23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Pombe za pakiti zinavyowagharimu vijana

pc-4Na Eliud Ngondo, Songwe


LICHA ya Serikali kupiga marufuku unywaji wa pombe haramu nchini, suala hili limekuwa tofauti kwa vijana wa mikoa ya Mbeya na
Songwe ambao wamekuwa wakinywa kwa wingi pombe hizo zinazoingizwa nchini kinyemela.

Pombe hizo zimekuwa zikiingizwa nchini na wafanyabiashara
wakubwa ambao si waaminifu wanaowatumia vijana kama vibaraka na kufanya udhibiti wake kuwa mgumu.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA katika
mikoa ya Mbeya na Songwe, umebaini kuwa baadhi
ya vijana wanazitumia kwa wingi na zimekuwa ni chanzo cha kuzorota kwa
nguvu kazi ya taifa.

 

POMBE HARAMU

Awali mkoa wa Mbeya kabla ya kugawanywa na kupata mkoa wa Songwe
ulikuwa unatajwa kuwa ni lango kuu  linalohusishwa na uingizaji wa
pombe haramu kutoka katika nchi za Zambia na Malawi.

Uingizwaji huo wa pombe hizo kali na ambazo ni haramu kwa mujibu wa
sheria za nchi, mikoa ya Mbeya na Songwe inaooenakana imekuwa ni sehemu ambayo vitu haramu vimekuwa vikiingizwa kwa urahisi
zaidi kuliko mikoa mingine.

Pombe hizo zimekuwa zikiingizwa kwa njia za panya kupitia vivuko
visivyo rasmi katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na Wilaya za
Ileje na Momba hasa katika mpaka wa Tunduma na kisha kusafirishwa
maeneo mengine ya mikoa hiyo pamoja na mikoa jirani ukiwemo Njombe.
NJIA ZA PANYA

MTANZANIA lilifanya uchunguzi na kubaina njia za panya zaidi ya 50
zinazotumiwa na wafanyabiashara kuingiza pombe hizo haramu.

Baadhi ya njia hizo zinazotumika kupitisha pombe hizo kwa Wilaya ya
Momba ni Mpemba, Tunduma, Nandanga, Relini na Migombani huku kwa
wilaya ya Ileje zikiwa ni Mbebe, Mapogolo, Ikumbilo, Msia,
Isongole, Bupigu na Ilondo.

Katika Wilaya ya Kyela zimebainika njia zaidi ya 30 na baadhi yake ni
eneo la Katumba Songwe, Kasumulu, Boda, Njisi, Lembuka, Kitwika na
Daraja la zamani la Mto Songwe ambapo katika maeneo hayo baadhi ya
wafanyabiashara wamekuwa wakibeba pombe hizo kwa kutumia mbinu ya
kuchanganya na mihogo ili wasishtukiwe.

Mbinu zingine zinazotumiwa na wafanyabiashara hao ni pamoja na kuwekwa katikati ya ndoo za maziwa ya mgando na hivyo kutogundulika kwa urahisi.

Vilevile katika baadhi ya maeneo inadaiwa kuwa watoto wadogo wamekuwa
wakitumiwa kusafirisha pombe hizo kwa kuchanganya na mahindi ya kusaga
ili wakionekana wamebeba mzigo wajulikane wanaenda mashine kumbe
ndio wanaingiza pombe.
Pia baadhi ya wafanyabiashara hao wamekuwa
wakiwatumia vijana wa bodaboda na waendesha baiskeli kuvusha bidhaa
hizo na kuweka pembeni mwa barabara na kuonekana kama mizigo halali
inayostahili kusafirishwa huku ikiwa imefunikiwa na majani au nguo.

Mmoja wa wauzaji wa pombe hizo haramu ambaye pia hakutaka kutajwa jina lake gazetini,
anasema pombe hizo zinaingiwa kwa wingi kutokana na njia
mpya zilizobuniwa na waingizaji.
Anaongeza kuwa pombe hizo ambazo zilikuwa zikiingizwa nchini awali zikiwa

kwenye vifungashio vya plastiki lakini kwa sasa wamebadilisha na kufungasha
kwenye chupa hali ambayo anadai kuwa ni vigumu kutambuliwa na mtu
ambaye si mtumiaji.

Anaeleza kuwa chupa hizo zinazotumika kufungashia pombe hizo
zinafanana na chupa za mafuta ya kupakaa hivyo ni vigumu kutambuliwa.

“Pombe nyingi haramu zinaletwa
zikiwa kwenye makopo ya plastiki na si kwenye viroba vya plastiki kama
ilivyokuwa awali, vina asilimia ya kilevi inayofikia asilimia 43.

“Watumiaji wa kitanzania wanapenda kutumia pombe za viroba
kutokana na kuuzwa bei ndogo tofauti na ya kitanzania, zinauzwa kwa Sh 1,000 wakati za
kitanzania zikiuzwa Sh 1,500,” kilisema chanzo hicho.
MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA

Meneja wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga,
anasema kuna changamoto kubwa kuweza kuzuia uingizwaji wa pombe
hizo nchini.

Anasema suala la viroba linapaswa kushughulikiwa na Serikali
kwa kushirikiana na wananchi ili kuweza kutokomeza uingizwaji huo kwa
madai kuwa kuiachia Serikali pekee haiwezi kutekeleza kwa ufanisi.

Anasema wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa mamlaka hiyo
kwa kutoa taarifa za watu wanaoingiza pombe
haramu kwa njia za magendo ikiwa ni pamoja na kuonyesha njia
zinazotumika katika usafirishaji wa pombe hizo.

Anasema pombe nyingi kutoka nchi jirani za Malawi na Zambia
hazijathibitishwa na mamlaka husika kama vile Shirika la Viwango nchini (TBS) na hivyo ni hatari kwa watumiaji.
MADHARA

Madhara ya matumizi ya pombe hizo zinaweza kumfanya mtumiaji aanze
kujitenga na watu kiakili na kimawazo, mtumiaji akiendelea kuzitumia
humfanya azoee na mwishowe hutumia kiasi
kikubwa kila siku.

Kuendelea kutumia pombe hizo kunachangia mtumiaji kuendelea
kupata madhara zaidi ambayo ni hatari na yanayodhuru afya yake, magonjwa ya zinaa na hata Ukimwi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles