufeli..

Mwakabibi anasema kati ya watahiniwa 794 wa kidato cha nne, 743 wamefaulu na wanafunzi 51 tu ndio waliofeli. “Shule ambayo imeongoza matokeo ya kidato cha nne ni ya binafsi ya Mtakatifu Thomas More Kibogora, iliyotahini wanafunzi 30, matokeo ya shule mbili za binafsi matokeo yake yako sawa na shule zetu za serikali na idadi ya wanafunzi ni 55. 

“Huu ni uthibitisho dhahiri kuwa shule za sekondari za Serikali zenye watahiniwa 709 ambazo ni za kata zimefanya vizuri kama shule za binafsi,” anasema.

Kuhusu masomo waliyofaulu, Mwakabibi anasema kuwa watahiniwa wamefanya vizuri zaidi katika masomo ya Uraia (Civics), Historia, Biolojia, Kiingereza, Jiografia na Kiswahili na kubainisha kuwa ufaulu huo ni matokeo ya uwapo wa walimu wa kutosha na wenye uwezo mkubwa wa ufundishaji na kufanya kazi kwa bidii na kujituma.

“Ili tuendelee kuwa namba moja, halmashauri inasimamia walimu katika kazi zao, inawahudumia na kujali mahitaji yao.  Pia, inashirikiana na shule, wazazi, wadau wengine ili wanafunzi wajifunze kwa bidii na kwa vitendo ili wapate maarifa na kutumia elimu yao katika maisha ya kila siku. Pia halmashauri ipate matokeo bora zaidi,” anasema Mwakabibi.

Anasisitiza; “Mafanikio yetu yamechangiwa na wazazi, walimu, ofisi ya mkurugenzi, madiwani, ofisi ya mkuu wa wilaya na wadau mbalimbali kama Mpango wa Ubora wa Elimu Tanzania EQUIP-T , kwa kuunda ushirikiano wa wazazi na walimu (Parent Teachers Participation).

“Ushirikiano huu, umesaidia kuwatia hamasa wazazi kushirikiana vizuri na walimu katika zoezi zima la kuchangia chakula kwa kutoa mahindi kilo tano kila mzazi kwa muhula mmoja,” anafafanua mkurugnezi huyo na kuongeza kuwa hatua hiyo imewezesha watoto kuwa na usikivu wakati wa ufundishaji na ujifunzaji na kuongeza ufaulu.”

Akichangia utoaji wa chakula shuleni Ofisa Elimu Sekondari, Joseph Mutahaba anasema; “Kakonko imefanikiwa kutoa chakula au uji katika shule za msingi 59 za serikali. Huu ni utekelezaji wa agizo la Serikali la wanafunzi kupata chakula wawapo shuleni.

“Zoezi hili limefanikiwa baada ya kuhamasisha na kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa kuchangia chakula au uji kupitia vikao mbalimbali.”

Mutahab anatoa wito kwaa halmashauri nyingine kuhakikisha kuwa zinakuwa na usimamizi wa karibu wa taaluma shuleni, kuwajali walimu, kuwapa moyo, kuwasikiliza shida zao, kuwahamasisha wafundishe kwa bidii, ushirikiano wa karibu wa wazazi, walimu na wadau wengine wa elimu katika kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji.

Anasisitiza kuwa haya ndio miongoni mwa mambo ya msingi yatakayoboresha elimu nchini.

Tofauti na halmashauri nyingine ambazo zina shule nyingi za binafsi ambazo hunyanyua viwango vya ufaulu wa halmashauri hizo, lakini kwa upande wa  Kakonko ambayo ina idadi ndogo ya shule za binafsi, shule za Serikali zimesaidia kunyanyua kiwango cha ufaulu hadi kushika nafasi ya tatu kitaifa katika halmashauri. Ulinganisho huo umefanywa kwa kupata maelezo ya Ofisa Elimu Mkoa wa Njombe, Halfan Omary ambaye anasema katika halmashauri ya Mji Njombe shule za binafsi zilizotahiniwa ni 16; waliopata daraja la kwanza ni 58, pili 167, tatu 162, nne 168 na sifuri ni 12. Shule za serikali zipo 15 daraja la kwanza 11, pili 61, tatu 146, nne 584 na sifuri 105. Jumla ya watahiniwa ni 1538. 

Ofisa Elimu Sekondari Mkoa wa Kagera, Wandare Lwakatare anasema Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, shule za binafsi zilizotahiniwa ni 13; daraja la kwanza 133, pili 209, tatu 171, nne 188 na sifuri 16. Kwa upande wa shule za serikali ni 16; daraja la kwanza 24, pili 97, tatu 167, nne 550 na sifuri 190 jumla ya watahiniwa ni 1757. 

Ukiangalia takwimu za halmashauri hizo tatu, utagundua kuwa shule za kata za Kakonko zimefanya vizuri kuliko za kata za halmashauri ya kwanza na ya pili.  Halmashauri ya kwanza Tanzania katika ufaulu wa kidato cha nne ni Manispaa ya Bukoba; kati ya watahiniwa 1757 waliofaulu ni 1542, waliofeli 215 na kupata GPA ya 3.5414 ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Njombe ambayo ilikuwa na watahiniwa 1538 na walifaulu 1418, waliofeli 120 na kupata GPA 3.6453.

Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ndio iliyoshika nafasi ya tatu ambayo ilikuwa na watahiniwa 794 kati yao watahiniwa waliofaulu ni 743 na waliofeli ni 51 na kupata GPA ya 3.6716. Kakonko ndio halmashauri yenye wanafunzi watahiniwa wachache zaidi katika halmashauri kumi bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles