MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema wamechukua tahadhari zote kuimarisha ulinzi wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kutoka kwa wabaya wake, huku akieleza kuwa, mambo yaliyokuwa yanatishia uhai wake kutokana na majeraha, sasa yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Mbowe akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili jana kutokea kwenye Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya, ambako Lissu amekuwa akipatiwa matibabu tangu usiku wa Septemba 7, baada ya kupigwa risasi mjini Dodoma, alisema mbali na kuimarisha ulinzi wa Lissu, hata viongozi walio huko wako kwenye hatari kubwa, wakihofia pia usalama wao.
“Kuna usalama mkubwa kwa Lissu, tumechukua tahadhari zote za kumlinda Lissu na kujilinda sisi wenyewe kwa sababu tunawindwa, bado tuna hofu baada ya tukio la Lissu kutokea,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe hakutaka kusema aina ya ulinzi waliomwekea Lissu, licha ya gazeti kuelezwa kwamba, kwa sasa ni watu wa karibu sana wanaoruhusiwa kumuona Rais huyo wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).
Afya ya Lissu
Katika hatua nyingine, kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook, alisema: “Yale yote yaliyokuwa yanatishia pengine uhai wake (Lissu) na usalama wake yamepungua kwa kiasi kikubwa na madaktari wanatoa matumaini makubwa.
“Vile vile, sasa hivi Lissu anaweza kuzungumza, nimezungumza naye, japo bado anapatiwa matibabu na ataendelea kwenda theatre (kwenye chumba cha upasuaji) kwa ajili ya upasuaji na kutibu majeraha mbalimbali aliyoyapata.
“Mhe. Lissu hana infection ya kifua, kwa sasa yuko vizuri, yuko imara, bado ni critical lakini bado yuko stable.
“Tuendelee kumuombea kila siku, wakati wote, aweze kupona kwa haraka na kuruhusiwa kutoka hospitali,” aliandika Mbowe.
Bavicha watangaza maombi, Polisi yakataa
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick ole Sosopi, alisema wameandaa maombi ya kumwombea Lissu na Taifa kesho katika Uwanja wa TP, uliopo Sinza Darajani, Dar es Salaam.
Alisema maombi hayo yanaitwa Tanzania National Youth Prayer for Lissu.
“Jambo hili si la kisiasa, Chadema hatuna msikiti wala kanisa. Tumefuata utaratibu, tumeandika barua kwa viongozi wote wa dini ili walete watu wa maombi na dua. Isitafsiriwe tofauti kwamba tunakwenda kufanya siasa, ni viongozi wa dini ndio wataongoza,” alisema.
Sosopi alisema suala hilo tayari limepokelewa vyema na watu wa itikadi tofauti na tayari uongozi wa kiwanja hicho pamoja na Serikali za Mtaa wamewaruhusu.
“Ni maombezi ya Taifa, tunafanya maombi kila siku, lakini tumeona la Lissu linatugusa moja kwa moja, ni kiongozi wetu, hivyo kuna wanaoguswa kutoa mchango wa kuomba na kuliombea Taifa ili watu wasiojulikana wajulikane,” alisema.
Kuhusu kutoa taarifa polisi, alisema: “Hatuombi kibali, sheria inataka kutoa taarifa kwa polisi na tulifanya hivyo. Tuna imani watakuja kutulinda,” alisema.
POLISI YAPIGA MARUFUKU
Wakati Sosopi akisema hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amepiga marufuku mikusanyiko hiyo ya maombi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mambosasa alisema: “Hakuna kusanyiko linaloruhusiwa, zipo sehemu maalumu za kufanya maombi ambazo hazizuiwi kama vile makanisani na misikitini, ambaye anaweza hata kukesha kanisani akakeshe hakuna atakayewafuata.
“Lakini wakijikusanya Msimbazi wakaenda Mbagala hayo ni maandamano, kusali ni suala ambalo lipo kila siku, utaratibu wa kuabudu hautaanza kesho wala haujaanza leo,” alisema Mambosasa.
Muda mfupi baada ya polisi kutangaza marufuku hiyo, Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita, kupitia mitandao ya kijamii, alisema: “Shughuli yetu ya Jumapili haijapangwa kuhusisha wala haitahusisha maandamano yoyote kama ambavyo Kamanda Mambosasa ametafsiri.
“Tumesema wazi katika taarifa yetu kwa jeshi hilo wilayani Kinondoni, kuwa shughuli ambayo tumeiandaa inahusu maombi ambayo yatahusisha watu wa imani za dini mbalimbali,” alisema Mwita.
Alisema waumini hao hawawezi kukutana ndani ya nyumba moja ya ibada, lakini wote hao wanaweza kukutana sehemu moja ambapo patakuwa mahali pa wazi na kuomba dua kwa utulivu pamoja.
Kutokana na hali hiyo, Mwita alitoa wito wa kumsihi Kamanda Mambosasa kusoma nakala ya barua na taarifa kuhusu shughuli hiyo ambayo imepelekwa katika mamlaka za kipolisi kama sheria inavyoelekeza.
“Wakati tukiendelea na maandalizi ya shughuli, tumeitisha kikao maalumu cha dharura cha vijana wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na viongozi kitaifa wa vijana kwa ajili ya hatua za mwisho kufanikisha shughuli hiyo,” alisema Mwita.
Polisi watawanya maombi ya Bawacha
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Bavicha, Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha) Mkoa wa mpya wa Ubungo, jana walitawanywa na Polisi kabla ya kuanza kwa maombi ya kumwombea Lissu.
Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa chama Wilaya ya Ubungo, Tecla Kulanigwa, alisema askari Polisi walifika katika ukumbi wa Api Forest Kimara Baruti walipokuwa wameandaa kufanya maombi hayo.
Alisema baada ya kufika wakiwa askari saba kwenye difenda na wengine wenye silaha kwenye boda boda, waliamuru kila mwanamke aliyekuwa katika eneo hilo kuondoka.
“Waliingia mpaka chooni walipokuwa wamejificha wanawake wengine na kuwatoa,’’ alisema.
NDUGAI AWAOMBA WABUNGE KUJILINDA
Wakati huo huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, amewaomba wabunge wawe na tahadhari saa zote pindi wanapokuwa majimboni.
Kauli hiyo aliitoa bungeni jana, wakati akiahirisha Mkutano wa Nane wa Bunge la 11.
Alisema licha ya Serikali kuwa na jukumu la kuwalinda wananchi, usalama wa mtu unaanza kwake mwenyewe kabla vyombo vya ulinzi havijamlinda.
“Huko majimboni mnakokwenda nawaomba msijiachie sana na kwa wale mlio na kawaida ya kukaa baa hadi usiku wa manane, jaribuni kuwa mnarudi nyumbani mapema,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Nawaambia hivyo kwa sababu usalama siku zote unaanza na wewe, halafu ndiyo vyombo vya ulinzi vinakulinda. Tutazame nyendo zetu na pia tuwaambie wananchi wetu wawe makini na watoto wao kwa sababu kuna utekaji wa watoto unaendelea.
“Umakini kwa watoto uongezeke, wajue nani anawapeleka shuleni na pia wajue nani anawafuata shuleni,” alisema.
HABARI hii imeandaliwa na AGATHA CHARLES, LEONARD MANG’OHA na ASHA BANI, Dar Na Maregesi Paul, Dodoma.