31.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

Mazoezi husaidia kujikinga na magonjwa zaidi ya 10

mazoezi-1024x682Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD.

UKIMWAMBIA mtu una dawa yenye uwezo wa kuzuia magonjwa zaidi ya kumi, kwa haraka haraka kila mtu ataihitaji dawa hiyo. Lakini mara tu utakapomwambia kwamba dawa hiyo ni kufanya mazoezi kila siku, utamwona akinyong’onyea.

Licha ya ukweli kwamba wengi wetu hatupendi kufanya mazoezi, tafiti zinaonyesha, kufanya mazoezi mara kwa mara kunaweza kukukinga na magonjwa zaidi ya kumi. Magonjwa hayo ni pamoja na kisukari, maradhi ya moyo na baadhi ya saratani. Mazoezi pia yanaweza kuzuia madhara ya kiafya yatokanayo na umri mkubwa.

Katika makala hii nitachambua magonjwa, aina ya mazoezi na shahidi za kisayansi zinazoonyesha ukweli huo.

 

SARATANI, KISUKARI, NA MAGONJWA MBALIMBALI YA MOYO

Mkusanyiko watafiti zaidi ya 40 zilizohusisha watu na nchi mbalimbali, ulibaini kwamba mazoezi huweza kuzuia magonjwa kama vile kisukari, magonjwa ya moyo na baadhi ya saratani.  Imeonekana pia kwamba, tofauti na kutokuvuta sigara, kuwa mkakamavu kwa kufanya mazoezi mara kwa mara ni mtindo wa maisha wenye faida lukuki kwa afya zetu.

Hakikisha unafanya mazoezi ya aerobics (kutembea, kukimbia, kuogelea au kuruka kamba) kwa muda usiopungua nusu saa kwa siku, angalau mara tano kwa wiki. Usisahau pia kufanya mazoezi ya nguvu (kuvuta na kusukuma uzito) angalau mara mbili kwa wiki. Ni muhimu pia kufanya mazoezi ya kunyoosha na kulainisha viungo kila siku.

 

UGONJWA WA HUZUNIKO (DEPRESSION)

Katika utafiti uliojumuisha tafiti zaidi ya 50, ilionekana kwamba mazoezi huweza kuzuia na hata kutibu tatizo la huzuniko. Tafiti hizi zimebaini kwamba, pamoja na kuongeza vichocheo vya kibailojia vya furaha mwilini, kufanya mazoezi humpa mtu fursa ya kujumuika, hivyo kupata wasaa wa kushirikiana na wengine, kitu ambacho ni muhimu sana katika kutibu tatizo hili. Mazoezi pia husaidia katika kuzuia magonjwa ya kusahau (dementia) na kiharusi.

Hakikisha unafanya mazoezi katika vikundi au clubs. Jiunge na kikundi cha mchakamchaka (jogging club) mtaani au katikamalipako pa kazi. Mazoziya aerobics yanapokuwa kama tabia, husaidia kuzuia na kutibu tatizo hili.

 

MADHARA YA AFYA YATOKANAYO NA UMRI MKUBWA

Inafahamika kisayansi kwamba umri unapoongezeka, uwezekano wa kupata magonjwa pia huongezeka. Hii ni sababu inayochangia watu wengi hata kuuchukulia uzee kama ugonjwa. Matatizo ya kiafya yanayotokana na umri mkubwa ni pamoja na kuumwa mgongo na magoti, mifupa kuvunjika kiurahisi na hata magonjwa ya kisukari, moyo na saratani.  Tafiti zimethibitisha kisayansi uwezo wa mazoezi kupunguza kasi ya kuzeeka, na kuonyesha kwamba, watu walio wakakamavu huishi maisha marefu kuliko wale wanaoishi kibwanyeye.

Zingatia kufanya mazoezi ya aerobics na yale ya nguvu kwa pamoja. Mazoezi ya kunyoosha na kulainisha viungo pia ni muhimu kama yalivyo mazoezi ya kuimarisha uwiano wa mwili au body balance. Mazoezi ya kuimarisha ‘balance’ ni muhimu katika kipindi cha uzee, kwani wazee huathirika sana na tatizo la kuanguka mara kwa mara ambako husababishwa na kukosa uwiano (balance).

 

SARATANI YA UKUTA WA UMJI WA UZAZI (ENDOMETRIAL CANCER)

 

Katika utafiti uliohusisha takribani wanawake 1400 ilibanika kwamba, kufanya mazoezi kwa saa 150 kwa wiki (wastani wa nusu saa kwa siku) kuliweza kuzuia uwezekano wa kupata saratani ya ukuta wa mji wa uzazi kwa zaidi ya asilimia 30.

Kutokana na faida zake katika kudhibiti tatizo la unene uliokithiri (obesity), mazoezi yanaweza pia kuzuia saratani ya matiti na ile ya utumbo mkubwa. Kwa ujumla mazoezi yanayo sehemu kubwa sana katika kuzuia saratani mbalimbali.

Kama ilivyoshauriwa hapo juu, fanya mazoezi ya aerobics angalau mara tano kwa wiki, kwa muda usiopungua dakika 30 kwa siku. Usiasahau kufanya mazoezi ya nguvu angalau mara mbili kwa wiki. Kumbuka, mazoezi si kwenda gym au kushiriki michezo pekee. Kutembea, kukimbia kupanda ngazi na hata kuendesha baiskeli ni mazoezi tosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles