28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

BOT yaendesha msako maduka ya kubadili fedha

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeanza utaratibu wa kufuta leseni za maduka yote yaliyokutwa yakiendesha biashara hiyo bila kuzingatia masharti ya leseni.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya BoT kufanya ukaguzi wa kawaida wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni jijini Dar es Salaam, ambapo ilibainika maduka mengi yanaendesha biashara hiyo pasipo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni.

Mbali na hilo, mwishoni mwa mwaka jana ukaguzi kama huo pia ulifanyika jijini Arusha ambapo maduka zaidi ya 30 yalifungwa na kusababisha adha kubwa kwa watalii, wasafiri na wafanyabiashara.

Vilevile kwa mujibu wa BoT, ukaguzi huo ulifanyika pia katika maeneo yote nchini na kubainika kuwa maduka mengi hayakidhi matakwa ya kisheria ya biashara hiyo.

Kutokana na hilo, jana BoT kupitia Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania, Jerry Sabi ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kufuta leseni za maduka yote yanayofanya biashara hiyo.

Katika taarifa hiyo Sabi alisema BoT iliyaandikia maduka hayo kuyataka kutoa maelezo kwanini yasifutiwe leseni kutokana na ukiukaji huo.

“Hatua zilizochukuliwa zinatokana na tathimini ya taarifa ambazo Benki Kuu ya Tanzania ilizipokea kutoka kwa waendeshaji wa maduka hayo.

“Aidha, kama ilivyoelezwa katika taarifa za Benki Kuu ya Tanzania za Novemba 2018 na Januari 31 Januari 2019, huduma za kubadilisha fedha za kigeni zinaendelea kupatikana katika mabenki na taasisi za fedha nchini kote pamoja na maduka ya fedha za kigeni ya Shirika la Posta Tanzania (TPC).

“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutahadharisha umma kutotumia huduma zisizo rasmi za ubadilishaji wa fedha za kigeni kutokana na hatari mbalimbali, ikiwemo kuibiwa au kupewa fedha bandia.

“Aidha, utumiaji wa huduma zisizo rasmi ni kinyume cha sheria za nchi. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watoaji na watumiaji wa huduma zisizo halali (black-market),”alisema mkurugenzi huyo.

Novemba 20 mwaka jana, Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga alizungumzia kuhusu operesheni ya kukagua maduka hayo, ambapo alisema operesheni hiyo ilifanyika kwa kushtukiza baada ya uchunguzi wa miezi sita kwa maduka hayo.

 “Baada ya mashauriano na wataalamu na kushirikisha vyombo vya upelelezi na usimamizi, ilionekana ili kufanikisha kazi iliyokusudiwa ni muhimu wahusika wote wadhibitiwe kwa wakati mmoja na kufanyiwa ukaguzi,” alisema Profesa Luoga.

Akizungumzia kuhusu kutumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika operesheni hiyo, Profesa Luoga alisema walilazimika kufanya hivyo kutokana na polisi wengi kusimamia usalama katika mitihani ya kidato cha pili inayoendelea.

“Hii ilihitaji ushiriki wa maofisa wengi sana kutoka vyombo mbalimbali na kuhakikisha kila mahali ambako ukaguzi uliendeshwa kuna usalama wa kutosha na wananchi wanaarifiwa kutokuingia sehemu husika kwa wakati huo.

“Zoezi hili lilihitaji watu zaidi ya 100, kwa sababu tulihitaji kuwafikia wote kwa wakati mmoja, baadhi ya askari wa JWTZ wakiwa katika sare zao bila silaha walishiriki zoezi hili, kwa sababu siku hiyo askari polisi wengi wapo kwenye kusimamia usalama katika vituo vya mitihani ya kidato cha pili inayoendelea,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles