24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

MAYANJA: MASHABIKI SIMBA ACHENI KUKARIRI

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amewaambia mashabiki wa timu hiyo waache kukariri kwamba lazima mchezaji fulani apangwe, kwani kikosi hicho kina wachezaji wengi na yeyote anaweza kutumika kutegemea na mfumo.

Kauli ya Mayanja ni jibu kwa mashabiki wa soka wa Simba ambao wamekuwa wakihoji sehemu zisizo rasmi sababu ya kiungo wa timu hiyo, Jonas Mkude, kutopangwa katika michezo kadhaa iliyopita ikiwemo Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na ile ya Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting na Azam FC.

Alisema yeye na kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, wanafahamu uwezo wa kila mchezaji  na namna ya  kuwatumia kulingana na mfumo, hivyo hakuna sababu ya mashabiki kuwa na wasiwasi mchezaji fulani anapokosekana kikosini.

“Mashabiki wanataka kuona wachezaji wanaocheza kila siku ni wale wale, inapotokea hawajawaona basi wanahoji, nawaomba watambue kila mara mfumo wa uchezaji unabadilika.

“Lengo ni kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri, kwa hiyo wasipomwona mchezaji fulani leo ujue itafika wakati watamwona tu, utaratibu huu wa kulazimisha ndio ambao umekuwa ukiigharimu timu hasa pale kocha anapokuwa hana msimamo,” alisema Mayanja raia wa Uganda.

Mayanja alizungumzia maandalizi yao kuelekea mchezo wa Jumapili dhidi ya Mwadui kwa kusema wamejiandaa kupata ushindi mnono baada ya kurekebisha kasoro kadhaa zilizojitokeza wakati wa mchezo wao dhidi ya Azam na kusababisha wapate suluhu.

“Tumeyafanyia kazi mapungufu ambayo yalijitokeza kwenye mchezo wa nyuma, hivyo malengo yetu ni kupata ushindi mnono kwa mabao yasiyopungua matatu na kuendelea.

“Tunawaomba mashabiki wawe na utulivu baada ya mchezo wa Azam kupita, kwani walitegemea tutapata ushindi mnono hivyo watambue Azam si timu ndogo, lakini kwa sasa tunawaahidi tutawapa mambo mazuri,” alisema Mayanja.

Kuhusu hali ya kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima, anayesumbuliwa na tumbo alisema anatarajia kurejea mazoezini leo kwa kuwa afya yake imeimarika.

“Niyonzima alipewa mapumziko na anaendelea vema, bila shaka kesho (leo) ataungana na  sisi mazoezini kujiandaa na mchezo dhidi ya Mwadui,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles