28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

Matumaini ya Ruge kurudi akiwa hai yalivyokatika

PATRICIA KIMELEMETA Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM

RAIS mstaafu Jakaya Kikwete ameeleza alivyomfahamu marehemu Ruge Mutahaba, huku akifichua kuwa alipotolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) nchini Afrika Kusini, taratibu za kumrudisha nyumbani zilianza kufanyika.

Alisema wakati Ruge akiwa nchini humo kwa matibabu, alienda mara tatu kumjulia hali.

Kikwete akiwa nyumbani kwa baba mzazi wa Ruge, Profesa Gelas Mutahaba, alisema katika safari zake hizo za kumjulia hali alimkuta katika hali ngumu, kati na nafuu.

“Nilipata taarifa Ruge ametolewa ICU ana nafuu, taratibu za kumrejesha nyumbani zinafanyika, taarifa za kifo chake zilinishtusha mno,” alisema Kikwete.

Alisema taifa limepoteza mzalendo, kijana mahiri aliyekuwa tayari kutoa fedha zake kwa lengo la kuwaendeleza vijana.

ALIVYOMFAHAMU

Kikwete alisema Ruge na Joseph Kusaga walikuwa kama watoto wake.

Alisema vijana hao kwa pamoja walikuwa wakimshirikisha katika shughuli zao za kimaendeleo na kujiongezea kipato.

Kikwete alisema katika kipindi chote, aliweza kuvutiwa na shughuli zao na wakati mwingine walikuwa wakimshirikisha katika kutatua changamoto zao zinazojitokeza.

Alisema Ruge alimwomba msaada wa vifaa wakati alipoanzisha programu ya THT na alishiriki kuizindua.

Kikwete alisema lakini pia aliweza kumwalika kuzindua fursa wakati inaanza, jambo ambalo lilimvutia kwa sababu alikuwa akiangalia vipaji mbalimbali kutoka kwa vijana waliofika kwenye uzinduzi huo.

“Nilitamani wakati huo niweze kuwawezesha, lakini uwezo wangu ukawa mdogo. Hata hivyo akaniomba niwe mlezi wa kikundi chao,” alisema Kikwete.

NDEGE TATU KUSAFIRISHA WATU MSIBANI

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa ndege tatu zinatarajiwa kutumika kusafirisha ndugu na jamaa kuelekea Bukoba.

Hayo yalisemwa jana na Msemaji wa familia, Annick Kashaha alipohojiwa ma gazeti hili kuhusu utaratibu wa mazishi.

Alisema ndege hizo zimetolewa na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), moja ikitolewa kwa ajili ya familia na nyingine zimekodishwa.

“ATCL imetoa ndege mbili kwa ajili ya ruti maalumu ya kusafirisha ndugu na jamaa wa marehemu, na ndege moja imetolewa na Kampuni ya Precision Air ambayo inachukuliwa na marafiki,” alisema Kashasha.

 Alisema pia kuna mabasi makubwa matatu ambayo yatatumika kusafirisha ndugu, jamaa na marafiki watakaokwenda Bukoba kwa ajili ya mazishi.

“Kuna mabasi makubwa matatu yamekodishwa kwa ajili ya kusafirisha wasindikizaji wa msiba ili kwenda Bukoba, Kagera kwa ajili ya mazishi,” alisema Kashasha.

KABURI LAANZA KUCHIMBWA

Katika hatua nyingine, maandalizi ya kumzika marehemu Ruge katika Kijiji cha Kiziru, Wilaya ya Bukoba yanaendelea ambapo uchimbaji wa kaburi ulianza jana.

Pia wageni kutoka maeneo mbalimbali wanaendelea kuwasili kijijini hapo tayari kwa mazishi.

SUMAYE

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema kuwa alikuwa akifahamiana na baba yake Ruge, Profesa Mutahaba miaka mingi.

Alisema alipotembelea studio ya Clouds, Ruge alimweleza matarajio yake katika kusaidia vijana ili waweze kuchangamkia fursa zilizopo ili wazifanyie kazi.

“Taifa limepata pigo kubwa kwenye msiba huu, kwa sababu aliweza kutumia nafasi yake ili kuwasaidia vijana waweze kutumia fursa zilizopo na kuzifanyia kazi,” alisema Sumaye.

Aliongeza kuwa kujitokeza kwa idadi kubwa ya watu kwenye msiba, ni ishara tosha kuwa uwepo wake duniani ulikuwa muhimu ili vijana waweze kujifunza kutoka kwake.

LOWASSA

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alisema kuwa Ruge aliwahi kupeleka vijana ofisini kwake wakati alipokuwa Waziri Mkuu ili waweze kupatiwa ajira.

“Wakati nilipokuwa Waziri Mkuu, marehemu aliwahi kuja ofisini kwangu kwa ajili ya kuwaombea vijana ajira pamoja na mashine za kurekodi nyimbo, nilizungumza nae na aliniomba ushauri,” alisema Lowassa.

NAPE

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alisema kuwa Ruge alikuwa ni zaidi ya rafiki kwani walikuwa wanafundishana, kutofautiana na kuelewana, lakini kuna mambo mengi amefanikiwa kwa sababu yake.

Alisema wakati akiwa kiongozi wa CCM, kuna mambo ambayo yamefanyika kwa sababu ya ushauri wake.

“Nilipokuwa waziri yapo mengi ambayo niliyafanya watu wakanisifu, lakini ilikuwa ni akili ya Ruge. Lakini pia alinifuata Dodoma na kunieleza changamoto za king’amuzi, nilipokea ushauri wake na kuufanyia kazi,” alisema Nape.

BASHE

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe alisema kuwa kifo cha Ruge siyo pigo kwa taifa bali kwa tasnia ya habari ambayo alikuwa nayo moja kwa moja.

Alisema dhamira ya Ruge ilikuwa kutengeneza vijana ili waweze kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kujiendeleza.

SHONZA

Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, michezo na Utamaduni, Juliana Shonza alisema kuwa amefahamiana na Ruge muda mrefu hasa katika kazi zake za kukuza vipaji ili waweze kufika mbali.

Alisema kutokana na kazi hiyo, amekuwa na mchango mkubwa katika jamii na tasnia ya habari kwa ujumla jambo ambalo limeifanya Serikali na wananchi kupata pigo.

GONDWE

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alisema kuwa kifo cha Ruge ni huzuni kwa sababu anagusa mioyo ya Watanzania hasa alipokuwa anagundua vipaji  vya vijana na kuvifanyia kazi ili waweze kupata njia ya kuondoka kwenye umasikini.

“Ruge aliweza kugundua vipaji vya vijana na kuvifanyia kazi ili waweze kuleta tija kwa taifa, kifo chake ni pigo na kwamba kimesababisha huzuni, hata hivyo nimefanya kazi na Ruge toka 1998, leo tunasherehekea kugundua vipaji vya vijana,” alisema Gondwe.

ZAINAB

Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdalah alisema kuwa miradi mingi inayotekekezwa katika wilaya yake imetokana na mawazo ya Ruge.

RATIBA YA MAZISHI

Akitoa ratiba ya mazishi, msemaji wa familia,

Kashasha alisema mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu imekamilika, na utawasili leo saa 9:00 alasiri na moja kwa moja utapelekwa katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi (GMH) Lugalo kuuhifadhi.

“Wakati mwili upo Lugalo, tunawaomba Watanzania wajumuike nasi katika maombolezo ambapo tutakuwa na mkesha hadi asubuhi,” alisema Kashasha.

Aliongeza Machi 2, asubuhi mwili utachukuliwa na kupitishwa nyumbani mara moja, ambapo saa tano kamili utakuwa katika Viwanja vya Karimjee kutoa fursa kwa Watanzanja kushiriki kumuaga.

Alisema ifikapo Saa 9:00 mwili utaondolewa na kupelekwa Uwanja wa Ndege kuuhifadhi ili Machi 3 waweze kusafirisha kwenda Bukoba, Kagera kwa mazishi yatakayofanyika Machi 4 katika eneo la Kizilu.

“Tunaishukuru serikali kutupa nafasi ya kuaga katika viwanja vya Karimjee ili kutoa nafasi kwa Watanzania kuweza kushiriki nasi kwenye msiba huu mzito, ambapo tutaanza saa 5:00 asubuhi hadi saa tisa mchana, siku ya Jumamosi,” alisema.

Kashasha pia aliwashukuru viongozi mbalimbali wa chama na Serikali waliofika nyumbani kwa ajili ya kutoa pole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles